Hii ndio chunusi na dawa 20 zinazotibu

11Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hii ndio chunusi na dawa 20 zinazotibu

CHUNUSI ni ugonjwa wa ngozi unaojulikana kwa wengi. Huwa unajitokeza kama uvimbe au vipele vidogo hasa katika sehemu za uso, kifuani na hata mgongoni.

 Vipele hivyo hutokea wakati vishimo vya kupitisha jasho katika ngozi vinapozibwa kwa mafuta au seli za ngozi zilizokufa au wadudu, yaani bakteria.

Kwa lugha ya kidaktari, chunusi inaitwa ‘Acne Vulgaris.’ Ni ugonjwa wa ngozi unaomuathiri binadamu kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, nchini Marekani pekee, inaelezwa kuathiri watu zaidi ya milioni 17.

Chunusi inaweza kujitokeza katika umri wowote wa binadamu, lakini ina kawaida ya kuwaathiri sana vijana, hasa katika umri wa balehe (adolescence).

Dawa 20 za asili

1. Barafu; Hii ni dawa inayoweza kupunguza chunusi zionekane ndogo na kupunguza madhara yanayosababishwa.

Namna ya kutumia barafu kutibu chunusi ni rahisi na haraka zaidi. Chukua kipande cha barafu na ukipitishe sehemu zilipo na chunusi mara kadhaa kwa wastani wa dakika tatu hadi tano.

Pia, mwenye chunusi ukumbuke kusafisha vizuri uso wako, kabla ya kuanza kupitisha hiyo barafu kwenye uso wako.

2. Kitunguu swaumu; Hii inajulikana kama kitu cha kushangaza katika tiba. Huko Mashariki ya mbali, inafananishwa na miujiza.

Hiyo ni kwa sababu ina nguvu za kuua bakteria mbalimbali na kuzuia magonjwa, ikiwemo kutibu chunusi. Kuna namna mbili ya kutumia kitunguu swaumu katika tiba ya chunusi.

Namna ya kwanza ni kukitumia kitunguu swaumu kwenye vyakula vinavyopikwa kila siku na namna ya pili, ni kukitwangwa kitunguu swaumu na kukipaka moja kwa moja katika sehemu yenye chunusi.

Mbali na harufu yake isiyopendwa na wengi, kitunguu swaumu, kina uwezo wa kumpa mtu afya na urembo unaouhitaji.

Kinasaidia kupunguza ukubwa wa chunusi. Hata hivyo, unahitajika umakini, kwani kitunguu swaumu kinaweza kuunguza ngozi yako, usipokuwa makini na ili kuepuka, jaribu kuchanganya kidogo na maji baada ya kukitwanga, ili kupunguza makali yake.

3. Limau; Dawa nyingine nzuri kwa ajili ya chunusi usoni na mwilini ni limau. Hiyo inapatikana kwenye vyakula vingi, mathalan haikosekani kwenye lishe ya supu au mapishi kama ya samaki.

Limau ina kiasi kingi cha vitamini C, inayoweza kutumika kama antibaiotiki inayozuia kuongezeka na kukua bakteria wanaosababisha chunusi. Pia, ina tindikali maalumu inayohamasisha chunusi kutoka katika ngozi.

Kinachotakiwa kufanywa ni kwamba, mtu anakata limau katika pande mbili au nne na kisha anapaka maji yake taratibu kwenye chunusi, kwa wastani wa dakika 10, kisha anajisafisha na maji safi.

Tindikali katika limau inaweza kuzidhuru seli zilizopo juu ya ngozi yako, hivyo tumia dawa hiyo mara moja au mbili kwa wiki na siyo kila siku.

Vitamini C iliyomo kwenye limau husaidia kukinga mwili dhidi ya magonjwa mengi, sababu ndiyo vitamini inayosaidia kuongeza kinga ya mwili.

Kinga ni bora. Hivyo, inaaswa kutumia lishe ya vitamini C kila mara au kunywa juisi ya limau kila siku, ili kuuweka mwili katika afya bora zaidi muda wote.

4. Mshubiri (Alovera); Mshubiri au Alovera kama ilivyozoeleka na namna nzuri kwa wote wanaotaka kubaki na ngozi nyororo na ya kupendeza kila siku.

Unafanyaje? Chukua kipande cha mshubiri ‘freshi’ na ukikate, kisha chukua maji yake na kupaka moja kwa moja usoni huku ukijisugua polepole kwa muda wa kati ya dakika 15 hadi 20, kisha kujisafisha na maji safi.

Dawa hiyo inatumiwa mara mbili hadi tatu kwa wiki. Hiyo ndiyo njia rahisi ya kutibu chunusi bila kukuacha na madhara mengine mabaya.

5. Dawa ya mswaki; Dawa ya mswaki au dawa ya meno ni nyenzo nyingine ya asili mtu anaweza kutumia kujitibu chunusi. Hii inatumika usiku tu.

Pakaa kiasi fulani cha dawa hiyo kwenye chunusi iliko na kulala nayo, kisha asubuhi ajisafishe na maji safi. Hilo linaloaswa kufanyika kila baada ya siku moja, hadi mgonjwa wa chunusi anapopona.

6. Tango; Hilo ni tunda, mboga pia chanzo kizuri cha kiini cha potasiamu na vitamini nyingi ambazo zina kazi muhimu katika ngozi ya binadamu. Ina kawaida ya kuifanya ngozi ionekane laini na inayopendeza.

Tango ni mojawapo ya dawa kamili za kutibu chunusi na rahisi katika kulitibu chunusi.

Unaanza kwa kulikata tango katika vipande vidogo mfano wa slesi na kisha inabandikwa juu ya ngozi yenye chunusi. Ukumbuka kwanza kusafisha kwanza yako, kabla ya kubandika hizo slesi za tango.

Namna nyingine ni ya kusaga tango, upate juisi yake na uchanganye na sukari na kisha jisuguwe nazo kwenye ngozi yenye chunusi kwa dakika walau mbili hadi tatu na unamalizia kwa kujisafisha na maji safi.

7. Asali; Asali mbichi ya asili ni dawa nzuri sana ya kutibu chunusi. Ina antibaiotiki ya asili inayosaidia kupunguza ukubwa wa chunusi na maumivu yake.

Pia, asali inaweza kuzuia ngozi isipatwe na maambukizi mengine, ambayo yangeweza kusababisha matatizo kwenye ngozi au makovu.

Hivyo, asali inachukuliwa kama sehemu ya dawa za asili nzuri zinazotibu chunusi.

Inavyotumiwa, inaanza kwa kusafisha ngozi vizuri na maji ya vuguvugu na kisha jipake asali moja kwa moja kwenye sehemu yenye chunusi. Inaacha kwa dakika 30 na kisha jisafishe na maji safi ya vuguvugu.

Dawa hiyo inatumika ama mara mbili au tatu, ndiyo inakuwa katika nafasi nzuri ya kutoa majibu sahihi ya kitabibu.

8. Baking Soda; Moja ya sababu za kutokea chunusi katika ngozi ni kuwepo uchafu juu ya ngozi. Matumizi ya ‘baking soda’ ni moja ya njia rahisi ya kusafisha taka hizo, hivyo kuifanya ngozi ipumue vizuri.

Kimsingi, mtu akiwa na chunusi, afikiri inasaidia kubandua seli za ngozi zilizokufa na kufanya mafuta yaliyozidi kuondoka.

Ni rahisi zaidi kutumia ‘baking soda’ kutibu chunusi. Hatua zake, inaanza na kuchukua ‘baking soda’na kuichanganya kidogo na vijiko vinne vidogo vya maji au maji ya limau na mchanganyiko huo unapakwa moja kwa moja kwenye chunusi, kisha inaachwa kwa wastani wa dakika 10, ndio mhusika anajisafisha na maji ya moto.

9. Mvuke; Huo unasaidia kusafisha ngozi. Ni rahisi sana kutumia mvuke kutibu chunusi.

Mchakato wake unaaza kwa kuchemsha maji kwenye chombo kilichofunikwa na inaachwa sufuria nafasi kidogo ya mvuke kutoka.

Mtu anachofanya anachukua taulo kidogo na kisha anajifunika usoni, huku akisogelea karibu na mvuke unapokea na kuruhusu umpate kwa mbali.

Baki hapo kwa dakika tano hadi 10, huku mtu akiwa umetulia au kitaalamu hutajwa ‘relaxed.’Huu mvuke utakusaidia pia kujisikia mtulivu na kukuondolea mfadhaiko wa akili.

Mwishoni wake ni kwamba mtu ajisafishe uso wake na maji ya baridi.

10. Papai; Dawa nyingine madhubuti ya chunusi ni papai. Tunda hilo ni moja ya matunda yanayotumika kwa ajili ya urembo kwa kinamama.

Hatua zake ni papai inachukuliwa na inachanganywa na asali kidogo, linakorogwa kidogo na kisha kujipaka sehemu yenye chunusi kusugua kwa dakika 15.

Baada ya hapo, mtu anatakiwa kujiosha usoni na maji ya moto na baada ya kumalizia, arudie kujisafisha na maji baridi.

Hilo linatakiwa kufanyika kwa wastani wa mara mbili mpaka tatu kwa wiki.

11. Aspirin: Hii ni dawa. Inatajwa kuwa moja ya dawa nzuri za chunusi.

Inachofanyika ni kuchukuliwa ama vidonge viwili au vitatu vya aspirin vinavyotwangwa kupata unga wake, kisha inaongezwa maji kidogo ili kupata mithili ya uji mzito unatokanao na mchanganyiko wa dawa na maji.

Kisha pakaa mchanganyiko huo moja kwa moja kwenye sehemu yenye chunusi kwa wastani wa mara 10 hivi, kisha jisafishe kwa kutumia maji safi.

Hilo likifanyika kwa wastani wa mara moja kwa wiki, linakuwa lenye mafanikio

12. Ute mweupe wa yai; Hiyo inaweza kuchukuliwa kama njia rahisi na isiyo na gharma katika kutibu chunusi.

Kwa mujibu wa wanasayansi, kutumia mchanganyiko wa ute mweupe wa yai na maji ya limau, ni namna nzuri ya kutibu chunusi.

Changanya ute mweupe wa mayai matatu na kijiko kidogo kimoja cha maji ya limau na ukoroge vizuri. Pakaa mchanganyiko huo usoni na uache kwa dakika 15, kisha jisafishe na maji ya moto.

Hilo nalo linaloshauriwa kufanywa kati ya mara moja au mbili kwa wiki.

13. Siki ya tufaa (Apple vider Vinegar); Imo katika dawa zinazojulikana kutibu chunusi. Ina uwezo wa kurudishia tindikali katika ngozi. Bakteria wabaya, mafuta na uchafu mwingine wataondoka juu ya ngozi inayotibiwa.

Changanya siki na maji kidogo na umwagie ndani ya kitambaa kisafi kizito na upitishe kitambaa katika sehemu yenye chunusi mara kadhaa kwa dakika 10, kisha jisafishe uso wako na maji ya baridi.

14. Chumvi na mafuta ya zeituni; Mchanganyiko wa chumvi na mafuta ya zeituni (olive oil) ni dawa nyingine inayotibu chunusi.

Mafuta ya zeituni yanadhibiti bakteria na huondoa sumu vitu ambavyo vinafanya kuwa dawa nzuri kutibu chunusi na matokeo ya chunusi.

Changanya nusu kijiko kidogo cha chai cha mafuta ya zeituni na kiasi kidogo cha chumvi katika chombo kisafi. Safisha vizuri uso wako.

Kisha jipake mchanganyiko huu kwenye uso wako na uache kwa dakika 10 hivi. Mwisho jisafishe vizuri na maji ya uvuguvugu.

15. Mdalasini na asali; Mchanganyiko wa mdalasini na asali ni dawa nzuri ya kutibu chunusi.

Changanya asali vijiko vikubwa viwili na mdalasini ya unga kijiko kikubwa kimoja na kisha safisha vizuri uso wako.

Hatua inayofuatia ni kupakaa mchanganyiko huo kwenye uso usiku na asubuhi na baada ya hapo unasafisha vizuri uso wako.

16. Binzari, maziwa na asali; Hii ni jozi ambayo utengenezaji matumizi yake yanahitaji Binzari ya unga, maziwa fresh, asali, bakuli na kijiko cha chai

Hatua kwa hatua namna ya kutumia:

a)Weka kijiko kidogo kimoja cha binzari ya unga ndani ya bakuli na kisha ongeza kijiko kidogo kimoja cha asali ndani yake.

Baada ya hapo, ongeza tena kijiko kidogo kimoja au viwili vya maziwa fresh na uchanganye vizuri mchanganyiko huo upate uji mzito.

Hatua inayofuata ni kuipaka mchanganyiko huo polepole kwenye sehemu yenye chunusi na baada ya kati ya dakika tano na saba hivi na ujisafishe uso wako. Lifanye hilo kati ya mara mbili au tatu kwa wiki.

17. Uwatu (Fenugreek); Ni dawa nyingine ya asili inayotumika kutibu chunusi, unaoondoa sumu na maambukizi mbalimbali.

Hatua chache za kutibu chunusi kwa kutumia uwatu ni kwamba, chukua kijiko kidogo cha unga wa mbegu za uwatu na ongeza maji kidogo kupata uji mzito na kisha pakaa mchanganyiko huo katika sehemu yenye chunusi.

Pili, iache hiyo kwa dakika 20 au hata hadi usiku mzima na kisha jisafishe na maji safi. Hilo linaweza kufanyika kwa wastani wa mara mbili au tatu kwa wiki

18. Tumia maganda ya ndizi; Unachohitaji hapo ni kuwa tu na maganda ya ndizi yanayoandaliwa kwa kwa hatua za kumenya ndizi na ganda lake likandamizwe katika sehemu ya ndani ya ganda hilo kwenye sehemu yenye chunusi.

Hilo likifanyika, unatakiwa usubiri kwa wastani wa dakika 30 na kisha jisafishe na maji safi.

19. Parachichi na asali; maandalizi yake inahitajika kijiko kimoja cha asali na parachichi zinazoandaliwa na kutumiwa kwa hatua zifuatazo.

a) Safisha vizuri uso wako.b) Kausha na taulo au kitambaa uso wako.c) Chukua nyama ya ndani ya parachichi.d) Ongeza asali kijiko kimoja ndani ya parachichi.e) Changanya vizuri vitu hivyo viwili kupata uji mzito.f) Pakaa mchanganyiko huo kwenye sehemu yenye chunusi na kuiacha kwa wastani wa kati ya dakika 15 mpaka 20 hivi na mwisho jisafishe na maji ya vuguvugu na ujifute vizuri

20. Mtindi na asali; Hii inaelezwa kuwa dawa rahisi zaidi za kutibu chunusi.

Mahitaji yake ni: Kijiko kimoja cha asali, piakijiko kimoja cha mtindi

Unaanza kwa kuchanganya mahitaji hayo mawili vizuri na kisha kupakaa polepole mchanganyiko huo usoni.

Inapokauka, hili linarejewa mpaka mchanganyiko wote na kisha inaachwa kwa dakika 10 hadi 15 na mwisho ajisafishe na maji ya vuguvugu.

Mambo muhimu ya kuzingatia:

  1. Fanya mazoezi ya viungo kwa saa moja kila siku. 

  2. Kunywa maji mengi kila siku.

3. Ondoa mfadhaiko.4. Weka homoni sawa kama hazijakaa vizuri.

5. Kuwa msafi wa mwili wote kila mara.6. Usiziguse chunusi au kuzitoboa na mikono yako au na chochote, kuepuka makovu yasiyo ya lazima. 

Vyakula vya kuepukwa na mwenye chunusi

Epuka vyakula vifuatavyo kama unasumbuliwa na chunusi kila mara, navyo ni pamoja na:

a) Vyakula vyenye mafuta sana

b) Vyakula vinavyopikwa katikati ya mafuta mengi

c) Kahawa

d) Chai ya rangi.

e) Pombe na vilevi vingine.

f) Chokoleti.

g) Popcorn.

h) Maziwa

i) Mapera

j) Vyakula vya kwenye makopo

k) Pizza.

 

L Makala hii imeandaliwa na Fadhili Paulo, tabibu wa dawa asilia anayepatikana kwa mawasiliano ya: WhatsApp +255769142586