Hii ndiyo tohara, ufundi wake na mazito yaliyojificha ina pozembewa

29Jun 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Hii ndiyo tohara, ufundi wake na mazito yaliyojificha ina pozembewa

TOHARAnitendo la kiafya na utamaduni unaofanyika kwa njia ya kitaalamu, kuondoa ngozi ya juu ya katika sehemu ya ‘faragha’ya mwanaume, ambayo kwa asili anazaliwa nayo.

Lengo la hatua hiyo, nikumuepushia magonjwa mbalimbali yanayoweza kumpata wakati wa ukuaji wake. Mara nyingi inafanyika kwa njia za kitaalamu hospitalini, katika historia ya huko nyuma, kwa kiasi kikubwa linafanyika kwa njia za kienyeji au kimila.

Kuna jamii nyingi na hasa za Kiafrika,zilizojenga mtazamo kwamba kutahiri watoto wadogo kuna madhara kiafya utotoni na hata mtoto huyo atakapokua, sehemu hiyo ya mwili haitokuwa vizuri na kumwathiri.

Ni mtazamo unaoleta hali ya kupingana kati ya wataalamu wa afya, wakiwamo madaktaridhidi ya baadhi ya viongozi wa dini, kila upande ukielekeza hoja ya kutokukubaliana na ya upande mwingine.

Wito anaoelekeza kwa jamii watahiri watoto hata baada ya saa 24 kuzaliwa,kwakuwa mtoto anaweza katahiriwa kitaalamu kabisa, bila ya kupata matatizo yoyote.

Kutahiriwa au tohara ni utamaduni wa muda mrefu ambao ulikuwapo kabla hata ya kuja kwa Yesu Kristo, utamaduni huo ulikuwapo hapa Afrika na kulikuwa na makabila yaliyoongoza, kulingana na teknolojia waliyokuwa nayo kwa wakati huo.

Daktari Hezron Phanuel
“Ni vizuri mtoto kutahiriwa baada ya saa 24 kuzaliwa hadi siku60 za kuzaliwa muda wowote anaweza kutahiriwa. Mtoto anayetahiriwakatika kipindi hicho awe ametimiza miezi tisa kabla ya kuzaliwa na awe na uzito zaidi ya kilo mbili na nusu,” anasema Daktari wa Watoto katika Hospitali ya Mkoa Temeke, Hezron Phanuel.

Anaongeza kuwa,ilimtoto awe kwenye usalama zaidi, mara nyingi madaktari tunashauri mtoto baada ya kuzaliwa, akishafikisha saa 24, anaweza akatahiriwa kitaalamu zaidi, bila ya kumsababishia madhara yoyote kiafya, kwa uangalifu.

“Zamani tulikuwa tunatumia njia ya kukata ile sehemu ya ngozi ya juu katika uume wa mtoto, lakini siku hizi kutokana na maendeleo ya teknolojia,tunashauri zaidi njia nzuri ya kumfanyia tohara mtoto ni ya kutumia ‘kiplastiki,’japokuwa ni ghali, kwa sababu ni salama zaidi.

“Mtoto hatokwi na damu sana, halafu kukosea na kumkata vibaya, siyo rahisi,” anasema na kuongeza faida nyingine kuwa siyo rahisi kupata maambukizina haitumii bandeji pasipo maumivu makali, au kuweka kovu kidonda kinapopona.

Dk. Glory Kunambi
Daktari Glory Kunambi kutoka Hospitali ya Pugu, Dar es Salaam, anasisitiza kwambakufanyiwa tohara ni kuanzia saa 24 mpaka wiki 8 tangu kuzaliwa, kwa sharti anayefanyiwa awe na uzito kuanzia kilo 2.5 na kuendelea, pia asiwe na magonjwa mengine yoyote.

Anasema, ukimfanyia tohara mtoto huyo kwenye umri mdogo, inakuwa vyema zaidi, kwani inamuepusha kuingia katika hatari ya maambukizi ya magonjwa, kamamkojo nchafu (UTI), fangasi na magonjwa mengine ambukizi.

Ushauri wake wa kitaalamu ni kwamba, si vizuri kwa mzazi kumchelewesha mtoto kufanyiwa tohara, kwasababu namna mzazi atakavyochelewa, ndivyo inavyoletamletea shida mtoto wake.

Anaeleza kuwa ni namna ngozi ya juu katika uume wa mtoto, hujikunja na kukusanya uchafu mbalimbali unaojenga mazali ya vijidudu/bakteria mbalimbali, wanaweza kumsababishia mtoto homa kali, au madhara mengineyo, ikiwamo kwenye njia ya mkojo.

Tumeshuhudia matatizo haya mara nyingi sana wazazi wanapokuja hospitali kupata huduma, mtoto anakuwa najoto kali, au ‘UTI’ ya mara kwa mara kutokana na kutotahiriwa.

“Hivyo, tunawashauri wazazi watahiri watoto wao mapemaili kuepusha matatizo madogo madogo kama haya. Tufike wakati sasa wazazi waache dhana potofu juu ya kumtahiri mtoto mdogo kwamba itamletea shida katika ukuaji wa uume wake atakapokua mkubwa,” anasema.

Tohara inavyofanyika
Dk. Glory Kunambi, anaeleza zaidi jinsi tohara kwa watoto inavyofanyika; kwamba mhusika mkuu kitaalamu ni mtoa huduma aliyepata mafunzo ya tohara ya watoto wachanga.

Huanza kazi hiyo kwakumfanyia mtoto uchunguzi wa awali, kama anastahili kufanyiwa tohara ya watoto wachanga.

Iwapo atapitishwa kuwa anafaa kiafya, huwekewa ganzi ya maumivu kwenye uume wa mtoto, kabla ya tendo lenyewe la tohara kufanyika.

Baada ya hapo, mtoa huduma anakata ngozi husika, tendo linalofanyika kwa sekunde chache, kwa kutumia kifaa maalum kilichoandaliwa mapema.

Kwa kawaida, kidonda cha tohara hakihitaji kushonwa, hivyo sehemu hiyo itafungwa nabandeji na mtoto kurejeshwa kwa mzazi au mlezi aliyemleta.

Pastiki; Iwapo itatumika njia ya kuweka plastiki maalum, kinachokfanyika ni kwamba, itavutwa ngozi ya juu ya uume wa mtoto na kubanwa na plastiki hiyo, ikiwa na pini maalum, bila ya kushonwa.

Maendeleo yake ni kwamba, jinsi kidonda kinavyopona, ndivyo kile plastiki hiyo inavyogea hadi kudondoka.

Inashauriwa, kila baada ya wiki moja, mzazi ampeleke mtoto hospitalini,kwa ajili ya kuangaliwa na daktari kuhusu maendeleo ya kidonda hicho.

Dk. Hezron anafafanua kuwa, madhara yanayompata mtoto anapochelewa kufanyiwa tohara,ni kama vile kupata maambukizi katika mfumo wa mkojo (UTI), kuvimba ngozi ya uume na maambukizi mengine.

Kutoka kwa wadau
Mkazi wa Ilala, jijini Dar es Salaam, anayejitambulisha kwa jina la Mama Jaydan, anasema alimfanyia tohara mwanawe hospitalini, akiwa na umri wa miaka saba, pasipo kuwepo tatizo lolote la kiafya katika historia ya mwanzo.

Mama Jaydan anasema, nafasi ya maradhi yanayohusiana na mkojo mchafu, ni zao la ukosefu wa umakini, hasa kumbadilisha mtoto mavazi kila anapojisaidia.

Anaeleza uzoefu wake kwamba, wanawe wote aliwafanyia toharawakiwa na umri unaozidi miaka miwili na hawajawahi kupatwa na maradhi tajwa.
“Kama mtu hauko makini, utashangaa mtoto katahiriwa na bado anasumbuliwa na UTI,” anasema Mama Jaydan.

Anadokeza tatizo alilokumbana nalo katika suala la tohara kwa wanawe,ni vidonda kuchelewa kupona, pia maumivu makali.

Mama Jaydan Anafafanua:“Ki-ukweli, si unajua ile sehemu ni laini, hivyo kidonda cha mtoto wa miaka saba, ambaye mishipa imeshakomaa. Lazima atapata maumivu makali.

“Ila kama ningewatahiri wakiwa wadogo, nahisi wasingepata maumivu kama wanayoyapata na kidonda kingepona haraka.

Anna Rashidi, nimama aliyemfanyia tohara mwanawe, siku tatu tu, baada ya kujifungua, Aaeleza ushuhuda wake:“Mimi nilimfanyia mwanangu tohara ndani ya siku tatu baada ya kujifungua. Nashukuru mwanangu hakupata madhara yoyote, alifanyiwa vizuri na madaktari bila ya shida yoyote.

“Na ninachoshukuru zaidi, mtoto wangu toka nimetahiri, mpaka sasa ana miaka 10. Hajawahi kusumbuliwa na UTI. Nilishauriwa nimfanyie tohara mapema, ili kuepusha magonjwa mbalimbali na kweli sikupata taabu yoyote katika makuzi.”

Anaendelea: “Kuna baadhi ya wazazi wanadai kuwa ukimtahiri mtoto akiwa mdogo sana, anaweza pata matatizo ya kiafya kama uume wake kutokuwa kama unavyopaswa.

“Lakini,niwaondoe hofu kuwa, si kweli mtoto kumtahiri akiwa mdogo ni vizuri zaidi, kwa sababu anapona haraka takriban siku tatu mpaka tano, anakuwa ameshapona kabisa, bila ya tatizo na wala haihusiani na tatizo la uume, labda kama atakuwa na ‘complications’ (utata).”

Kiongozi wa kanisa mojwapo, lililoko eneo la Kitunda jijini Dar es Salaam, anashauri kwamba ni busara mtoto atahiriwe walau katika siku zisizopungua 14 na anapona, lakini ni vyema zaidi akiwa na walau miezi zaidi ya mitatu.

Hata hivyo, tohara kwa watoto wa kiume, inashuriwa kufanyika mapema ili kumuepushia magonjwa.

Faida za tohara
Inaelezwa kuwa, inapunguza maambukizi ya magonjwa ya njia ya mkojona katika kipindi cha baadaye, inapunguza uwezekano wa kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Aidha, tohara inaepusha uwezekano wa maambukizi ya saratani ya uume.

Changamoto za tohara
Moja ni kama ilivyo kwa upasuaji mwingineo, kwamba unaweza kuambatana na madhara madogo madogo, yaliorodheshwa kuwa:

• Maumivu makali baada ya kufanyika tohara,yanayoweza kupunguzwa kwa kutumia dawa ya ganzi, ambayo kwa baadhi ya watu, dawa hiyo ina madhara yake.

• Kutokwa na damu nyingi (inatokea mara chache zaidi haswa kwa wale wenye matatizo ya damu).

• Kidonda cha tohara kupata maambukizi ya bakteria, kiasi cha kuhitaji matibabu zaidi na dawa za antibaiotiki. Hata hivyo,kwatohara za watoto wachanga, madhara hayoni madogo na si mara kwa mara.

Hata hivyo, kuna umakini imechukuliwa, kwambawatoa hudumahusika, wamepewa mafunzo ya kukabiliana athari hiyo.