Hiki hapa kilichojificha nyuma ya ukeketaji uliokubuhu Serengeti

05Dec 2019
Sabato Kasika
Serengeti
Nipashe
Hiki hapa kilichojificha nyuma ya ukeketaji uliokubuhu Serengeti
  • *Kwanini hawaachi? Aanika ‘A’ hadi’ Z’

UKEKETAJI una madhara makubwa kwa mwanadamu, ikiwamo mhusika kutokwa damu nyingi, kuambukizwa maradhi iwapo vifaa vilivyotumiwa havikuwa safi, pia kuambukizwa na kuenea hadi katika viungo vya ndani vya uzazi, kumsababisha ugumba hata vifo.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu akizungumza kwenye mahafali ya wasichana walihitimu mafunzo ya ujasiriamali, waliokimbia ukeketaji. Kushoto ni Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly. PICHA: SABATO KASIKA.

Hatari nyingine ni kuambukizwa virusi vya Ukimwi wakati wa ukeketaji, kuziba mkojo na damu ya hedhi kwa kwa mwanamke, maumivu makali wakati wa kujamiiana na matatizo wakati wa kujifungua.

Ni hali inayoelezwa kumpunguzia mwanamke hamu ya kujamiiana, kuharibu umbile na kazi za viungo vya uzazi vya nje vya na madhara kimwili na kisaikolojia.

Kauli hiyo inatoka kwa Dk. Majaliwa Marwa, Mratibu wa Mradi wa Ukimwi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Maendeleo (UNFPA) nchini Tanzania.

Ingawa ukeketaji bado upo kwenye baadhi ya mikoa nchini, jitihada hizo zimechangia kuwafanya baadhi ya ngariba kuachana na kazi hiyo na kuwa waelimishaji wa jamii kuachana na mila hizo potofu.

Miongoni mwao ni Muhabe Marwa, wa mazi wa Mugumu, Serengeti mkoani Mara, anayeamua kuachana na kazi hiyo, sasa anaelimisha jamii kuacha kazi hiyo akiwa nyumba salama ya Hope for Girls and Women Tanzania.

Ngariba huyo anaweka wazi kile ambacho kimejificha nyuma ya ukeketaji na kusababisha ukatili huo kuendelea ndani ya jamii ingawa umepigwa marufuku nchini, huku wahusika wakichukuliwa hatua za kisheria.

KILICHOJIFICHA

Mama huyo anaiambia Nipashe, kabla ya mahafali ya wasichana waliokimbia ukeketaji na kulelewa katika nyumba salama, ngariba huyo anasema kuna biashara inafanywa na makundi matatu.

Anataja kundi la ngariba, wazee wa mila na wazazi wa watoto ambao wote wanafaidika na vitendo vya ukeketaji vinavyopingwa kila anayepiga vita ukatili.

Ngariba anafafanua kuna mgawo wa fedha zinazotokana na ukekeji na kwamba ndicho chanzo kikuu ya kuendelea kuwapo kwa vitendo hivyo kwenye baadhi ya maeneo ikiwamo Serengeti.

"Yaani ni kwamba, kukeketa msichana mmoja ni Sh. 30,000, na katika hizo fedha, Sh, 10,000 ni ya wazee wa kimila zinazobaki ni za ngariba, lakini wazazi wanafaidika kwa kuwaoza watoto wao waliokeketwa," anasema.

"Nilianza kazi hii mwaka mwaka 2016 na kukeketa wasichana 60, ukipiga hesabu ya kila msichana Sh.30, 000, utagundua kuna kiasi kikubwa cha fedha nilipata na kuwapa wazee wa mila sehemu yao," anasema Muhabe.

Anasema, kuna wakati gharama ya ukeketaji inaongezeka kufikia Sh. 35, 000 au 40,000 kwa kila msichana iwapo atakutwa ameshaanza tendo la ndoa.

"Kabla ya kukeketa huwa kuna dawa ya asili ambayo msichana anawekewa sehemu za siri, ili kubaini kama ameshaanza mambo ya kikubwa au bado. Kama atakuwa ameanza, gharama ya kukeketwa itaongezeka," anasema.

Muhabe anasema, hilo linafanyika kwa vile anayetakiwa kukeketwa ni ambaye hajajamiiana, lakini kwa kuwa anaunganishwa na wenzake, inabidi akakeketwe kwa gharama kubwa.

"Unaweza kudhani wazazi wa watoto hawafaidiki, lakini ukweli ni kwamba wanawatoa wakeketwe wakiamini kwamba baada ya hapo wataolewa na hivyo na hivyo kupata mahari," anasema.

Anasema, fedha wahusika wanazopata kwenye ukatili huo, ndizo zinasababisha baadhi ya ngariba na wazee wa mila kukumbatia mila ambazo jamii inazikataa sasa, hivyo elimu inahitajika kuepusha madhara kwa mabinti.

ALIVYOJISALIMISHA

Ngariba huyo anasema alianza kazi hiyo mwaka 2016, lakini mwaka uliofuata aliacha, baada ya kuelimishwa na Mkurugenzi wa taasisi ya HoPe for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly.

"Mwaka 2016 ulikuwa unagawanyika kwa mbili, hivyo nilianza kwa kukeketa wasichana 60, ila akaja Rhobi na kuniambia niache kazi hiyo nitafungwa, nimaamua kuiacha," anasema.

Anasema, baada ya hapo alichukuliwa kwenda nyumba salama iliopo Mugumu na sasa anatoa elimu kuhusu mambo ya mila na desturi kwa wasichana waliopo katika nyumba hiyo.

DC AWAPASHA

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu, alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya wasichana waliohitimu mafunzo ya ujasiriamali, wanolelewa na Nyumba Salama ya Mjini Mugumu.

Babu anawataka ngariba, wazee wa mila na wazazi kuwaacha mabinti wasome, wasiwatese na mila zao zilizopitwa na wakati.

Anaweka bayana, serikali itaendelea kupambana na wote wanaojihusisha kwa na ukeketaji wilayani mwake, akisisitiza: “Ngariba, wazee wa mila na wazazi acheni vitendo hivyo, acheni watoto wasome kwa ajili ya maisha yao ya baadaye."

"Kama mila zenu za ukeketaji zina maana, kwanini vijana wenu wanakwenda kuoa kwingine? Hebu badilikeni na msipobadilika, jueni serikali haijalala, inaendelea kupambana na mila potofu," anasema.

Hoja yake kwa Mkurugenzi wa taasisi ya Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwelly, asikate tamaa katika vita dhidi ya ukeketaji, kwa vile serikali iko nyuma yake.

"Ninajua kuna vitisho ambavyo umekuwa ukikutana navyo, katika vita hii. Wewe endelea usikate tamaa, serikali inaunga mkono juhudi zako na inataka vitendo vya ukeketaji vikomeshwe kwenye jamii," anasema.

•Kesho usikose simulizi ya ajira mapya ajira ya ngariba mstaafu.

Habari Kubwa