Hivi ndivyo vilivyo vipodozi vyenye sumu mwilini mwako

14Mar 2019
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe
Hivi ndivyo vilivyo vipodozi vyenye sumu mwilini mwako
  • • TFDA Kagera yalia na mipakani

MATUMIZI ya vipodozi visivyo salama yamekuwa yakiwaathiri wananchi na hasa kinamama, katika njia ya kutafuta kupendeza kimaumbile.

Baadhi ya wazalishaji na wauzaji wa vipodozi vya asili, katika banda lao, kwenye Maonesho ya 41 ya Biashara ya Kimataifa katika viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam. PICHA: BLOGU YA MICHUZI

Katika kundi hilo la vipodozi ambavyo baadhi ni tatizo, linajumuisha mafuta, losheni, krimu, poda, manukato, rangi za mdomoni au lipstiki.

Wataalamu wanaainisha kwamba, kuwapo vipodozi salama, pia upande wa pili kuna viambata vya sumu vyenye madhara makubwa katika miili ya watu.

TFDA Kagera

Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), imekuwa ikipambana na uingizwaji na matumizi ya vipodozi hivyo, ingawa baadhi ya wananchi wamekuwa wagumu kuviacha, kwa sababu za kutokujua na wengine wanajua.

Daniel Pyuza, Mfamasia wa Mkoani Kagera, anaeleza wanavyotumia fursa mbalimbali, zikiwamo maadhimisho ya Wiki ya Mafamasia Duniani, kuelimisha umma athari za vipodozi kwa afya yao.

Pyuza anayeiwakilisha TFDA mkoa wa Kagera katika maadhimisho hayo, anasema wanatumia nyenzo tofauti kuelimisha, ikiwamo radio, machapisho, mikusanyiko, shule na vyuo.

“Tunataka watu wapate elimu kuwa sio kila kipodozi kinafaa,” anasema na kufafanua kwamba, TFDA inawajibika rasmi kusajili, pia kudhibiti matumizi ya vipodozi nchini.

Pyuza anasema, visivyotakiwa kwa matumizi ni vipodozi vyenye viambata vya sumu na vilivyopigwa marufuku au kwisha kwa muda wake.

Anasema kuwa vipodozi ambavyo muda wake umekwisha, ni hatari kwa maana ya kemikali zilizotumika zinaweza kuwa na sumu.

Pia anataja vipodozi visiyoonyesha tarehe ya kuharibika kwamba navyo havifai, kama ilivyo kwa vile ambavyo havijaandikwa kwa lugha za ama Kiswahili au Kiingereza.

Pyuza anataja vipodozi vingi vinavyopatikana mkoani Kagera, ni losheni na krimu, ambavyo vingi vinapokamatwa vina kiambata cha sumu.

“Inaharibu ngozi, maana inaharibu kiasili ambacho hutoa rangi. Kiasili hicho kinapoharibika, mwanga wa jua unakwenda kupiga moja kwa moja kwenye ngozi na kusababisha mtu kupata madhara, ikiwamo saratani ya ngozi,” anasema.

Anaeleza namna ya kuvitambua viambata vya vipodozi, ni kuangalia lebo yake na sehemu na kukagua uwapo wa viambata kisichoruhusiwa.

“Mwananchi yeyote akikuta kipodozi anachotaka kununua kimeandikwa moja ya kiambata kilichotajwa kuwa hakifai, asikinunue na badala yake atoe taarifa TFDA kwa hatua zaidi,” anasema Pyuza.

Anafaanua kwamba, kuna kampuni nyingi zinazokwepa kuweka viambata vya kutambulisha ambavyo havijaandikwa uhalali wake, kama vinafaa kiafya au la.

“Tumeishaliona hili kama mamlaka na kwa kushirikiana na ofisi za wilaya na mkoa, tumekuwa tukifanya ukaguzi wa kushtukiza wa mara kwa mara kwenye maduka ya vipodozi, ili kubaini vipodozi ambavyo vina viambata hatari, lakini havijaandikwa,” anasema.

Madhara yakoje?
Anataja madhara ni mtumiaji anapokuwa mjamzito na Pyuza ana ufafanuzi: “Ndiyo maana inashauriwa sana, mjamzito asitumie dawa wala kipodozi, bila ya ushauri wa mtaalamu wa afya.”

Maeneo mengi yanajumuisha madhara ya kuugua saratani kama ya ngozi, maini, ubongo, mapafu, mfumo wa damu, utumbo mpana na kibofu cha mkojo.

“Madhara mengine ni uharibifu mkubwa wa ngozi, macho, ini, mapafu na figo, maana hizo kemikali ni sumu zinazoweza kusababisha kuharibu hiyo mifumo,” anaongeza.

Katika orodha hiyo, yamo madhara ya ngozi kuungua, maumivu makali, ngozi kuwa nyekundu, kutokwa vipele, kupata mzio na kuwashwa mwili mzima.

“Mhusika pia anaweza kupata magonjwa ya akili, mishipa ya fahamu hasa kichwani, uharibifu wa ubongo na mtindio wa ubongo kwa watoto wachanga na walioko tumboni.

“Hii kwa mtoto inatokana na mama mjamzito kutumia vipodozi ambavyo havifai,” anasema Pyuza, akitaja hatua za madhara ni ngozi kuwa nyembamba na laini na mwisho, mhusika anapopata jeraha au kufanyiwa upasuaji, kidonda kinachelewa kupona au kutopona kabisa.

Kuna sura nyingine, anatadharisha, kuna watumiaji wanaopata madhara kama chunusi kubwa wanashindwa kufuata ushauri wa kitabibu, wakatumia kipodozi kingine chenye madhara zaidi.

Anasisitiza kuwa tatizo la kudhibiti vipodozi lipo mkononi mwa mtumiaji, huku vingi ni batili na vinaingizwa nchini kwa ‘njia ya panya.’

Hali mipakani

“Ukienda mpaka wa Mtukula (wilayani Misenyi), kuna ofisi ya TFDA, magari yote yanayokuwa yanaingia kupitia mpaka huo yanakaguliwa, ikitokea kuna watu wamekamatwa wanachukuliwa hatua” anasema.

Anataja baadhi ya hatua zinazochukuliwa kuwa ni kuteketezwa kwa vipodozi, kupigwa faini, kifungo ikithibitika mahakamani, au vyote kwa pamoja.

Pyuza anasema, baadhi ya nchi jirani zinaruhusu vipodozi vinavyokatazwa nchini, jambo linalofanya baadhi kununua vipodozi katika nchi jirani na hawagunduliki.

Anasema, wamekuwa wakifanya ukaguzi wa kushtukiza katika maduka ya vipodozi na mengine, ambayo yamegundua kasoro hizo na wanaziuza kwa siri.

“Kuna maduka tumeyabaini na tumekuwa tukifanya ukaguzi wa kushtukiza kuondoa vipodozi hivyo na wahusika kupigwa faini. Lakini, tunaendelea na elimu kwa umma kupunguza tatizo,” anasema.

Anatoa mfano wa ukaguzi mwaka jana uliofanyika eneo la Kemondo Bukoba Vijijini, kulikamatwa vipodozi batili vyenye thamani zaidi ya Sh. milioni moja na wahusika alitozwa faini.

Pyuza anasema kuwa tovuti ya TFDA, imeorodhesha vipodozi vyote vilivyopigwa marufuku nchini na mkoani Kagera, wilaya zilizoathirika zaidi kwa vipodozi batili anavitaja kuwa ni Missenyi na Kyerwa, zilizoko jirani na mpaka wa nchi.

TFDA inavyojipanga

“Tunawaelimisha pia juu ya njia wanazopaswa kufuata, ili kusajili biashara zao na namna majengo wanayoyatumia katika shughuli zao yanavyopaswa kuwa,” anasema Nuru Mwasulana, Mkaguzi Chakula wa TFDA, Kanda ya Ziwa.

“Hapa nchini wajasiriamali wadogo ndiyo wengi, tunataka kuona wanakua kutoka walipo na kupata mafanikio makubwa zaidi hadi kufikia kuwa wajasiriamali wakubwa,” anasema.

Anasema program hiyo ni ya kitaasisi na katika Kanda ya Ziwa, watahakikisha wanafikia mikoa sita zenye jumla ya halmashauri 45.

Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Ziwa, Julius Panga, anasema mamlaka hiyo inaendesha ukaguzi wa kila mara katika kuuza vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba, ili kubaini vinavyouzwa bila usajili wa TFDA.

“Ukaguzi huu wa mara kwa mara umekuwa ukilenga pia kubaini kama watu wote wanaojihusisha na biashara za bidhaa zinazodhibitiwa, wana vibali na maeneo ya kuuzia au kuzalishia yamesajiliwa?” anasema kwamba, wamegundua mapugufu hayo.

Panga anasema, katika kipindi kati ya Januari na Juni mwaka jana, TFDA Kanda ya Ziwa, ilikagua majengo ya kuhifadhi vipodozi 287 na kubaini mapungufu makubwa.

“Katika ukaguzi huo, vipodozi vyenye uzito wa tani 93.21 vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh.milioni 165.8 vilikamatwa katika jiji la Mwanza na mkoa wa Simiyu,” anaeleza.

“Kwa mujibu wa kanuni za TFDA, mteja anayekamatwa anauza au kuhifadhi bidhaa ambazo haziruhusiwi kuuzwa kwa mujibu wa sheria, hutakiwa kutoa faini ya asilimia 25, kama tozo ya kuteketeza bidhaa husika,” anasema Panga.

RMO Kagera

Mganga Mkuu wa Mkoa Kagera, Dk. Marco Mbata, anaeleza undani wa vipodozi, kwamba ina madhara, kutokana na madini au vinasaba ilivyo navyo kuwa havifai mwilini mwa binadamu.

“Vipodozi hivi mpaka viandikwe na daktari kuendana na ugonjwa fulani ambao vinaweza kutibu. Lakini, kama mhusika amevitumia muda mrefu hata kama aliandikiwa, lazima daktari kila baada ya muda fulani awe anavikagua,” anasema.

Dk. Mbata anaeleza kemikali na madhara yake kwenye ngozi, akitoa mfano wa kumgeuza rangi mtumiaji na anaifafanua ngozi ya mwanadamu kwamba imeumbwa katika madaraja ya matatu; Ngozi ya juu, kati na chini.

Anfafanua:“Ngozi ya juu iliumbwa ili ifanye kazi ya kuzuia bakteria wakitua wanashindwa kupenya.
Kwa hiyo kutumia vipodozi, hivyo vinakwangua ngozi na hali hii inaweza kusababisha saratani ya ngozi.”

Anasema mtu anapovitumia vipodozi hivyo kwa muda mrefu, vinaweza kumpatua maradhi ya figo, kwani madini yanapomuingia, yanarundikana mwilini.

“Pia, mhusika anaweza kupata bakteria, kupatwa na vijipu uchungu, ngozi inaweza kuwa na michubuko kwa sababu zile nguvu zote zimeondolewa,” anasema Dk. Mbata.

Waathirika
Marry Michael, mkazi wa Mafumbo katika manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa watu walioathiriwa na matumizi ya vipodozi visivyo salama.

Mama huyo anasema alianza kuvitumia na kuendelea vizuri lakini baadae vilimuathiri mfano asipotumia mwili wake uliwasha, alipata vipele na ngozi kubabuka.

Anasema kuwa alipoona anapatwa na madhara hayo aliamua kuachana navyo na kuwa sasa anaendelea vizuri na ngozi yake ya asili imeanza kurudi kama awali.

“Nilivitumia kwa kuwa sikuwa na elimu juu ya vipodozi hivi, lakini nilipopata madhara na kulazimika kufika hata hospitali kupata tiba na kuambiwa niache kutumia, nikaacha,” anasema.

Mwananchi mwingine ni Jackline James mkazi wa Nshambya pia katika manispaa hiyo, anasema yeye kawaida hutumia mafuta ya mgando ya watoto, akiamini hayawezi kuwa na madhara mwilini mwake.

“Sifahamu kama mafuta haya yana madhara katika mwili wangu, kwa kuwa naona yametengenezwa kwa ajili ya watoto basi naamini hayana madhara” anasema.

Jackline anasema kuwa, elimu aliyonayo ni kwamba akiwa mjamzito, hapaswi kutumia vipodozi vya kujichubua ngozi, maana aliambiwa akijichubua itakuwa hatari atakaposhindwa kujifungua kwa njia ya kawaida, kwani akifanyiwa upasuaji, anaweza asipone kwa wataalamu kushindwa kumshona.

“Vipodozi vinaharibu ngozi ya juu. Niliambiwa hata ukipata ajali, wataalam wanaweza kushindwa kukushona na kujikuta unapata madhara makubwa zaidi au wakati mwingine kusababisha kifo” anasema.

Hivyo, Jackline, anaona elimu na ushauri vitolewe juu ya madhara yatokanayo na vipodozi vyenye viambata vya sumu, kwa kuathiri wajawazito tu, hata wasio wajawazito.

“Kuna mtu unakutana naye ngozi imejaa mabaka, hayaeleweki mpaka unaogopa, ukifuatilia utakuta katumia vipodozi visivyo salama, elimu izidi kutolewa ili watu wafahamu ni vipodozi vipi wanapaswa kutumia, kila mmoja kulingana na ngozi yake,” anasema.

Pia, Stella Charles, mkazi wa Kashai katika Manispaa ya Bukoba, anasema huangalia namna kipodozi anachotaka kununua kina nembo ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), basi maana vitu vingine hana uwezo wa kuvibaini na kama hakina hanunui.

Aidha, analalamikia lugha inayoandikwa kwenye baadhi ya vipodozi kuwa ni kikwazo, kwa kuwa baadhi zinaandikwa katika namna isiyoeleweka na baadae kuwaingiza wahusika katika madhara.

Mkazi mwingine wa Manispaa ya Bukoba, Claudia Bambanza, anasema hana uwezo wa kufahamu kuwa kipodozi husika hakiruhusiwi na kwamba anachokiona kinampendeza, kinafaa kutumika.

“Tunaathirika kwa sababu ya kutokuwa na uwezo wa kugundua kama havifai, wanaohusika na udhibiti wawe makini, maana sisi tunaona hizo ndizo bidhaa nzuri za kutumia” anasema.

Wanaume je?

Kinababa nao hawakuwa nyuma kama anavyozungumza Justine Kaijage, kuwa walio wengi wananunua vipodozi kwa kufuata harufu na marashi yenye mvuto.

“Lakini habari ya wananchi kujua madhara bado uelewa ni mdogo na ndiyo maana kuna wataalam wenye ufahamu wa haya masuala, wadhibiti ili visivyoruhusiwa kwa matumizi visiingizwe” anasema.

Anasema binafsi hawezi kuruhusu mke wake kutumia vipodozi hivyo, lakini akadai anaweza kujikuta anavitumia kutokana na kushindwa kupambanua.