Hofu ongezeko mimba kwa wanafunzi likizo ya corona

21May 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Hofu ongezeko mimba kwa wanafunzi likizo ya corona
  • *Mkoa wajipanga kila kona

UNAPOTAMKA kilio cha mimba za utotoni, hapana shaka jicho na kidole kikuu cha lawama ‘namna moja’ kiko kwa mkoa wa Shinyanga.

Wasichana wa Shinyanga wakiwa katika tamasha maalum linalowahusu. PICHA: MTANDAO

Hapo kuna mimba lukuki za watoto, vivyo hivyo kwa ndoa zao. Moja ya sababu kuu inatajwa kuwa wazazi na walezi wanatekwa na tamaa ya mbadala wa mifugo.

ALIVYOJIPANGA DC

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, hakubaliani nalo hata kidogo, nakuja na uamuzi mgumu katika eneo lake la utendaji, akiongozwa na mtazamo ‘bora lawama kuliko fedheha.’

Anatekeleza hilo kwa mtindo wa kuhamasisha mashirika na watendaji wa serikali, kuanzia kwenye kitongoji, kijiji na kata kueneza darasa wazazi na walezi waachane na ndoa za utotoni, hasa katika kipindi kilichopo ‘likizo ya corona’ walio nayo wanafunzi hivi sasa.

Tahadhari ya Mkuu wa Wilaya huyo ni kwamba, kuna uwezekano baadhi ya wazazi kutumia mwanya huo kuozesha watoto wao ndoa za utotoni, ili wapate mifugo, kwa sababu ya likizo kuwa ndefu, jambo litakalozima ndoto za wanafunzi.

“Natoa onyo kwa wazazi na walezi wasiozeshe watoto wao ndoa za utotoni katika kipindi hiki cha likizo ya corona na yule ambaye atabainika kufanya hivyo, serikali itamchukulia hatua kali za kisheria,” anaonya Mkuu wa Wilaya kwa ukali.

Anageuza uso kwa wadau akiendelea: “Mashirika ambayo mnatoa vifaa vya kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona katika maeneo ya vijijini, toeni pia na elimu ya ukatili kwa wananchi, ikiwamo wazazi wasiozeshe watoto wao ndoa za utotoni, ili shule zitakapofunguliwa wote warudi shule na kutimiza ndoto zao.”

POLISI NAO?

Mtekelezaji wa maagizo hayo ya Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama Wilaya, Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Shinyanga, Debora Magiligimba, anavalia njuga mimba na ndoa za utotoni, akiwa mahsusi na kitendo cha wazazi kuogesha watoto wao dawa za mvuto wa kimapenzi.

Anaeleza, mtazamo wa wana Shinyanga unazama mbali katika kupata wachumba, ili waozeshwe kwa mbadala wa mifugo kwa wazazi na walezi.

"Nilipokuja hapa mkoani Shinyanga mwishoni mwa mwaka jana (2019), kulikuwa na tatizo la mauaji yatokanayo na imani za kishirikina, ambalo nimelipunguza na kubakia tatizo la mimba na ndoa za utotoni, hasa katika Wilaya ya Kishapu.

"Ikabidi nikae na viongozi wa dini, watendaji wa vijiji na kata kuzungumzia tatizo hili, nikaambiwa tatizo kubwa ni mila na desturi za uogeshaji watoto wa kike dawa za mvuto wa kimapenzi, pamoja na mnada kuwa kichocheo cha ngono zembe," anafafanua Kamanda.

Pia, anawaonya wote ambao ama watawapatia ujauzito wanafunzi na kuwaozesha ndoa za utotoni, jeshi hilo halitakuwa na huruma nao, wataangukia mikono ya sheria.

Davis Msangi ni Mkuu wa Upelelezi (RCO) mkoani Shinyanga, anajazia hoja hiyo kwa tahadhari kwa wazazi, akiwataka wasiwaozeshe watoto wao katika umri mdogo, ili waweze kutimiza ndoto zao, pia tahadhari zao kiafya.

Kwa mujibu wa Sheria ya Elimu ya Mwaka 2002, pia Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya Mwaka, inamwingiza kwenye kifungo cha muda mrefu, mtu anayethibtika kushiriki ngono na ama binti mwanafunzi au anayeangukia umri chini ya miaka 18.

MTEKELEZAJI KAMPENI

John Myola, Mkurugenzi wa Shirika la Agape, mtekelezaji wa mradi wa kutokomeza mimba na ndoa za utotoni katika Halmashauri ya Wilaya za Shinyanga na Kishapu, anasema katika kipindi kilichopo wanafunzi wakiwa likizo.

Kwa mujibu wa mkuugenzi huyo, hivi sasa wanalenga kujikinga na maambukizo ya virusi, wakipitia elimu ya kuzuia mimba kwa wanafunzi.

Anasema, wataanza kutoa elimu hiyo katika Kata ya Mwamala, ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, eneo wanakotekeleza mradi wa kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, kuwalinda wanafunzi ama wasipate au kuozeshwa.

“Shirika letu la Agape, mbali na kuanza kutoa elimu kwa wananchi ya kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona na kugawa vifaa vya kujikinga.

“Pia, tutakuwa tukitoa elimu kwa wazazi ya kuacha kuozesha watoto wao ndoa za utotoni, bali wawaache wasome ili watimize ndoto zao na kuja kuwasaidia hapo baadaye,” anaeleza Myola.

“Katika kipindi hiki cha janga la maambukizo ya virusi vya corona tukiendelea kukaa kimya na kutopiga kelele, tutajikuta shule zikifunguliwa watoto wengi wasiende shule sababu ya kupewa ujauzito au wengine wameshaozeshwa na wazazi wao ndoa za utotoni,” anaongeza.

OFISA USTAWI

Ofisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Shinyanga, Lidya Kwesigabo, anaonyesha shaka kwamba katika ‘likizo ya corona’ huenda kukatokea ongezeko la ujauzito na ndoa za wanafunzi, sababu ni usimamizi duni, akidai mabinti kuzurura ovyo mitaani.

Anasema uzururaji ovyo wa watoto mitaani hasa kwa watoto wa kike wanakuwa katika hatari kubwa ya kupewa mimba, sababu kuu ni kukosa uangalizi, huku wazazi wanajawa na tamaa ya mifugo, kwa kuwanadi mabinti kwa wanaume, hawapo tayari kuwaona nyumbani muda wote.

“Nimeagiza maofisa ustawi wa jamii kila wilaya mkoani hapa, kutoa elimu kwa wananchi hasa katika kipindi hiki cha wanafunzi, ambao wapo katika ‘likizo ya corona’ watoe elimu ya wazazi, wasiozeshe watoto ndoa za utotoni, pamoja na kuondoa watoto wote wanaozurura ovyo mitaani,” anasema Lydia.

WADAU

Katibu Mpango Mkakati Kitaifa wa Serikali wa Kupunguza Ukatili wa Kijinsia Dhidi ya Wanawake na Watoto Mkoa wa Shinyanga (Mtakuwwa), Tedson Ngwale, anasema mkakati uliopo serikalini ni kuendelea kupunguza mimba na ndoa za utotoni na elimu kwa jamii, kuhusu madhara yaliyopo.

Ngwale anataja takwimu za mimba za utotoni Shinyanga kuanzia mwaka wa fedha uliopita (Julai 2018 hadi Juni 2019), kuna watoto 168 waliopewa mimba na kuacha masomo.

Anataja mgawanyiko wake, kuna jumla ya shule za sekondari 161 na msingi saba na katika mwaka huohuo wa fedha, jumla ya wanafunzi 32 wameolewa ndoa za utotoni na kubainisha kuwa hofu yake kwa mwaka huu (2020) huenda takwimu zikaongezeka.

Katibu Mipango huyo, anaelekeza hofu ya watoto watakaa nyumbani kwa muda mrefu nyumbani, inaweza kuwaacha pabaya.

Habari Kubwa