Hoihoi kupata bomba waliochangia maji na wanyama visima kata jirani

10Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Kahama
Nipashe
Hoihoi kupata bomba waliochangia maji na wanyama visima kata jirani
  • Mfadhili: Vuta nyumbani, mtunzaji wewe
  • Mama kuamka alfajiri, binti mimba ‘stop’
  • Zahanati kupumua wagonjwa wa kuhara

SERIKALI imekuwa ikipambana kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na binafsi katika kuwapelekea wananchi walio pembezoni mwa miji huduma ya majisafi na salama.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha, akikinga ndoo ya maji ya mkazi wa Kata ya Iyenze, katika uzinduzi wa mradi wa maji uliojengwa na World Vision Tanzania. PICHA: SHABAN NJIA.

Katika utekelezaji, inachimba visima virefu na vifupi ikiwa na kuwajengea maghati ya maji, yanayotumiwa na wananchi kujikimu dhidi ya adha ya kukosa maji, ili kama namna ya kupisha visima vya kienyeji au madimbwi ambavyo sio salama kiafya.

Wananchi nao wamekuwa wakijitahidi kuchimba visima kwenye maeneo yanayopatikana maji kirahisi, lakini mwisho wake visima hivyo vimekuwa vikikauka kutokana na shughuli za kibinadamu.

Kutokana na baadhi ya vijiji na kata kuwa na changamoto ya majisafi na salama, wananchi wake wamekuwa wakitumia maji yaliyotuama madimbwini, wakichangia na mifugo, hata kuwasababishia ongezeko la magonjwa ya kuambukiza, kama ya kuhara.

Hata asilimia kubwa ya maradhi yanayoripotiwa katika zahanati vijijini na vituo vya kata, mengi yanayoongoza ni yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.

Wadau wanena

Kutokana na changamoto hizo, Shirika lisilo la kiserikali la World Vision Tanzania, wilayani hapa mkoani limejenga mradi wa maji wa kutumia umeme wa jua unaotoa zaidi ya lita 5,350 za maji, kwa matarajio ya kuwahudumia wananchi zaidi ya 30,000 katika kijiji na kata ya Iyenze ndani ya Halmashauri, iliyoko katika mji wa Kahama.

John Massenza, ni Meneja wa Shirika lisilo la kiserikali la World Vision Tanzania, Kanda ya Ziwa, anasema wamechimba kisima katika kijiji na kata ya Iyenze, ambako kitawahudumia wananchi hao maelfu.

Anasema, lengo la mradi pia ni kuwahudumia watoto zaidi ya 10,000 ambao kwa asilimia kubwa, ndio walikuwa wakitaabika na maradhi yatokanayo ya matumizi ya maji machafu na itasaidia kuhudumia kituo cha afya na taasisi za elimu.

Masenza anasema, mradi huo wa kutumia umeme umegaharimu Sh. milioni 150 na unawagusa kinamama kwa kuwanusuru kuamka alfajiri kwenda kata jirani kutafuta huduma ya maji.

Unalindwaje? Meneja huyo anasema, ili mradi usife ni vyema serikali ya kijiji ikaanzisha utaratibu wa kisheria ya wananchi kuchangia japo gharama au tozo kupitia ndoo za maji wanazochota na ikitokea tatizo, wanawajibika kurekebisha.

Masenza anafafanua kuwa, miradi mingi inakufa baada ya wahisani kuikabidhi kwa wananchi na chanzo kikuu kinatokana na usimamizi mbovu wa mradi.

Kwa mujibu wa Masenza, lengo la mradi ni kuhakikisha maji yanafika sokoni au magulioni na taasisi za elimu.

Mratibu Mradi

Mratibu wa mradi, Machibya Mwalla, anasema kila mwananchi anatakiwa kuvuta maji nyumbani kwake, kwani lita za maji zinazopatikana ni nyingi sana, kulinganisha kiasi cha wakazi hao.

Mbali na hiyo, ansema maji hayo yatapatikana muda wote na matarajio ya sasa ni kuyapeleka katika Kituo cha Afya cha Iyenze na shule za msingi na sekondari zilizopo katika kijiji na kata ya Iyenze.

Anasema, mradi kwa sasa uko chini ya serikali ya kijiji na matarajio ni kuona kila mwananchi ananufaika nao, huku akisisitiza haya ya kila mmoja kuwa mlinzi wa mradi, kunusuru wasio na nia njema wakaiba mfumo wa umeme wa jua na miundombinu mimgineyo.

Watumia maji

Monica Jefta, ni mkazi wa kijiji cha Iyenze, anayesema walikuwa wanatembea umbali mrefu kutafuta huduma ya majisafi na salama kwa zaidi ya kilomita 20 kwenda kwenye kata za jirani kutafuta maji.

Anaeleza uzoefu wa walikotoka, waliamka alfajiri wakiwaacha waume na watoto majumbani, kwenda maji na wakati mwingine walilazimika kutumia maji ya mashimoni na madimbwi, wakichangia na mifugo yao ambayo, hali anayosema ilihatarisha afya zao.

“Ndoa zetu ziliingiwa na mashaka pale tulipokuwa tukiamka alfajiri na kwenda vijiji vya kata ya jirani kwenda kutafuta huduma ya maji na wakati mwingine wenzetu waliingiwa na wasiwasi na kutishia kutuacha na tukiacha kutafuta maji hakuna kupika wala kupakua,” anasema Monica.

Pia anasema kuwa, kuna wakati walilazimia kuwaachisha shule watoto na kutoendelea na masoko kwa siku moja ili kwenda kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, jambo lililokuwa linamnyima mtoto kusoma kwa kipindi ambacho ndani ya maji yanakuwa yamekwisha.

Samson Mabula, anasema kitendo cha wake zao kuamka alfajiri kwenda kutafuta huduma ya maji kilikuwa kinawatia wasiwasi mkubwa juu ya usalama wao na kuhofiwa, kusalitiwa kwenye ndoa huku wengine wakidiriki kuvunja miji yao.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mayala Jagadi, anasema walikuwa wanashambuliwa na maradhi yanayotokana na kutumia maji ambayo sio safi na salama kutokana na kutumia maji ya mitaroni na madimbwi yanayotumiwa na mifugo.

Mayala, anasema kukosekana kwa maji pia kulisababisha kijiji chao kuwa na ongezeko la mimba kwa wanafunzi na watoto wao, walitumia kufanya matendo hayo wanapokwenda kutafuta huduma ya maji kwa zaidi ya kilomita 20.

DC Kahama

Anamringi Macha, ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, anayesema kupatikana kwa huduma ya maji karibu, kutasaidia ongezeko la uzalishaji na shughuli za kijamii, kutokana na wakati waiotumia wanajamii wake na hasa kinamama, walielekea kutafuta maji.

Mkuu wa Wilaya anaeleza matazamio kwamba, afya za wananchi zitaimarika, tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyumba na kuongeza maji ambayo kwa sasa yanatumika yamepimwa na kuthibitishwa hayana madhara na yanafaa kutumiwa.

Pia anasema sambamba na hilo, afya za watoto waliodhoofika na wengine kudumaa kutokana na kushambuliwa na magonjwa mengi zitaimarika.

Anarejea kauli ya viongozi wa World Vision, kwamba hivi sasa kila mmoja anapaswa kutunza mradi usiharibike, jambo linaloweza kuwahatarisha warejee kutumia maji ya visima vya kenyeji, kama walikotokea awali.

Pia anaunga mkono wanakijiji na kata ya Iyenze, kuchangia gharama za matumizi ya maji, ili wahisani World vision Tanzania inapoondoka, mradi ujiendeshe na kuondokana na dhana ya pindi utakapoharibika watarekebishiwa.

“Hatutaki kurudi nyuma kutumia maji tena na wanyama wetu ambao tunawafuga. Tuutunze mradi wetu kama dhahabu usije ukaharibika na kuanza tena kinamama kutembea umbali mrefu kutafuta maji na ikiwezekana wekeni tozo za kisheria, ili ikitokea tatizo tuweze kukarabati,” anasema Macha.

Mkuu wa Wilaya anasema, serikali kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo, wataendelea kutoa huduma ya majisafi na salama katika maeneo yote vijijini na kata ambazo zina changamoto za huduma hizo.

Hivi karibu, serikali ilianzisha huduma ya maji vijijini, ambazo watajihusisha na upelekeaji maji katika vijiji vyote vyenye changamoto ya ukosefu wa majisafi na salama na kusaidia kupunguza adha kwa wananchi wanaochangia maji na wanyama.

• Soma ripoti maalum Uk. 18.

Habari Kubwa