Hongera Rais kuleta vigezo vipya vya uongozi

28Feb 2016
J.M. Kibasso
Nipashe Jumapili
Hongera Rais kuleta vigezo vipya vya uongozi

Hivi karibuni Rais John Magufuli alibainisha baadhi ya vigezo vitakavyotumika katika uteuzi wa wakuu wa mikoa na wilaya unaotarajiwa kutangazwa javascript:void(0);wakati wowote.

Rais Dk. John Magufuli.

Vigezo hivyo ni pamoja na namna wakuu hao wa mikoa na wilaya wanavyokabiliana na kero kama ugonjwa wa kipindupindu, njaa, migogoro ya ardhi na upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari katika maeneo yao.

Katika kusisitiza vigezo hivyo, Rais JPM alinukuliwa akisema ni aibu sana kukaa kwenye ofisi nzuri, kulala kwenye nyumba nzuri na kutembelea gari nzuri wakati jirani kuna wanafunzi wanakaa chini.

Sipendi kuonekana kuwa mnafiki, mchonganishi wala mroho wa madaraka, isipokuwa kwasababu hoja hii imeletwa na kiongozi wa juu, hivyo sioni kama itakuwa ni dhambi wananchi wa kawaida pia wakapata fursa kutoka dukuduku zao.

Ni kweli changamoto hizi zipo kwani kila uchao ni kilio cha upungufu wa madawati, madarasa, kuzuka kwa kipindupindu, mapigano kati ya wafugaji na wakulima, wezi wa mifugo, njaa na mengine yanayofanana na hayo.
Swala la kujiuliza ni je, ni nani alaumiwe kati ya wananchi na viongozi wa serikali?

Nianze kutoa mchango wangu kwa kumpa pongezi Rais JMP kwa kuibua hoja hii muda muafaka kwasababu tawala za awamu zote zilizopita zilishindwa kuona ukubwa wa kero hizi na hivyo kufanya utatuzi wake kuwa vigezo vitakavyowafaulisha wakuu wa Wilaya, Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri kuingia kwenye uongozi.

Bila shaka hata Rais Magufuli anazijua sababu ambazo zimetufikisha hapa tulipo. Na ndiyo maana alikuja na falsafa ya “Hapa kazi tu”.

Sababu zipo nyingi lakini kubwa ni mazoea ya kuleana, kubebana, kuoneana haya, kujifanya macho hayaoni, sikio halisikii lakini kubwa zaidi ni mazingira ya uteuzi wa viongozi.

Wahenga walinena “Mtoto wa nyoka ni nyoka”. Naomba nimwambie Rais Magufuli bila kumun’unya maneno kwamba uteuzi wa viongozi umegubikwa na uswahiba na undugu. Mteule ambaye ni mtoto wa mkubwa fulani serikalini au kwenye chama haogopi chochote kwasababu ana kinga.

Nitoe mfano hai: hivi karibuni Rais alimteua Waziri Mkuu asiye na jina kubwa na kwa kweli kazi yake inaonekana katika utekelezaji wa falsafa ya “Hapa kazi tu”.

Rais JPM akitaka kero hizi zipungue, asihangaike kutafuta mchawi kwani wateule watokanao na wazazi wenye majina makubwa ndio tatizo. Arudi chini ambapo kuna viongozi wazuri, lakini hawavumi.

Sipingani na utaratibu wa zamani uliozoeleka wa kuteua wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kutokana na majina makubwa la hasha, bali ninachotaka kusema ni kwamba sifa na vigezo vya kumwezesha mtu kuteuliwa, visiegemee tu kwenye watoto wa vigogo wenye majina makubwa.

Namwomba Rais JPM akitaka kero hizi ziishe, awaibue viongozi wasiokuwa na majina makubwa kwani watu, pia, wamechoka kusikia majina yale yale siku zote. Nchi hii ni ya wote kwanini wachache ndio wawe “wateule” wa kuongoza nchi.

Hivyo zoezi aliloanza Rais JPM kuibua vipaji vya viongozi wasiofahamika, lisiishie katika uteuzi wa Waziri Mkuu tu na Mawaziri bali liwe endelevu hasa katika ngazi za wilaya na mikoa.

Hata hivyo, lazima niseme kuwa wananchi pia wana mchango mkubwa wa kusaidia serikali kufikie malengo yake.
Kama alivyobainisha Rais Magufuli hivi karibuni wakati akizungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, Watanzania pia wanatakiwa kujipima kwa kujiuliza wameifanyia nini nchi yao.

Rai hiyo ya Rais ni mwiba unaochoma; ni sawa na kusema 'sheria ni msumeno'. Bila shaka ujumbe wake umefika kwa walengwa kwa sababu serikali pekee haiwezi kupunguza kero zote bila kupata msaada kutoka kwa wananchi.

Hata agepatikana kiongozi kutoka mbinguni, bila kupata ushirikiano kutoka kwa wananchi hakuna analoweza kulifanya.

Ifike mahali na sisi tujiulize tumeifanyia nini nchi. Tutambue kuwa hakuna mtu kutoka nje ya nchi atakayekuja kutuondolea kero hizi za upungufu wa madawati katika shule za msingi na sekondari zetu, njaa, migogoro ya ardhi.

Kila tunapoamka tujiulize, mchango wetu unagusa vipi taifa. Hakuna kisichowezekana kama tukisema “Nchi hii ni yetu sote”.

J.M. Kibasso
Mob: 0713 -299 044 / 0767 399 004
Email: [email protected]

Habari Kubwa