Huu hapa ujasiriamali na ubunifu wake ulivyo

17Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Huu hapa ujasiriamali na ubunifu wake ulivyo

NI vigumu kujadili ujasiriamali, pasipo kuelewa maana yake halisi. Wataalamu wanautafsiri kwamba ni mchakato au utaratibu wa kubuni au kuandaa, kuanzisha na kisha kuendesha biashara mpya. Hivyo, mbunifu huyo ndiye anayeitwa mjasiriamali.

Wajasiriamali wakiwa kazini. PICHA: MTANDAO.

Pia, wanazuoni wanautaja kuwa ni uwezo wa uthubutu wa kuendeleza, kupanga na kusimamia biashara pamoja na changamoto zake za hasara, katika safari ya kusaka faida.

Na ili kufanikiwa, wataalamu hao wanasema kuna kanuni kadhaa za kuzingatia. Kwanza, anatakiwa awe mbunifu ambayo ni kanuni muhimu kwa kila mjasiriamali. Ubunifu hauishii kutengeneza, bali maboresho ya vitu unavyotengeneza.

Ubunifu huo, una sura kuu tatu; ubunifu katika kuendeleza na kuboresha bidhaa au huduma iliyoko sokoni, ubunifu katika kuzalisha kipya, kwa kuzingatia hitaji la soko na ubunifu katika uendeshaji biashara tajwa.

Kanuni ya pili ni nidhamu; mjasiriamali lazima athamini kazi yake, muda na pesa inayopatikana, akifanya hilo kwa kujinyima na kujibana, kufikia malengo makubwa kikazi.

Tatu, ni budi awe sehemu ya shughuli zake na mahitaji ya bidhaa au huduma hiyo katika eneo hilo kwa kwa wateja wake, katika eneo unakofanya shughuli zake.

Mfano huwezi kuuza bidhaa, ambayo katika mahali husika ni marufuku. Ni lazima eneo hilo liwe na uhitaji wa huduma au bidhaa inayotakiwa.

Nne, bidhaa au huduma husika inapaswa iendane na thamani ya bidhaa au huduma, maana bei ya bidhaa au huduma inaweza kumvuta mteja au kumfukuza. Ni lazima bei ilingane na thamani ya huduma au bidhaa, pia nguvu za kiuchumi za wateja.

Tano, matangazo ya bidhaa au huduma kwa mjasiriamali, lazima yahakikishe yanatengeneza mtandao wa wateja kujua bidhaa au huduma iliyoko sokoni, kwa njia mbalimbali zinazofaa.

Haitoshi kama mjasiriamali kutengeneza bidhaa nzuri au kuwa na huduma nzuri, lakini jirani zako hawajui na hawana taarifa ya bidhaa yako au huduma yako ndio maana unaona matangazo ya biashara kwenye vyombo vya habari Tv na redio kila mara.

Ndio maana unaona nchi yetu inajitahidi kutangaza vivutio vya utalii huko kwenye nchi zingine ili waujue Mlima Kilimanjaro upo Tanzania, mbuga za wanyama wa kila aina na kadhalika wanasema ‘biashara ni matangazo.’

Mjasiriamali lazima utangaze bidhaa yako au huduma yako kwa njia yoyote ili iwafikie wateja wengi kadri iwezekanavyo.

Maneno ya hamasa na kutiana moyo na historia za watu waliofanikiwa za kutokata tamaa, kujituma, kujiamini, sijui nini haya yote yakuwa na umuhimu na faida pale utakapokuwa umetimiza kanuni za ujasiriamali na biashara yako ili usipoteze fedha zako na mikopo ukauziwa dhamana zako bure.

•Kwa mujibu mtandao

Habari Kubwa