Idara ya Uhamiaji na mwarobaini janga wahamiaji haramu nchini- 2

16Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
Musoma
Nipashe
Idara ya Uhamiaji na mwarobaini janga wahamiaji haramu nchini- 2

WIKI iliyopita, tulianza kuona namna Idara ya Uhamiaji inavyokabiliana na changamoto mbalimbali katika mipaka, hasa za wahamiaji haramu wanaoingia nchini bila vibali vya kuishi, kinyume cha sheria.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala (mwenye kipaza sauti).PICHA: MTANDAO

Tuliishia pale ambapo Msemaji Mkuu wa Idara hiyo Ally Mtanda, alipofafanua athari za wahamiaji haramu kwa taifa baadhi zikiwa ni kuhatarisha usalama wa wananchi na ongezeko la uhalifu kama vile ujambazi.

Leo msemaji huyu anazungumzia aina za uraia katika sehemu hii ya mwisho.

AINA TATU ZA URAIA WA TANZANIA

Akizungumzia aina za uraia, Mtanda anasema kwamba uraia wa Tanzania unasimamiwa na sheria za nchi za uraia Namba 6 ya mwaka 1995 pamoja na kanuni zake za mwaka 1997.

Anabainisha kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo, zipo aina tatu za uraia nchini:

“Kuna uraia wa Tanzania wa kuzaliwa, uraia wa Tanzania wa kurithi na uraia wa Tanzania wa Tajinisi,” anasema.

URAIA WA KUZALIWA

Msemaji huyo wa idara anasema kwamba kwa mujibu wa sheria ya Tanzania ya uraia Namba 6 ya mwaka 1995, mtu yeyote anayefuzu kuwa raia wa Tanzania wa kuzaliwa ni yule aliyezaliwa nchini na ambaye wakati wa kuzaliwa kwake, mmoja wa wazazi wake ni raia wa Tanzania.

URAIA WA KURITHI

Mtanda anasema, mtu yeyote aliyezaliwa nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, siku ya Muungano au baada ya Muungano anahesabika kuwa raia wa Tanzania wa kurithi.

“Hiyo ni kuanzia tarehe ya kuzaliwa kwake, kama siku ya kuzaliwa kwake, mama au baba yake ni raia wa Jamhuri ya Muungano kwa kuzaliwa au tajinisi,” anasema na kuongeza:

“Hiyo ina maana kwamba wazazi wake walikuwa ni raia wa Tanzania wa kurithi, wakati wa kuzaliwa kwake… mtu huyo hawezi kuwa raia wa Tanzania wa kurithi.”

URAIA WA TANZANIA WA TAJINISI

Kwa upande wa uraia wa Tanzania wa Tajinisi, Mtanda anasema kwamba mtu yeyote ambaye si raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuzaliwa au kurithi anaweza kuomba uraia wa Tanzania wa tajinisi.

“Hiyo ni kwa mujibu wa vifungu vya sheria Namba 8 na 9 (1) vya sheria ya Tanzania ya uraia ya mwaka 1995,” anasema.

Mtanda anabainisha, kwa mujibu wa sheria hiyo, Waziri mwenye dhamana ya masuala ya uraia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, ambaye ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kutoa au kutotoa uraia wa Tanzania, kwa wageni walioomba uraia.

SIFA ZAKE NI ZIPI?

Mtanda anasema, mgeni anayetaka kuomba uraia wa Tanzania anapaswa kuwa na sifa zinazotakiwa.

“Kwanza, mwombaji awe na umri wa miaka 18 au zaidi na awe na uwezo wa kufanya maamuzi yanayokubalika kwa mujibu wa sheria za nchi…awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda wa miezi 12 mfululizo kabla ya kutuma maombi ya uraia,” anasema na kuongeza:

“Katika muda wa miaka 10 kabla miezi 12, awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muda usiopungua miaka saba.”

Sifa zingine anazozianisha ni pamoja na mwombaji awe anaelewa vizuri lugha ya Kiswahili au Kiingereza lakini pia awe na tabia nzuri.

Aidha, Mtanda anabanisha kuwa awe pia amechangia na ataendelea kuchangia katika kukuza uchumi, sayansi, teknolojia na utamaduni wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Na awe amekusudia kuishi moja kwa moja ndani ya nchi ikiwa ombi lake la uraia litakubaliwa,” anafafanua.

TARATIBU ZA KUOMBA URAIA WA TAJINISI

Kwa upande wa utaratibu wa kuomba aina hii ya uraia, Mtanda anasema kuwa mgeni ambaye ana umri wa miaka 18 na kuendelea anatakiwa kujaza fomu za maombi ya uraia zinazopatikana katika ofisi zote za uhamiaji za wilaya, mikoa, ofisi kuu Zanzibar na Dar- es Salaam.

“Anatakiwa kutoa matangazo ya nia yake ya kuomba uraia mara mbili mfululizo, kwenye gazeti lililosajiliwa Tanzania,”anasema.

MCHAKATO KUSHUGHULIKIA MAOMBI YA URAIA

Ili kuhakikisha kuwa wageni wanaopewa uraia ni wale wenye manufaa kwa Taifa, Mtanda anasema maombi yote yanapaswa kupitia na kujadiliwa katika vikao vya kamati za ulinzi na usalama.

“Hiyo ni katika ngazi ya shehia kwa Zanzibar au kata kwa upande wa Tanzania bara…kwamba kata anayoishi mwombaji atahojiwa na ombi lake kujadiliwa na kikao hicho, hatimaye litapelekwa ngazi ya wilaya kwa hatua zaidi,” anasema na kuongeza:

“Wilayani, maombi yake yatawasilishwa katika kikao cha ulinzi na usalama cha Wilaya ambacho hujadili maombi ya uraia, hatimaye kutoa maoni na mapendekezo yake katika ngazi ya mkoa,”anasema.

NGAZI YA MKOA

Mtanda anasema kwamba katika ngazi ya Mkoa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa hujadili maombi yaliyowasilishwa na ngazi ya wilaya na kutoa maoni na mapendekezo yake kuhusiana na maombi hayo.

“Hatimaye maombi hayo kwa upande wa Zanzibar hutumwa kwa Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar, ambaye hutoa ushauri na mapendekezo yake kwa kamati ya kujadili maombi ya uraia,” anasema.

OMBI LA URAIA WA TAJINISI KWA MTOTO

Kwa upande wa aina hii ya maombi, Msemaji huyu wa idara anasema waziri mwenye dhamana ya uraia anaweza kuruhusu mtoto wa raia yeyote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupata uraia wa tajinisi.

Anafafanua kuwa hiyo ni baada ya maombi rasmi kuwasilishwa na mzazi au mlezi wa mtoto huyo.

URAIA WA TAJINISI KWA MWANAMKE ALIYEOLEWA

Mtanda anabainisha kuwa mwanamke aliyeolewa na raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wowote wa uhai wa mumewe, anaweza kuwasilisha maombi ya uraia wa Tanzania wa tajinisi.

Anasema ombi la uraia kwa mwanamke aliyeolewa linapaswa kuwasilishwa pamoja na viambatanisho vya vielelezo.

“Viambatanisho hivyo ni pamoja na cheti cha ndoa kilichosajiliwa na mamlaka husika nchini, pasipoti ya taifa lake ambayo haijaisha muda wake,” anasema na kuongeza:

“Hiyo ni pamoja na uhalali wake wa kuwepo nchini, yaani kibali cha kuishi nchini, pamoja na vielelezo vingine vinavyothibitisha kuwa mume wake ni Mtanzania.

URAIA WA NCHI MBILI

Kwa upande wa uraia wa nchi mbili, Mtanda anasema mtoto aliye chini ya umri wa miaka 18 ambaye ni raia wa Tanzania, anaweza kuwa na uraia wa nchi nyingine.

“Lakini akifikisha umri wa miaka 18, anatakiwa kuukana uraia wa nchi nyingine kama anapenda kuendelea kuwa raia wa Tanzania na akishindwa kukana uraia wa nchi nyingine atakoma kuwa raia wa Tanzania pale atakapozidi umri wa miaka 18,” anasema.

Mwandishi wa Makala haya anapatikana Kanda ya Ziwa kupita namba 0682 869 244

Habari Kubwa