IFAD inalenga kushiriki katika ubia unaowapa watu kipaumbele

13Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
IFAD inalenga kushiriki katika ubia unaowapa watu kipaumbele

Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) ni miongoni mwa mashirika yanayojiushughulisha na suala zima la uhakika wa chakula na ambalo lina uhusiano wa karibu kabisa na Siku ya Chakula Duniani.

NA Mwatima Juma.IFAD

Unafanya kazi kwa pamoja na serikali kuandaa miongozo ya sera za chakula, kuwasaidia wakulima wadogo kutumia mbinu bora za kilimo na uzalishaji wa mazao, na kuwasaidia wakulima hao kufikia masoko kukuza kipato, kujihakikishia chakula na lishe bora.

IFAD pia inawaunganisha wakulima na wajasiriamali vijijini kupata mitaji ya kifedha. Mwishoni mwa 2016, IFAD ilikuwa imeingia ubia na serikali 16 katika kanda ya mashariki na kusini mwa Afrika kukiwepo programu 42, yenye kugharimu zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 2.

Kwa hapa Tanzania IFAD ni mmoja wa wafadhili wa Mradi wa Kuboresha Miundombinu ya Soko na Mnyororo wa Thamani (MIVARF) ambao ulibuniwa na Serikali ya Tanzania ili kutekelezwa katika mikoa 29 nchi nzima.

Utekelezaji wa MIVARF ulianza rasmi Julai 2011 na tarehe ya kukamilika kwake ni Machi 31, 2022.

Mradi huu, unaotekelzwa nchini kote, una lengo moja kuu la kuchangia juhudi za kupunguza umaskini na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa misingi endelevu kwa kukuza vipato na uhakika wa chakula kwa walengwa.

Wanufaika wa Mradi huu wanajumuisha Kampuni ya Masoko ya Usangu (UMACO). Kupitia msaada wa MIVARF, ilihakikiwa na kuangalia maeneo ya kuongeza thamani ya mchele uliokuwa ukiuzwa.

Kuptia ushirikiano wa mkoboaji wa mpunga wa eneo hilo, MIVARF ilianza kuwahamasisha wakulima kukoboa mpunga wao ili uwe mchele na kuwawezesha kupata bei nzuri sokoni. Wakati huo huo, uamuzi ulichukuliwa kuunda kampuni hiyo.

Lengo la kuanzishwa kwake lilikuwa kutafuta wanunuzi watarajiwa wa mchele, kutambua mahitaji yao na kuwapa mchele bora uliofungashwa. Ilipofika Agusti 2015, UMACO ilisajiliwa rasmi.

Miongoni mwa changamoto walizokutana nazo ilikuwa ni namna ya kuchagua wabia 50 waliokuwa wanatakiwa kisheria kutoka miongoni mwa watu 150 waliokuwa wanasema wangependa kuwa wanahisa.

Baada ya kuchaguliwa, mwanahisa alitakiwa kununua hisa tano zenye thamani ya Shilingi 10,00 kila moja.

Mwanzoni baadhi ya wanahisa walikuwa wakijivuta kulipia gharama hizi. Mbinu za ujengaji wa uwezo zilitilia hili maanani kwa kuzingatia tofauti za watu kielimu na uzoefu kwani hili lilikuwa linaathiri uwezo wao wa kuelewa na kujenga stadi muhimu.

UMACO iliomba usajili wa hati ya ubora wa mchele kutoka Mamlaka ya Chakula na Vipodozi Tanzania (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ili kukidhi matakwa ya ubora na usalama.

Vipaumbele vya wanunuzi vilifaniwa tathmini ili kuona aina gani ya vifungashio ziagizwe kutoka kwa wazalishaji waliochaguliwa wa vifungashio.

Kwa mfano, ilibainika kuwa mifuko ya kilo 5 na kilo 10 iliyokuwa wazi kuonesha ndani ilipendwa zaidi na wateja ambao wangeenda kuuhifadhi mchele huo majumbani mwao. Juhudi za kuuza mchele wa Usangu zilijumuisha kuutangaza katika maonesho ya kilimo yaliyofanyika sehemu mbali mbali. Maeneo haya yalijumuisha Mbeya, Dar es Salaam, Morogoro, Lindi na Arusha.

“Nimegundua kuwa tunaweza kuuza mchele wetu wenyewe badala ya kuwategemea madalali kwani kufanya biashara hii kupitia kampuni yetu ni rahisi na ina faida zaidi,” anasema Bi. Kuruthum Mickdadi Abdallah, mkulima na mwanahisa wa UMACO.

Mwezi Julai 2016, kama sehemu ya shughuli za kuendeleza masoko, duka la mauzo ya mchele la UMACO lilifunguliwa Dar es Salaam. Mfano mwingine wa namna MIVARF inavyobadilisha mbinu za kilimo katika jamii za kitanzania ni simulizi ya Saada Ibrahim na Jerard Hamis, ndugu hawa wawili wanashirikiana mmoja wa wazazo, wameunganishwa kupitia kilimo.

Jerard alilelewa na baba yake mjini Iringa, wakati Saada alikulia kwa mama yake Itunundu, kijiji chenye wakazi 14,420. Pamoja na tofauti zao za makuzi, wote wawili Saada na Jerard walishawishika kuwa njia pekee ya kutoka kwenye umaskini ni kupitia kilimo.

Walipoanza kujitegemea, walianza kulima mpunga pale Itunundu, kijiji cha mababu zao. Pamoja na kwamba walikuwa wana miliki heka saba za ardhi, kwa miaka mingi walikuwa wamenaswa kwenye umaskini kutokana zaidi na malipo madogo waliyokuwa wanapata kutoka kwa madalali. Kwa maneno yake mwenyewe Saada anasema: “Hapakuwa na fursa ya kujadiliana beo kutoka kwa madalali.

Tulikuwa tunalazimishwa kukubali bei walizotupa.” Saada, Jerard na wanajamii wengine kutoka eneo lao walipata mafunzo ya biashara kutoka MIVARF. Hii ilipelekea kuundwa kwa mpango wa Biashara wa kikundi ili kununua mashine ndogo ya kukoboa mpunga ambao ni zao la tatu kwa umuhimu Tanzania.

Kitendo hiki cha kuongeza thamani kiliongeza thamani zaidi ya mara tatu kwa kila kilo ya mchele.

Mafunzo juu ya mbinu bora za kilimo yaliyotolewa na programu pia yaliwawezesha kuongeza uzalishaji wa mpunga kwa Zaidi ya mara mbili kutoka gunia 10 had 20 kwa heka. Ongzeko la uzalishaji na vipato pekee havitoshi kumtoa mtu kwenye umaskini.

Mabadiliko makubwa nay a kweli kwa Saada na Jerard yalikuja kufuatiwa kuanzishwa kwa ushirikiano wa kibiashara baina ya Vyama vya Ushirika na Masoko (AMCOS), ambapo Saada na Jerard ni wanachama, na Kundi la Makampuni ya Raphael (RGL), lenye makao yake makuu jijini Mbeya.

Ubia huu, uliowezeshwa na MIVARF, umewafaidisha ndugu hawa wawili pamoja na wanachama wengine 146 wa AMCOS, ambao mashine zao ya kukoboa mpunga zinaendeshwa na mtaalamu anayelipwa na RGL.

RGL ni moja ya makampuni yanayoongoza ya kukoboa na kusambaza nafaka hapa Tanzania. Ilianzishwa mwaka 1995 kama biashara ya familia, na kusajiliwa kama kampuni mwaka 2010. Sasa, RGL inafanya kazi na wakulima wadogo 6,000, ambapo asilimia 55 ni vijana na wanawake.

RGL inatumia njia ya kuwafundisha wakulima wadogo, kulingana na hatua ya maendeleo walioyofikia katika vyama vyao.

Kwa wakulima kama Saada na Jerard, ambao ni wanachama wa chaka kikuu cha ushirika, RGL inafanya kazi kupitia wakulima wakubwa.

Pale ambapo wakulima hawajaunda vikundi, RGL inafanya kazi na taasisi za uongozi vijijini kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika. Katika maeneo mengine, wanamiliki na kuendesha sehemu za uhifadhi wa pamoja wa mazao Pamoja na mamlaka za vijiji.

Kuendeleza juhudi juu ya mafanikio haya ya msaada wa programu ya MIVARF, RGL imeunda Muungano wa Wazalishaji Mpunga kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kuunda mahusiano ya kibiashara, sio tu na wakulima wadogo, lakini pia wasambazaji wa pembejeo, watoa huduma na taasisi za fedha.

Ubunifu huu wa ubia kati ya umma, binafsi, wazalishaji unahakikisha kuwa wakulima wadogo wanaheshimiwa na sio kufanywa watu wa chini katika ubia.

Kwa maneno ya Mkurugenzi wa IFAD hapa Tanzania, Francisco Pichon: “Ili kufanikiwa, muungano huu wa ubia unahitaji utambuzi wa kina wa washiriki wa umma na binafsi na utayari wao pamoja na uwezo wa kujenga ubia imara.

Wajasiriamali wa sekta binafsi kama vile wauzaji wa jumla, wasindikaji, wauzaji nje, vyama vikuu vya ushirika na taasisi za fedha, zihusishwe kuanzia mwanzo ili kujua vyema mahitaji na fursa zao, na namna watakavuyochukulia juhudi za mradi kwa ushirikiano wao.’’