IGP `azuia utata’ kuelekea Uchaguzi Mkuu Nigeria

16Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
IGP `azuia utata’ kuelekea Uchaguzi Mkuu Nigeria

WAKATI Nigeria ikielekea katika Uchaguzi Mkuu wa Februari mwaka huu, Rais Muhammadu Buhari amempendekeza Inspekta Jenerali Msaidizi kutoka jimbo la Nasarawa, kuziba nafasi ya Inspekta Jenerali wa Polisi Ibrahim Idris anayestaafu.

Rais Muhammadu Buhari (aliyekaa kulia), akiwa na IGP Ibrahim Idris.PICHA: MTANDAO

Mteuliwa huyo, Abubakar Adama, ameripotiwa na vyombo vya habari vya ndani vya Nigeria kwamba alikuwa Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Sera na Mafunzo ya Mikakati (NIPSS).

Kuteuliwa kwa Inspekta Jenerali mpya kunatajwa kuwa jambo la msingi hasa baada ya kustaafu kwa Idris ambaye jana alitimiza miaka 60 akiwa amelitumikia jeshi hilo kwa miaka 35 kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.

Jumatatu iliyopita, IGP mstaafu, Idris alimtembelea Rais Buhari kwenye makazi yake ya urais yaliyopo Villa jijini Abuja ili kumuaga.

Hakuna taarifa rasmi iliyotolewa baada ya kikao cha wawili hao, lakini vyanzo vya uhakika vilielezea kuwa Rais Buhari angelitangaza jina la IGP mpya jana (Jumanne).

Chanzo hicho kilieleza kuwa Rais Buhari na IGP Idris walikutana kwenye mazunguzo yaliyotawaliwa na usiri mkubwa.

IGP Idris aliteuliwa na Rais Buhari Machi 21, 2016 kuchukua nafasi hiyo kutoka kwa IGP aliyekuwapo, Solomon Arase aliyejiuzulu Juni 21, 2016.

Hata hivyo, uteuzi huo umeibua hoja tofauti kutoka kwa makundi ya kiraia na vyama vya siasa nchini humo, wengine wakiunga mkono na wengine wakipinga.

Makundi mawili ya kijamii nchini humo, yalitoa wito kwa Rais Buhari kuongeza muda wa utumishi kwa IGP Idris kwa vile kustaafu kwake wakati taifa hilo likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu si jambo lenye tija.

Kwa mujibu wa Makundi hayo, Baraza la vijana la Tiv na Jumuiko la Vijana Arewa, kustaafu kwa IGP Idris kunaweza kuchochea hujuma dhidi ya masanduku ya kura.

Mike Msuaan, Rais wa Baraza la Vijana wa Tiv na Msemaji wa Jumuiko la Vijana wa Arewa, Muhammad Salihu, wakasema kwa nyakati tofauti kuwa kiu yao kuona uchaguzi huo unakuwa huru na haki ni kwa Rais Buhari kumuongezea muda IGP Idris.

Hoja kama hiyo inatolewa pia na muungano wa vyama unaojulikana kama Coalition of United Political Parties (CUPP), wanaosema uteuzi wa IGP mpya si jambo lenye tija kwa wakati huu.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Jumapili na Msemaji wa CUPP, Ikenga Ugochinyere, ilisema kwamba, “Muungano wa wapinzani tunamkumbusha Rais Buhari atimize matakwa ya Sura ya 215 (1) ya Katiba ya mwaka 1999, ambayo yanaeleza wazi kwamba ni Rais pekee atakayemteua ofisa wa polisi kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi.”

Lakini hoja hiyo inapingwa na chama cha Peoples Democratic Party (PDP) kinachomtahadharisha Rais Buhari kutomuongezea muda wa utumishi IGP Idris kwa miezi sita.

Katibu wa Uenezi wa Taifa wa chama hicho, Kola Ologbondiyan, akawaambia waandishi wa habari mwishoni mwa mwaka jana kuwa, hatua yoyote ya kumuongzea muda IGP Idris itachukuliwa kama njama za kufanikisha ‘uchakachuaji’ wa matokeo ya Uchaguzi Mkuu.

BUHARI ATAFUTA MUHULA WA PILI

Rais Buhari atawania katika uchaguzi huo wa Februari mwaka huu, akikabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa mpinzani wake, Makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Atiku Abubakar.

Rais Buhari (75) ambaye ni mtawala wa zamani wa kijeshi katika taifa hilo lililopo Magharibi mwa Afrika, aliteuliwa bila kupingwa katika chama tawala cha All Progressives Congress (APC).

Wajumbe takribani 7,000 wa chama hicho waliokutana jijini Abuja mwaka jana, walitekeleza uteuzi huo kwa kile kilichoitwa ‘kutimiza wajibu’.

Msemaji wa Rais Buhari akazungumzia matokeo na kusema: “kwa vile hapakujitokeza mpinzani yeyote, hiyo ni ishara kwamba wanachama wote wanaridhishwa na utendaji kazi wa Rais na wana kiu ya kuona mafanikio mengi zaidi katika utawala wake.”

Chama cha APC kiliingia madarakani mwaka 2015, kikiwa cha kwanza kutokea upinzani nchini humo, kushinda kupitia sanduku la kura katika uchaguzi wa kidemokrasia.

Lakini Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unatarajiwa kuwa mgumu, ukichochewa na kuwapo raia wa nchi hiyo wanaokosoa mfumo wa utawala wa Rais Buhari.

MAKAMU WA RAIS MSTAAFU KUCHAGIZA UPINZANI
Nao upinzani kupitia kilichokuwa chama tawala cha Peoples Democratic Party (PDP) kilimteua Abubakar (71) kuwa mshindani wa Rais Buhari.

Abubakar ambaye ni mwanasiasa na mfanyabiashara nguli nchini humo, ameshashiriki kuwania urais mara nne bila mafanikio.

Mgombea urais huyo anatokea jamii ya waislamu wachache, Kaskazini mwa Nigeria, akiwania nafasi hiyo wakati Nigeria kukiwa na kanuni isiyoandikwa ya kupishana uongozi wa awamu mbili kwa wanaotoka Kusini na Kaskazini mwa nchi hiyo.

Uteuzi wa Abubakar ulifanyika katika mkutano ulioitishwa kwenye mji wenye utajiri wa mafuta wa Port Harcourt, Kusini mwa Niger delta.

Abubakar alipata kura 1,532 dhidi ya 693 alizopata mshindani wake wa karibu, Aminu Tambuwal, gavana wa zamani wa jimbo la Kaskazini mwa Sokoto.

Abubakar alitokea idara ya forodha alipohudumu kwa takribani miongo miwili. Kisha alijiunga katika sekta binafsi akiwekeza katika biashara ya huduma za mafuta, kilimo na viwanda vingine.

Kutokea hapo, alijiunga na serikali ya kiraia alipojitokeza kuwa mwanasiasa nchini Nigeria. Hata hivyo, alikabiliana na ‘majanga’ la kuwa na wanawake wengi, watoto zaidi ya 20 na kashfa kadhaa za rushwa.

BABA NENDA TARATIBU

Aprili mwaka jana, Rais Buhari ndipo alipovunja ukimya na kuweka wazi nia yake ya kuwania urais kwa muhula wa pili.

Jenerali mstaafu huyo aliyekuwa mtawala wa kijeshi wa taifa hilo katika miaka ya 1980, anakabiliwa na shinikizo kubwa la kutakiwa kujiuzulu hasa kutokana na kudhorota kwa afya yake kulikosababisha atumie miezi kadhaa kwa matibabu jijini London, Uingereza mwaka jana.

Nchini Nigeria upo msemo wa mzaha dhidi ya Rais Buhari kwamba “Baba nenda taratibu’. Hiyo ni kwa sababu ya kuchukua miezi sita tangu kuingia madarakani, alipotangaza baraza la mawaziri, pia akishutumiwa kwa namna anavyoshughulikia uchumi wa taifa hilo ‘ulioporomoka’ mwaka 2016.

Aidha, Rais Buhari anakosolewa kwa kushindwa kudhibiti mambo yanayoathiri usalama nchini humo zikiwamo shughuli za kikundi cha wanamgambo wa Boko Haram, mapigano ya wakulima na wafugaji na utekaji ulioshamiri Kusini mwa Nigeria.

Makala haya yameandikwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali. Mwandishi anapatikana kupitia simu namba +255 754 691540 ama barua pepe:[email protected].