Ijue Msalaba Mwekundu na mizizi yake

15Oct 2020
Yasmine Protace
Mkuranga
Nipashe
Ijue Msalaba Mwekundu na mizizi yake

MSALABA Mwekundu au Red Cross ni neno maarufu duniani na kihistoria, hasa pale panapotokea majanga mbalimbali. Hawa ni wanaojitolea kufanya kazi kuwanusuru majeruhi na misaada mingineyo.

Ni shirika la muda mrefu linalofanya kazi ya kuhudumia wanajamii au kutoa huduma ya kwanza kwa waliopata matatizo mbalimbali katika vita na majanga ya moto.

Katibu Mkuu wa Msalaba Mwekundu Tanzania, Julius Kejo, anasema asili ya mwasisi huyo ni mfanyabiashara kutoka nchini Uswisi, Herny Dunant, aliyeandika kitabu mwaka 1862 kuifahamisha dunia vita na akatoa mapendekezo ya kupunguza madhara yake.

Anasema, mzaliwa huyo wa mwaka 1822 aliyefariki mwaka 1910, kazi yake ilisaidia sana watu nchini Uswisi. Mwaka 1901, alitunukiwa zawadi ya kwanza ya Amani ya Nobeli.

Anasema vita tajwa vilitokea mwaka 1859 Kusini mwa Italia na akapendekezwa katika hilo: Kuanzishwa Shirika la Msalaba Mwekundu, ambalo ilitaka kuundwa mashirika yasiyofungamana upande wowote katika nchi.

Kejo anataja pendekezo lingine ni kuwapo mkataba wa kimataifa kulinda na kusaidia majeruhi wa kivita; na lingine kulikuwapo nembo ya kutambulika kote duniani, inayoonyesha kutofungamana na upande wowote, ikijitatambulisha na kulinda wafanyakazi wanaotibu.

Anasema matokeo ya mapendekezo ya mwaka 1863, ndio yalianzisha Kamati ya Kimataifa ya Kudumu huko Geneva, Uswisi kuhudumia majeruhi wa kivita.

Katibu huyo anasimulia kuwa, Msalaba Mwekundu ilianza kutumika kwa kuweka nembo ambayo inalinda majeruhi na wafanyakazi wa kutoa huduma za kibinadamu na mwaka 1859, Red Cross Society ilianzishwa katika nchi mbalimbali.

Tanzania ilianza kabla ya Uhuru na mwaka 1949 kulishakuwapo shughuli zake nchini. Kejo anaendelea kuwa:" Mwaka 1962 ilitungwa Sheria Namba 71 ya Mwaka 1962 ambayo Red Cross ikianzishwa Tanzania.'

Anasema, imekuwa ikihamasisha kuchangia damu, ili kunusuru wenye uhitaji wa damu na asasi hiyo ni wasaidizi wa serikali, mamlaka za umma na watu wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya na kijamii.

MAJUKUMU YAKE

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Red Cross Tanzania, John Busunga, Msalaba Mwekundu hufanya kazi ya kujitolea, akimaanisha majukumu yake kwamba:

“Huduma ya kwanza ni muhimu jamii kuijua, kwa sababu mtu anapopata tatizo, wanamsaidia na baadaye kumpeleka hospitali, kama tatizo bado litakuwapo.”

Anafafanua kuwa, baadhi ya watu wanapata matatizo katika miili yao, lakini watu wanakumbana na matatizo pale wanapokosa huduma ya kwanza na kuchangia uokoaji maisha ya binadamu, kwa kutoa msaada kwenye matatizo.

Busunga anasema asilimia 80 ya shughuli za Msalaba Mwekundu zinafanywa na watu vijijini na Mhamasishaji Mkuu, Dk. Christopher Nzera, anasema zilianza kutolewa kupitia kamati za kimataifa.

Anasema kuanzishwa kwake ni kuwasaidia walioumia vitani, lengo lingine ni kustawisha haki na afya kwa binadamu, ikiwa asasi isiyobagua.

Pia, Naibu Katibu anasema wamekuwa wakiwafundisha watu namna ya kufanya huduma ya kwanza, ili iwasaidie watu penye matatizo na kuna miradi 25 nchini, wanayoiendesha nchi nzima.

Hapo anataja mradi uliokuwapo mkoani Kigoma, kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye mazingira magumu, kwa kuwapa mitaji na kujifunza ufundi kama wa cherehani na makenika.

Anasema kuna mradi kwa vikundi 21 vilivyoundwa kwa ajili ya ujasiriamali; na mradi wa majisafi na salama kuzifikia kaya 5000 nchini, huko Simanjiro mkoani Arusha.

"Simanjiro kaya 3420 katika vijiji vitano, wamewasaidia shule kupata maji na vyoo,” anaeleza na kuongeza kuwa wakimbizi zaidi ya 100,000 kutoka nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DCR) na Burundi, wanahudumiwa na madaktari na chumba cha mochwari.

Kuhusu huduma ya kwanza, anasema inafanyika katika mikoa yote kitaifa.

Mratibu wa Msalaba Mwekundu, Pemba, Selemani Mohamed Ally, anasema ni kosa kutumia nembo ya ‘Red Cross’ kwenye huduma ya dawa au kuweka katika nguo za kufanyia kazi.

Anasema msako ukianza kwa kuwakamata wanatumia nembo ya Msalaba Mwekundu, ikitumika kuitapeli mhusika anatozwa faini kati ya shilingi milioni tatu hadi tano.

Habari Kubwa