Ijue Saccos iliyokamata walimu na watumishi umma Missenyi, Bukoba

22May 2020
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe
Ijue Saccos iliyokamata walimu na watumishi umma Missenyi, Bukoba
  • • Kusamehe deni ‘waliotumbuliwa’ vyeti
  • • Mwasisi wake asimulia ilichomfanyia
  • • Yasaidia madawati 200, kila wilaya 50%

KATIKA aina za ushirika zilizomea nchini, ule wa kuweka na kukopa, maarufu Saccos, kwa sasa umekamata sana nchini.

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Denice Mwila (kushoto na shati la kitenge), akipokea madawati 100 kutoka Burute Saccos. Kulia (aliyevaa koti jeusi) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Innocent Mkandara. PICHA: LILIAN LUGAKINGIRA

Mkoani Kagera katika wilaya za Bukoba na Missenyi, mwaka 2006, walianzisha Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Walimu na Watumishi wa kada nyingine, kiitwacho Burute Saccos Ltd, kikiwa imara kwa miaka 14 sasa.

Ni chama ambacho hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana, kilishatoa mikopo kwa wanachama wake, zaidi ya shilingi bilioni 2.2.

Hata hivyo, ni ripoti inayoonyesha baadhi ya wanachama walishindwa kurejesha mikopo yao, hivyo kusababisha deni la zaidi ya shilingi milioni 97.2 ambayo haijalipwa.

Hadi kumalizika mwaka jana, Burute Saccos ilikuwa na jumla ya wanachama 1,351 na mtaji wa zaidi ya Sh. bilioni 1.9, kwa mujibu wa hesabu zake zilizokaguliwa.

MWENYEKITI

Gerald Kigundu, Mwenyekiti wa Burute Saccos anasema walilazimika kuingia mkataba na kampuni maalumu ya kukusanya madeni, kuhakikisha deni linarejeshwa kwa wakati.

Kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa baina ya pande zote mbili, kuna wanachama 37 wanaodaiwa kiasi hicho hadi kufikia Machi 31 mwaka huu.

Mwenyekiti huyo anasema, chama kilianza na wanachama 520 wakiwa na mtaji wa zaidi ya shilingi milioni 34.5 uliojumuisha hisa za wanachama (Sh. milioni 22.4); Akiba ya lazima Sh. milioni 2.4; akiba za mafungu Sh. milioni 1.8; tengo la mikopo iliyoshakani Sh. milioni 1.8 na malimbikizo ya ziada zaidi ya Sh. milioni 6.1.

Kwa mujibu wa Kigundu, waanzilishi wa Burute Saccos walikuwa walimu pekee na baadaye ikafungua milango kwa watumishi wa umma kada nyinginezo, lengo ni kuwapunguzia adha ya kukopa benki kwa riba kubwa.

"Wakati chama kinaanzishwa kilikuwa kinatoa mikopo kwa riba ya asilimia 18, lakini kwa sasa kinawakopesha wanachama kwa riba ya asilimia tisa tu kwa mwaka," anasema.

"Kama chama tuna jukumu la kuendelea kutoa mikopo kwa wanachama wetu, kusimamia na kuratibu urejeshaji wa mikopo, kukusanya akiba, hisa na amana kutoka kwa wanachama, ili kuwezesha umoja wetu kuwa endelevu," anasema.

Pia, anaeleza sababu ya kuanzisha usahirika huo ilikuwa kuwanusuru wanachama wake walioanza kukopa pasipostahili kwa riba kubwa.

"Hiki ni chombo cha heshima ambacho kinatunza pia faragha za wahusika, baadhi yao heshima zilianza kushuka kutokana na mikopo isiyostahili," anasema Kigundu, anayeeleza hatua za awali, chama hakikuwa na mtaji unaotosheleza mahitaji.

Kigundu anataja jitihada za kujiboresha walizozifanya ni kuwahimiza wanachama kuongeza uwekezaji katika hisa, akiba na amana.

"Mbali na mikopo kila mwisho wa mwaka tunatoa gawio, pia tunatoa elimu kwa wanachama ikiwamo ya ushirika na ujasiriamali, ili wajue matumizi bora ya mikopo. Pia, tunafanya tathmini kwa mikopo tunayotoa ili kuona maendeleo ya mtu aliyekopeshwa," anasema.

Kwa mujibu wa mwenyekiti, kazi ya kuhakiki vyeti kwa watumishi wa umma iliyofanywa na serikali mwaka 2016, iliwapoteza wanachama 24 walioondolewa kazini wakiwa na mikopo yenye zaidi ya Sh. milioni 67.9 kufikia Desemba mwaka jana.

"Kwa kutambua maisha magumu yanayowakabili, Mkutano Mkuu wa Mwaka 2019 uliona ni busara kuwasamehe na sasa tunafuatilia kibali kutoka kwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika, ili tuweze kuwafutia madeni yao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo," anasema.

Kuhusu namna inavyowiana na jamii, Kigundu anasema, mwaka huu chama kimetoa msaada wa madawati 200, nusu yake kwa Shule za Msingi Kemondo, Mubembe na Ibaraizibu, zilizoko katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba.

"Madawati mengine 100 yametolewa kwa shule tatu za msingi ambazo ni Bugango, Mabale na Mwisa za wilaya ya Missenyi, msaada wote huu una thamani ya shilingi milioni 11," anasema mwenyekiti.

Pia, anasema wamewekeza katika shamba la miti lenye ukubwa wa ekari 1.2, imenunua na kumiliki hisa katika benki mbalimbali; kununua kiwanja na kujenga ofisi yake inayorahisisha huduma na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.

IENDAKO

Mwenyekiti Kigundu anasema, Burute Saccos ina mipango ya kupunguza kiwango cha riba kwa wanachama, kuwezesha wanufaike, inayoendana na mtazamo wa kuongeza idadi ya wanachama wake.

Ni mkakati unaoendana na kuimarisha mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ili watendaji husika waweze kutoa mikopo kwa njia ya mtandao (online).

"Kwa sasa anayehama eneo la Saccos ilipo anapoteza uanachama, lakini kwa mpango huu uliopo wa kuimarisha mfumo wa Tehama, utawezesha hata walioko nje ya eneo kunufaika," anasema Kigundu.

Kufuatia chama hicho kuwa na uchaguzi mkuu mwaka huu anatumia fursa hiyo kuwashauri wanachama kuwachagua viongozi wenye weledi ambao wataweza kusimamia na kuendesha chama chao vizuri na kuwezesha kuendelea kuwepo kwa manufaa zaidi kwa wanachama.

DC MISSENYI

Kanali Denice Mwila, Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, ni miongoni mwa viongozi waliopokea msaada wa madawati kwa ajili ya shule tatu za msingi zilizoko wilaya kwake.

Anatumia fursa hiyo, kuishukuru Burute Saccos kuchangia madawati, lengo ni kuboresha mazingira ya watoto kujifunzia. Rai yake ni taasisi nyingine kuiga mfano.

"Shule zilizolengwa kweli zina mahitaji makubwa ya madawati, mfano Bugango, shule ya msingi ina wanafunzi wengi na mahitaji ni makubwa mpaka tumelazimika kuanzisha darasa jingine pembeni, ili kuona kama itaweza kumudu idadi ya wanafunzi waliopo," anasema.

MWASISI WAKE

Brighton Mwombeki, mwanachama mwanzilishi wa Burute Saccos, anasema mikopo aliyokwishachukua kwa awamu tano, imemsaidia kuboresha maisha yake, amekarabati nyumba yake, kuendesha kilimo na ufugaji.

"Nilikuwa na kuku kama 200 na sasa baada ya kuona wamezeeka nimewauza na kupata shilingi 900,000, lakini najiandaa kuleta wengine.
“Pia, nina ng'ombe, nalima bustani kama nyanya, kabichi, pilipili hoho, nyanya chungu na mabohora (passion fruits)," anasema.

Anataja mengine; mashamba ya migomba, kahawa yenye miche 400 na miti ekari mbili, miradi iliyowezesha kumpatia mahitaji muhimu ya familia yenye watoto wanane, saba wanalipiwa ada na mahitaji ya shule.

Mwombeki, hasiti kuwashauri watumishi wenzake kuchukua mikopo, wakiwa tayari na mipango mizuri ya matumizi yake.

"Kuna watumishi wengine wana kawaida, wakisikia kuna sehemu wanatoa mikopo wanakwenda kuchukua bila kuangalia athari zake, hawajui wataitumia kwa mambo gani na watalipa vipi, matokeo yake mshahara unatoka hela yote inachukuliwa," anasema.

Habari Kubwa