Ijue shida ya utapiamlo na undani wake ulivyo

21May 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ijue shida ya utapiamlo na undani wake ulivyo

UTAPIAMLO si msamiati mgeni kwa jamii. Asasi ya Reichet Fundation ya nchini katika tovuti yake inatafsiri: “Ni ugonjwa unaoathiri kukua kwa mwili na akili ya mtoto (na mtu mzima).”

Mtoto mwenye afya njema, akipatiwa mlo kwa utaratibu. PICHA: MTANDAO

Ni namna ya mwendelezo wa kinachosemwa kimataifa, ikiwamo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) na Shirika la Chakula la Kilimo Duniani (WHO).

Kimsingi, ni maradhi yenye tabia ya kumjengea mtoto wasifu kadri anavyozidi kukonda, macho na utosi wa kichwa hubonyea, ngozi na mishipa ya mwili inakauka na uwezo wa kudhibiti joto mwili hupungua.

Chanzo chake kikuu ni ukosefu wa vitamini na madini ya kutosha mwili, ikiangukia zaidi kwa namna mbili: Mosi ni, ukosefu wa protini, nishati, vitamini na madini mwilini, pili kuwapo maambukizo ya kila mara ya maradhi kwa mtu.

“Magonjwa kama vile kuharisha, surua, malaria, na magonjwa ya kupumua hudhoofisha mwili sana na kupunguza vitamini na madini. Magonjwa hayo humfanya mgonjwa apoteze hamu ya kula naye hula chakula kidogo sana na hivyo anapata utapiamlo.

“Kwa upande mwingine, mtoto asiyepata chakula cha kutosha anaweza kuambukizwa magonjwa kwa urahisi. Jambo hilo huongeza idadi ya watoto wanaokufa kwa sababu ya kukosa vyakula vinavyojenga mwili,” zinafafanua taarifa za wadau wa afya kimataifa.

VIPI MTOTO?

Watoto wanakua haraka na hivyo wanahitaji nishati na protini nyingi zaidi. Vivyo hivyo, wajawazito na wanaonyonyesha wanaweza kuupata utapiamlo.

Mtoto mchanga huanza kuathiriwa akiwa tumboni, sababu kuu ni mama anapokosa chakula cha kutosha au kilicho bora kabla na wakati wa mimba, hata akijifungua mtoto mwenye uzito mdogo.

‘Kichanga’ anapoachishwa kunyonya mapema na akakosa lishe stahiki na kichafu, mama huyo naye anaweza kuangukia katika utapiamlo.

Utapiamlo unamwathiri mtoto kwa njia nyingi, ikiwamo ukuaji, mathalani anapokosa madini ya kutosha hasa chuma, aiodini, zinki na vitamini hasa vitamini A, kunamuweka pabaya mtoto kiafya.

Kwa nini sasa inawashambulia watoto? Ni kwa sababu wanakua haraka, hivyo wanahitaji nishati na protini nyingi zaidi. Vivyo hivyo kwa wajawazito na wanaonyonyesha.

Mtoto mchanga anaathirika kuanzia tumboni, iwapo mama hatopata chakula cha kutosha, kabla au na wakati wa ujauzito.

Pia, hutokea mtoto anapoachishwa kunyonya mapema, asipolishwa vizuri, au usafi usipozingatiwa, anaweza kuugua utapiamlo.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), linasema ukosefu wa vitamini A kumewaathirti watoto wachanga milioni 100 duniani, wakapata upofu na kudhoofisha mfumo wao wa kinga, hivyo kuwapunguzia uwezo wa kujikinga na maambukizo.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa, inarejea madhara ya utapiamlo mwilini, kama vile moyoni, figo, tumbo, mapafu na ubongo na uchunguzi unaonyesha, makuzi duni ya mtoto yana athari za kudumu akilini.

Hata hivyo, Unicef inakiri jitihada zinazofanyika kwa kauli: “Zaidi ya robo tatu ya watu wanaokufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na ukosefu wa chakula, hufa kwa sababu ya utapiamlo mdogo au wa wastani.”

VYANZO KIJAMII

Kuna mambo mengine ya kijamii, kiuchumi, kitamaduni na kimazingira yanayochangia kuwa visababishi vya utapiamlo.

Vilevile kunatajwa mgawo duni wa chakula kwa kuwabagua kinamama na kuwanyima fursa za elimu rasmi na zisizo rasmi na athari za mazingira kusababisha uhaba wa chakula.

Ripoti ya Hali ya Uhaba wa Chakula Duniani ya mwaka 2001, ilionyesha kati ya Oktoba mwaka 1999 na Juni, 2001, nchi 22 duniani ziliathiriwa na ukame; vimbunga au mafuriko nchi 17; nchi 14 vita vya wenyewe; huku migogoro nchi 3 na mbili, matetemeko ya ardhi.

VYANZO VIKUU

Asasi za kimataifa zikiwamo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wa Watoto (Unicef) na Shirika la Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (WHO), zinaorodhesha vyanzo vyake katika maeneo makuu matatu.

Kunatajwa kuwapo vyanzo vya karibu: Hapo ni kama ukosefu wa pesa; uzalishaji mdogo wa chakula; matunzo na uhifadhi duni wa vyakula; uchaguzi usio sahihi wa vyakula, mpango, usimamizi na matumizi yasiyo sahihi ya mapato na ulishaji duni. Hiyo inahusu zaidi watu wazima.

Aidha, kuna mtazamo kwa wanaonyonyesha, wagonjwa na wazee; Inabeba mitazamo kama maandalizi duni na usafi, kinga na tiba ya magonjwa na matumizi ya huduma za afya.

Kurejea, andiko la kimataifa la mwaka 2004 la Unicef na WHO, liitwalo ‘Unicef Framework in FAO (2004) Family Nutrition Guide’ pia, lina ufafanuzi kuhusu mchango wa umaskini na maisha duni, kuukaribisha utapiamlo.

Ni ripoti inayotoa viashiria vya uhalisia wa maisha duni kama vile kutumia maji kidogo kuliko mahitaji, mazingira ya dhiki, msongamano wa makazi na huduma duni za afya, vyote vina nafasi yake.

Mengine yanaangukia katika umaskini uliokithiri kwa jumla na ukosefu wa fursa za ajira; usawa katika mgawanyo na udhibiti wa rasilimali katika jamii, wilaya, nchi na ngazi za kimataifa.

Sambamba na hiyo, mashirika hayo ya Umoja wa Taifa yanataja ukosefu wa elimu kwa kinamama, msongamano, uharibifu wa mazingira; machafuko na migogoro ya kisiasa; ukosefu wa huduma za afya, elimu; na ubaguzi katika jamii.

LISHE BORA

Lishe bora inaangukia pia katika vyakula vilivyoimarishwa. Hapo inatajwa ni vyenye nyongeza ya virutubisho ambavyo, kupitia lishe za kawaida kama vile vya kila siku, ikiwamo unga, nafaka na mafuta yatokanayo na mimea, sukari na chumvi, huku viazi vitamu vyenye rangi ya chungwa na manjano, wataalamu wanavitaja kuwa na utajiri wa Vitamini A.

Pia, mlo wa vyakula vilivyoimarishwa na kampeni mbalimbali za lishe kimataifa na mamlaka za kiafya, zinatajwa kuwa na maana kubwa kwa uhai wa binadamu.

WALAKINI

Hata hivyo, ripoti za uchambuzi huo, unataja walakini kwamba, vyakula vilivyoboreshwa mara zote haviwafikii walengwa kutokana na aina ya mahitaji ya kila mlaji kuwa tofauti.

Wadau hao wa afya wa kimataifa, wanafafanua kwamba vyakula vingi kwa sasa vimeimarishwa kulingana na mahitaji ya mtu mzima.

Kwa vile mahitaji ya virutubisho hutofautiana kulingana na umri na afya ya mtumiaji, vyakula vilivyoimarishwa havitoshelezi mahitaji ya kila mtu na havitoi kiwango kinachohitajika kwa ajili ya watoto au wajawazito, kusaidia ukuaji na uzazi.

Pia, kupatikana vyakula hivyo bado ni tatizo kwa sababu vyakula hivyo hupatikana kwa wale wanaoweza kununua vyakula vilivyohifadhiwa.

•Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa taarifa za kimataifa.

Habari Kubwa