Ili kukabili msongamano masomo yawe kwa ‘shifti’

30Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Ili kukabili msongamano masomo yawe kwa ‘shifti’

JANA shule zimefunguliwa rasmi na imethibitishwa kwamba si wakati wa kuendelea kujifungia ndani ‘lockdown’ kwani kutasababisha matatizo mengi zaidi kwenye jamii. Ni kwa sababu uchumi wa mtu mmoja mmoja unategemea shughuli anazozifanya kila siku.

Wanafunzi wakikaa kwa kuachiana nafasi darasani inaweza kuwa njia mojawapo ya kupunguza uwezekano wa kuambukizwa corona. PICHA: MTANDAO

Kwa hiyo, kufungiwa kazi hizo kungeleta madhara makubwa kwa taifa.

Baada ya shule za msingi na sekondari kufunguliwa ni jambo jema kwa wanafunzi, wazazi, walimu pamoja na kwa serikali yenyewe inayoangalia uelekeo mpya wa corona.

Pamoja na tangazo hilo ni muda wa kuishauri serikali hasa Wizara ya Elimu, wakati wanafunzi wako madarasani kwani ni lazima waendelee kuwa salama zaidi kuepuka maambukizo ya COVID -19 kwasababu kipindi serikali ilipotangaza kufunguliwa shule ilieleza umuhimu wa kujihadhari.

Maana ya angalizo hilo ni kwamba ugonjwa upo ndiyo maana hadhari zinapaswa kuendelea kuchukuliwa na ili watoto wawe salama wakati wa masomo yao.

Shirika la Afya Duniani (WHO), pamoja na Wizara ya Afya zimeainishwa njia mbalimbali za kujikinga na ugonjwa wa corona, miongoni mwa njia hizo ni pamoja na kunawa mikono kila mara kwa maji tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono venye asilimia zaidi ya 60 ya kileo, kuvaa barakoa na kukaa umbali wa zaidi ya mita mbili kutoka mtu hadi mtu.

Hili nalo linaleta changamoto kwa vile hali halisi ya shule za nchi hii inafahamika kuwa ni finyu na uchache wa vyumba vya madarasa katika shule za msingi na sekondari ni dhahiri.

Wanafunzi wanakaa kwa kubanana kwani chumba kina uwezo wa kuchukua wanafunzi 45 wanakaa zaidi ya 60 kwa shule nyingi, kwa hiyo uwezekano wa kuzingatia umbali wa angalau wa mita mmoja ni mgumu sana tena ikizingatiwa kwamba ugonjwa huu unasambaa haraka sana kwa kugusana ama kukaribiana na mwenye maambukizo.

USHAURI

Ni katika maeneo mawili, moja ni kuhusu shule za kutwa za serikali na za binafsi, pili ni kuhusu shule za bweni pia za serikali na binafsi.

Kwa shule za kutwa ambazo wanafunzi wanakwenda kila siku shuleni na kurejea nyumbani jioni, kwahiyo ni wanafunzi ambao wana muingiliano mkubwa na jamii.

Wengi wanapokwenda shuleni wengine wanatumia usafiri kama daladala kwa mfano walioko Dar es Salaam au kwenye miji yenye misongamano mikubwa kunaweza kusababisha kupata maambukizo na kuyaleta shuleni ambako nako kuna msongamano kwenye vyumba vya madarasa na hivyo kufanya uwezekano mkubwa wa ikiwa mmoja amepata mahali fulani kusababisha wengi kuambukizwa.

KUTUMIA AWAMU

Nini kifanyike sasa ? Kuna haja ya shule hizi zote za msingi na sekondari kuwa na shifti (kusoma kwa awamu mbili).
Ikimaanisha madarasa yatenganishwe mfano shule za msingi kuanzia darasa la kwanza mpaka la tatu.

Hawa waingie asubuhi mpaka mchana na kisha waliosalia wanaingia mchana na kuendelea vivyohivyo kwa shule za sekondari ili kuwapa nafasi ya kupangwa kwa nafasi kwenye vyumba vya madarasa.

Inawezekana ikawa usumbufu hasa namna ya kupanga ratiba za masomo kwa sababu madarasa yatagawanywagawanywa lakini sina hakika kama linaweza kuwa tatizo kubwa kwa walimu kufanya hivyo.

MSONGAMANO WALIMU

Suala la awamu liende sambamba na kuwapanga kwenye shifti pia, kwasababu hali ya walimu ni ileile shule nyingi zinatumia madarasa kama ofisi kwa hiyo hata walimu nao wana misongamano kwenye ofsi zao.

Kwa upande wa shule za bweni huku kuchukua tahadhari kuna unafuu ikilinganishwa na shule za kutwa kwani hao hawajachanganyikana na jamii za watu wa nje ya shule licha ya kwamba kuna walimu wanaotoka nje ya mazingira ya bweni.

Wanafunzi wako bweni uwezekano wa kuzuia muingiliano na watu wa nje ni rahisi zaidi kwa watumishi kwa maana ya walimu na wafanyakazi wengine kuchukua tahadhari wao wenyewe ili wasiwe sababu ya maambukizo.

Wanaweza kutafuta mahitaji na kurudi shuleni lakini kwa wanafunzi hakuna shida wakishaingia wameingia na kutoka ni mwisho wa muhula kwa hiyo kama itatokea wamefika shuleni hakuna mwenye maambukizo si rahisi kuyapata.

Katika maelezo yake, Wizara ya Elimu ilieleza kwamba watoto wadogo chini ya miaka mitano wasivalishwe barakoa kutokana na maelekezo ya kitaalam ni jambo jema lakini watoto hawa wanatoka kwenye familia huku ambako sisi kama wazazi tunachangamana sana.

Kwa hiyo uwezekano wa kuwaambukiza watoto na wao wakapeleka shuleni ni mkubwa ndiyo maana njia sahihi ni shifti ili wakibaki wachache wanaweza kutawanywa vizuri kwenye vyumba na kuzuia kusongamana.

Kunawa mikono hilo litawezekana japo pia litakuwa na changamoto zake moja ikiwa ni upatikanaji wa maji ya kutosha ikizingatiwa kwamba kwasasa ni kipindi cha kiangazi hapo mbinu mbalimbali zitatumika ili kuhakikisha yanakuwapo na hapo kunahitajika ushirikiano mkubwa kati ya shule na wanavijiji au wananchi ili huduma za maji zipatikane pamoja na vitakasa mikono.

Pengine hili suala la shifti au awamu wizara ilishaliona na kulijadili.

Huenda ilionekana kuna kubwa lakini nashauri kama lilionekana litakuwa na changamoto ni bora zitafutiwe ufumbuzi ili lifanyike kwa nchi nzima na kama pengine hamkulijadili kama wizara ni wakati muafaka wa kulifanyia kazi.

Utaratibu huu unaweza kufanyika kwa majaribio mpaka mwezi Disemba 2020 kama utakuwa na mafanikio basi utaendelea mpaka pale hali itakaporidhisha kurudi kwenye utaratibu wa kawaida.

KELELE ZA ADA

Aidha ni vyema kuzingatia ushauri wa serikali kwa wamiliki wa shule binafsi kuhusu malipo ya ada na michango mbalimbali kwamba busara inahitajika kati ya pande zote mbili kutokana na ukweli kuwa janga la corona limeathiri watu wengi kiuchumi.

Ajira nyingi zimekufa na mishahara kupungua na hivyo wapo wazazi watakaoshindwa kulipa ada za watoto wao kwa wakati, basi ni busara pia wamiliki na wakuu wa shule hizo kufahamu hilo ili kazi isiwe moja ya kudai ada kila wakati.

Badala yake ifahamike kwamba kuna tatizo la kiuchumi, kwa upande wa wazazi nao wajikongoje ili walimu nao wapate mshahara ili shughuli za uendeshaji wa shule zisiwe ngumu kiasi cha kukwama lakini ni muhimu zaidi busara na hekima ikatumika kabla ya kutazama upatikanaji wa fedha pekee.

Maoni: 0689157789, [email protected]

Habari Kubwa