Ilipo TRC ujenziI reli ya kisasa

25Nov 2018
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Ilipo TRC ujenziI reli ya kisasa

BAADA ya miaka 100 ya kutumia reli ya kati iliyojengwa na wakoloni wa Kijerumani, Tanzania imefungua ukurasa mpya wa ujenzi wa reli ya kisasa almaarufu, Standard Gauge Railways (SGR), ambayo pamoja na kusafirisha shehena na abiria kwa ufanisi zaidi, ni lango la biashara ya kimataifa........

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, (aliyeinama), akikagua mataruma ya zege yanayofungwa kwenye reli ya SGR, wakati alipotembelea kambi ya mkandarasi Yapi Merkezi anayejenga SGR iliyoko Soga mkoani Pwani, Oktoba 3, 2018. PICHA: MARY GEOFFREY.

linalounganisha Tanzania na mataifa kadhaa yasiyo ya bahari ikiwamo Rwanda na Jamhuri ya Congo.

Ujenzi wa reli ya kisasa unasimamiwa na Shirika la Reli (TRC), likishughulikia miradi mikubwa miwili ya ujenzi wa SGR, mwingine ni kurejesha njia ya reli ya Tanga, Arusha na Moshi iliyoharibiwa baada ya maturuma na reli kung’olewa na siku za usoni TRC itahusika na kujenga reli za Mtwara , Mbamba bay na njia ya Singida.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio ya TRC katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya tano jijini Dar es Salaam, anasema utekelezaji wa mradi huo wa SGR unalenga kuchochea ukuaji wa uchumi na biashara baina ya Tanzania na nchi nyingine duniani.

“Ni kwasababu usafirishaji kwa kutumia reli unabeba shehena kubwa kwa mara moja na ni wa gharama nafuu ukilinganisha na aina ya nyingine za usafirishaji hasa kwa mizigo mikubwa na mingi inayokwenda umbali unaozidi kilomita 400," anasema Kadogosa.

Anaeleza kuwa, SGR ina mtandao usiopungua kilomita 2,561 kwenye kanda ya kati inayounganisha mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Katavi na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo.

Kadogosa anawaeleza wanahabari kuwa, SGR ina uwezo wa kusafirisha uzito mkubwa hadi tani 10,000 kwa treni moja kwa mwendokasi wa kilomita 120 kwa saa kwa treni ya mzigo na za abiria ni kilometa 160 kwa saa.

AWAMU ZA UTEKELEZAJI

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, anasema, mradi huo unatekelezwa kwa utaratibu na usanifu na kujenga kwa usanifu anafanya mkandarasi mwenyewe na kwamba upo katika sehemu tano, na sehemu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo ina urefu wa kilomita 1,219 za reli pekee usiohusisha njia za kupishana.

Anakitaja kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kuwa kina kilomita 300 kati ya hizo 205 ni njia kuu na kilometa 95 ni njia za kupishania.Aidha, awamu ya pili na ujenzi kuanzia Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma yenye urefu wa kilomita 422 ikijumuisha kilometa 336 za njia kuu na 86 za kupishana. Katika njia hiyo kuna kipande cha reli kuanzia Makutopora hadi Tabora chenye kilometa 376.5 yenye kilometa 294 za njia kuu na za kupishana ni kilometa 73.5.

Kadogosa anataja kipande kingine cha reli kutoka Tabora hadi Isaka chenye urefu wa kilometa 162.5, kikihusisha kilometa 130 za njia kuu na za kupishania ni 32.5. Kingine kinaanzia Isaka hadi Mwanza chenye urefu wa kilometa 311.25 kati ya hizo za njia kuu ni 249 na za kupishania ni kilometa 62.5.

Aidha, anasema ujenzi wa SGR kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro unatarajiwa kukamilika ifikapo Februari 2021 na kwamba mpaka sasa zimetandikwa zaidi ya kilometa 15 ambazo zinajengwa kwa kodi za Watanzania.

Kuhusu uthamini wa ardhi inakopita reli hiyo, Kadogosa anasema kilometa za ardhi 116 zimekamilika katika maeneo ya Morogoro hadi Kilosa, Ihumwa hadi Gulwe wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma na kwamba ujenzi wa tuta ambalo reli hutandikwa juu yake lenye kilomita 80 limesafishwa na tayari kilometa 33 zimeshajazwa udongo .

Kuhusu gharama za mradi anasema ni Sh. trilioni 7.1 ambazo ni fedha za walipa kodi na kwamba mradi wa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ni Sh. trilioni 2.7 na kipande cha Morogoro hadi Makutupora ni Sh. trilioni 4.4

KAZI ZINAZOENDELEA

Mkurugenzi Mkuu wa TRC anasema katika kazi hizo za ujenzi, shirika hilo linategemea kuwa na stesheni 14 kati ya hizo 10 zitakazohudumia treni ya mizigo na kwamba stesheni kubwa ni tatu -Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma, vituo viwili vyenye miundombinu, karakana za kuunda treni na huduma za bandari kavu zitakuwa Kwala mkoani Pwani na Ihumwa Dodoma.

“Kazi kubwa zinazoendelea ni usanifu, ujenzi wa madaraja, tuta la reli, makalavati, kuzalisha mataruma yenye zege, ujenzi wa miundombinu ya ishara na mawasiliano na nguzo za umeme wa SGR. Mataruma ya njia ya reli yanazalishwa nchini na kiwanda kipo Soga mkoa wa Pwani katika kambi ya ujenzi wa reli ya kisasa," anasema Kadogosa.

Anaeleza kuwa, kwa siku huzalisha mataruma 1,080 na kila taruma lina uzito wa kilo 380 na kwamba yanahitajika 500,100 kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na mengine 703,300 yatatumiwa kujenga reli kutoka Morogoro hadi Makutupora.

Anaeleza zaidi kuwa mataruma yote yatatengenezwa katika kiwanda cha Soga na tayari yameshazalishwa mataruma 27,000 na pindi mataruma 500,000 yatakapotengenezwa kiwanda hicho kitakuwa mali ya serikali.

NGUVU KAZI

Akizungumzia kampuni za ujenzi Kadogosa anasema katika utekelezaji wa mradi huo, TRC imetoa zabuni kwa wakandarasi ambao ni ubia ikiwamo Yapi Markezi kutoka Uturuki na Mota Engil kutoka Ureno kwa upande wa kazi ya Dar es Salaam hadi Morogoro.

Aidha, kampuni 16 za wazawa zinashiriki kwenye mradi huo katika ujenzi wa reli ya kisasa kama wakandarasi, wasambazaji na bidhaa na watoa huduma.

“Lengo ni kuwapo na ushiriki wa kampuni za wazawa na kujifunza kutoka kwa wakandarasi wa kigeni. Katika maradi huu kuna wafanyakazi 60,500 ambao Watanzania ni asilimia 96 na asilimia nne ni wageni kutoka nje.”

Anasema pia TRC inaandaa timu ya Watanzania vijana watakaoajiriwa na kupatiwa mafunzo maalum ili waweze kupokea mifumo hiyo mipya inayojengwa kwa teknolojia ya kisasa na hatimaye waweze kufanya uendeshaji na matengenezo ya mfumo yote ya SGR.

“Vijana hawa watajengewa uwezo ndani na nje ya nchi na tayari wameanza kutoa mafunzo kwa vijana 110 ambao ni wahitimu wa shahada mbalimbali zitakazohitajika katika uendeshaji wa mifumo ya SRG na baadae 110 wataenda nchi mbalimbali," anasema Mhandisi Kadogosa.

FAIDA ZA MRADI

Kwa upande wake Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Patrick Balozi, anasema reli hiyo ni mhimili mkubwa katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kupeleka mapinduzi kwenye sekta ya viwanda, kilimo, ujenzi, ufugaji, usafirishaji, madini na utalii.

Anasema utarahisisha usafiri na kuchochea uanzishwaji wa miji midogo katika sehemu zilizojengwa stesheni ambazo zitakuwa kivutio kwa wananchi mfano maeneo ya Soga, Ruvu na Kwala kwa mkoa wa Pwani, anasema pia mradi huo utaajiri vijana wengi wa Tanzania na hivyo kuongeza fursa za ajira nchini.

Anasema ni mradi unaowanufaisha Watanzania wengi lakini pia unabadili historia ya nchi. Kwa namna ulivyo ni wa kukomboa uchumi wa Watanzania, vijana wengi wakiwa kazini wakiwamo wanawake watapata kazi.