ILIVYO KAMPENI MAALUM SERIKALINI KUWAPAISHA KINAMAMA KIUCHUMI

14Feb 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
ILIVYO KAMPENI MAALUM SERIKALINI KUWAPAISHA KINAMAMA KIUCHUMI

SEKTA ya Maendeleo ya Jamii nchini, hivi sasa kitaifa imo katika orodha ya mafanikio makubwa katika kuhakikisha jamii inajiletea maendeleo, kwa kutumia fursa zilizopo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, akishiriki ujenzi wa vyumba vya bweni la wasichana wa Shule ya Sekondari Kirare, jijini Tanga ikiwa, kuunga mkono juhudi za wananchi. Kushoto ni Diwani wa Kata. Jirani ni Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa. PICHA: HISANI YA WIZARA.

Inawezekana kukawapo maeneo mtambuka katika tathmini hiyo, lakini Nipashe imeangukia katika sura kuu tatu, chini ya kivuli cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Hapo panatajwa: Uwezeshaji wanawake kiuchumi, huduma kwa wazee, ustawi wa watoto na usimamizi wa mashirika yasiyo ya kiserikali. Majukumu hayo yote yaaangukia katika Idara ya Maendeleo ya Jamii.

Ni idara inashughulikia masuala ya ustawi na jinsia kwa kuweka kipaumbele katika kuwezesha wanawake kiuchumi.

UWEZESHAJI WANAWAKE

Katika jitihada za Wizara kuwezesha wanawake kiuchumi, Serikali kupitia Benki ya Posta Tanzania, imeendelea kuwawezesha wanawake kupata mikopo yenye masharti nafuu katika mikoa 26 nchini, kiasi cha Sh.Bilioni 2.5 zimetolewa kwa wanawake wajasiriamali 3,035 wa mikoa 26 nchini.

Pamoja na mikopo ya masharti nafuu, serikali pia imeendelea kuhamasisha wanawake kujiunga na vyama vya ushirika wa kuweka na kukopa, maarufu Saccos zipatazo 130 zilizoanzishwa katika mikoa Mara, Mwanza, Tanga, Kigoma, Dodoma, Kagera, Shinyanga, Simiyu, Rukwa, Ruvuma, Mbeya, Lindi, Mtwara, Geita, Manyara na Dar es Salaam.

Ripoti iliyopo ni kwamba, serikali imekuwa ikitoa mafunzo kuhusu urasimishaji na uboreshaji bidhaa na kuunganishwa na Mamlaka za Udhibiti wa Ubora wa Bidhaa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), yaliyotolewa kwa wanawake wajasiriamali 7,713 ili kuongeza ubora wa bidhaa na kuwawezesha kupata taarifa za masoko ya bidhaa zao.

Pamoja na utoaji mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake, inaelezwa serikali pia imeendelea kutenga fedha asilimia tano kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake katika Halmashauri 185.

Aidha, serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko huo unaongezeka kila mwaka, Sh.Bilioni 3.4 zilitolewa mwaka 2016/17; Sh. bilioni 8.8 mwaka 2017/18; Sh. bilioni 16.3 na mwaka 2018/19; Sh. bilioni 11.1 zilitolewa kuwezesha wanawake wengi zaidi kuinuka kiuchumi.

NGUVU KWA WANAWAKE

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mkoa Rukwa mwaka 2018, Waziri mwenye dhamana, Ummy Mwalimu, anawataka Wakurugenzi wa Halmashuri zote nchini kutenga asimilia nne kwa ajili ya mikopo ya wanawake yenye tija, itakayoweza kuwasaidia kuongeza vipato vya kujikwamua kiuchumi.

Waziri Ummy anasisitiza kufikia azma ya Tanzania ya Viwanda, halmashauri hazina budi kujiwekea mikakati ya utoaji mikopo mikubwa itakayowawezesha wanawake na wananchi kwa ujumla kufikia azma zao.

Kuhusu utekelezaji wa agizo hilo kutoka kwa Waziri, kuna halmashauri 185 zimetoa Sh.Bilioni 39.7 katika Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ndani ya miaka minne, ikinuia kuwezesha mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake
wajasiriamali 877,071.

Serikali, pia imeshafanya uhamasishaji kwa wanawake wajiunge na mifuko ya hifadhi ya jamii na kutoa mafunzo kwa wanawake wajasiriamali 207 wa Mkoa wa Mwanza, kuhusu namna ya kujiunga na mifuko hiyo.

SHERIA MPYA

Sheria ya Fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa imeongezewa kifungu kuzielekeza halmashauri zote kuchangia asilimia 10 ya mapato yao ya ndani, kwa ajili ya mikopo ya masharti nafuu kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Hiyo imeenda na utaratibu wa kuondoa kero kwa wajasiriamali wanawake, kwa mamlaka za serikali za mitaa zinawajibika kutenga maeneo ya biashara kwa wajasiriamali, wakiwamo wanawake na sasa kuna halmashauri 150 zimeshatenga maeneo ya biashara na viwanda.

Pia, serikali imetenga maeneo rasmi yenye ukubwa wa hekta 15,822.64 kwa ajili ya biashara kwa wajasiriamali, Hapo inajumuisha mama lishe, wauza mboga katika mikoa ya Arusha, Iringa, Mara, Rukwa, Tanga, Shinyanga, Mwanza, Kilimanjaro,
Singida, Morogoro, Singida, Manyara, Njombe, Kagera, Dar es Salaam, Dodoma, Lindi, Geita, Tabora na Ruvuma.

HUDUMA WAZEE

Idara hiyo imekuwa na jukumu la kushughulikia ustawi wa wazee nchini na imendelea kuhakikisha wazee wanatambuliwa na kupatiwa huduma za matibabu bila malipo.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee Duniani hivi karibuni mkoani Mtwara, Waziri Ummy, anasema serikali imewatambua wazee 1,897,021 katika halmashauri 185, ndani ya mikoa 26 ya Tanzania Bara, wazee 766,227 walipatiwa vitambulisho vya matibabu sawa na asilimia 40 ya wote wanaostahili.

Waziri Ummy, anaongeza kufikia Juni, 2019 idadi ya wazee waliopatiwa vitambulisho vya matibabu bure wameongezeka kutoka 213,025 akiwataja wanaume kuwa 106,129 na wanawake 106,896 mwaka 2015/16 hadi kufikia wazee 766,227. Kati yao wanaume wako 391,647 na wanawake 374,577.

Katibu Mkuu, anayeshughulikia idara hiyo, Dk. John Jingu, anasema serikali inatoa huduma za msingi za chakula, malazi, mavazi na matibabu kwa wazee wasiojiweza wanaoishi katika makazi 16 ya wazee yanayomilikiwa na serikali.

Dk. Jingu pia anasema, Mkakati wa Kutokomeza Mauaji ya Wazee (2018 - 2023) umeandaliwa ili kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu haki za msingi kwa wazee na kuongeza kuna wabaraza ya wazee 8,183 yameanzishwa katika halmashauri kuwezesha upatikanaji haki kwa wazee nchini.

USTAWI WATOTO

Dk. Jingu anasema, ili kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya uonevu, ukatili, udhalilishaji, utumikishwaji
na mila potofu, serikali imeanzisha Mtandao wa Mawasiliano ya Simu Namba 116, ili kuwezesha jamii kutoa taarifa za vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Kupitia mtandao huo, kuna jumla ya watoto 3,833 waliofanyiwa ukatili waliwezeshwa kupata huduma za chakula, vifaa vya shule, huduma za sheria na afya.

Anasema serikali imeanzisha vituo vya huduma jumuishi za pamoja kushughulikia wanaosumbuliwa na katika mikoa tisa nchini anayoitaja kuwa ni: Mbeya, Dar es Salaam, Pwani, Kilimanjaro, Arusha Shinyanga, Iringa, Mwanza na Tabora.

Lingine linalotajwa katika hilo, kuna Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 11,520 zimeanzishwa, katika mgawanyo maalum: Mbili katika ngazi ya taifa; zingine 26 ngazi ya mkoa; 112 katika ngazi ya halmashauri; 2,592 ngazi ya kata; na 8,788 ngazi ya kijiji/mtaa.

Dk. Kingu anasema serikali imeratibu upatikanaji huduma za misingi za malazi, chakula, mavazi, matibabu na elimu kwa watoto walio katika mazingira hatarishi, wanaoishi katika makao ya watoto katika mikoa 26.

“Watoto wanaoishi katika makao ya watoto wanaongezeka kila mwaka ambapo mwaka 2015/16 makao ya watoto yalihudumia watoto 4,379, mwaka 2016/17, watoto 4,515; mwaka 2017/18, watoto 6,132; na mwaka 2018/19, watoto 13,420,” anasema

Katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika mwaka huu mkoani Geita, Waziri Ummy, anasema katika kuimarisha haki ya ushiriki wa mtoto, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuhimiza Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuongeza bajeti ya kuwezesha utendaji wa mabaraza ya watoto.

Anasema mabaraza hayo yanatoa fursa kwa watoto kujadili masuala mbalimbali yanayohusu haki na ustawi wao na pia kuishauri Serikali kuhusu masuala hayo.

Vilevile, Waziri Ummy anasema mpaka kufika Machi, mwaka huu serikali ilianzisha mabaraza ya watoto 19 katika ngazi ya mikoa, mabaraza 121 katika ngazi ya halmashauri za manispaa, wilaya, miji.

Aidha katika ngazi za kata kuna jumla ya mabaraza 733, sambamba na kuwapo mabaraza 795 katika ngazi ya kijiji ambayo, yamekuwa na mchango mkubwa.

Katika kuimarisha ustawi na maendeleo ya familia nchini, anasema wizara hiyo yenye dhamana na ustawi wa jamii, imetoa mafunzo ya malezi chanya kwa wazazi na walezi 635 kwenye ngazi ya familia ndani ya jumla ya halmashauri 132 katika mikoa 26 nchini, kuhusu stadi za malezi chanya kwa watoto.

Aidha, elimu hiyo imewezesha kuanzishwa kwa vikundi vya Malezi 1,184 katika halmashauri 15 za mikoa saba.

USIMAMIAJI NGO

Pia, kwa kipindi hicho serikali imeendelea kusajili, kufuatilia na kuratibu shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali, ili kukuza mchango wako katika kusaidia jamii kufikia maendeleo yao.

Taarifa iliyopo ni kwamba, serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa uratibu wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) unaowezesha kufanyika kwa malipo ya ada mbalimbali, inayotekelezwa na asasi hizo zisizo za kiserikali na wanufaika miradi.

Pia, anataja kwamba ni mfumo unaosaidia kujua kiasi cha fedha kilichotumiwa na wafadhili kwa miradi inayotekelezwa, ili kujenga uwazi na uwajibikaji, sambamba na kuboresha uratibu wa mashirika kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Taifa.

Habari Kubwa