Inahitajika hamasa kilimo DSM, mvua miezi 8 yaneemesha mapori

14Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Inahitajika hamasa kilimo DSM, mvua miezi 8 yaneemesha mapori

WATAZANIA wengi huenda wameanza kuelewa masuala ya mabadiliko ya tabianchi, lakini kuna uwezekano kuwa hawayatilii maanani, licha ya kuyazungumzia na kuyafuatilia.

Visumbufu vinavyoshambulia mazao. PICHA ZOTE: MTANDAO.

Kinachoonekana kuwa hakijafanyika ni kuchukua hatua kukabiliana na mabadiliko hayo na kujua kuwa kila kunapokuwa na mabadiliko chanya ni lazima kufanya jambo.

Mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya kubadilika kwa hali ya hewa kunakoletwa na ongezeko la joto duniani kutokana na kuharibu anga za juu ambazo zinasababisha mionzi mikali ya jua kupenya na kuifika duniani.

Huenda wengi wanaamini kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi zinamhusu mkulima au mfugaji zaidi kwa vile ndiye anayetegemea ardhi na mvua, bila kujua kuwa madhara yapo kwa kila binadamu.

Athari hizi zinawagusa wote kwa kuwa joto na fukuto kali mathalani, hukausha maji mwilini na kuongeza uwezekano wa kuwa na maradhi ya kuwa na mawe kwenye figo, kupata magonjwa ya ngozi hata saratani inayotokana na kupenya kwenye ngozi mionzi mikali ya jua maarufu kama ultra violet rays (UVA).

Mabadiliko ya tabianchi yanawalazimu wengi kubadilika na kuona kuwa ni zama za kuchukua hatua kulingana na misimu ikiwa na mvua watu kulima na kufuga zaidi pamoja na kutunza maji.

KUPUUZA MVUA

Kuanzia Oktoba mwaka 2019 hadi Oktoba 2020, mvua ilinyesha kiasi cha kutosha na katika mikoa mingi ikiwamo Dar es Salaam.

Utafiti uliofanywa na Nipashe sehemu mbalimbali Dar es Salaam, wakati wa kipindi hicho, unadhihirisha kuwa watu hawajabadilika kifikra na wala hawathamini mvua hasa kuitumia kwa kilimo.

Mvua iliyoanza Oktoba hadi Mei 2020, ikinyesha miezi nane ni msimu ambao masika na vuli viliungana, lakini licha ya kunyesha huko, watu wengi Dar es Salaam hawakuwa na hamasa ya kujishughulisha na kilimo.

Nipashe ilitembelea maeneo mengi kama Madale, Msumi, Makabe, Kibamba, Kiluvyia na Kibaha na kugundua kuwa kuna sehemu nyingi zenye mashamba na viwanja ambavyo havijajengwa.

Japo watu walishuhudia mvua kwa karibu mwaka mzima, watu hawakujishughulisha na kulima mahindi, kunde, mihogo, mabogo na mazao mengine yanayostawi ukanda huo.

Pengine mvua ya miezi nane ambayo ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi, ilitegemewa kuwa fursa ya kupanda mihogo, viazi, mbaazi, migomba na matunda hasa mapapai lakini hakuna jitihada za kutosha za kusafisha vichaka ambavyo baada ya mvua vimezidi kuimarika na kuwa makazi na wanyama na wadudu.

Wakazi wengi wa Dar na mikoa mingi nchini tangu Mei hadi mwezi huu wanalalamikia upepo mkali ambao unakausha maji kwenye madimbwi, mazao hasa matunda, unavunja miti na kusababisha vumbi kujaa ndani ya nyumba.

Baada ya mvua ya miezi nane sasa ni upepo wa takriabni miezi mitatu ukivuma mchana na usiku, lakini maghala yao hayana akiba ya chakula wala maji.

Huenda wakazi wa Dar es Salaam wanakosa wahamasishaji, hivyo ni wakati wa kuamua namna ya kuhamasisha watu kutumia mapori na kulima chakula wakati wa mvua.

Mazungumzo na baadhi ya wakazi wa Dar yanaonyesha kuwa wanafahamu kuwa kuna mabadiliko lakini wanakosa hamasa ya kuhimiza kilimo.

Jimmy Mbajo, anayeishi Madale anasema kilimo Dar kina changamoto nyingi kama ongezeko la wadudu wanaoshambulia mapapai, mboga, mastafeli na mapera lakini hakuna maofisa ugani wanaowapa ufumbuzi na kuwahamasisha kulima.

“Kuna panzi na funza wengi wanashambulia mahindi. Mhindi ukichipuka unashambuliwa. Unaweza kupanda lakini ikiwa kazi ngumu kupata mazao. Ili kuvuna utahitaji kutumia dawa kwa wingi kuua wadudu.”

Anazungumzia suala la ukungu na wadudu wanaoibuka na kushambulia mazao kama matunda hasa mapapai na maembe, mapera mboga za majini na kusababisha majani na matunda hayo kuwa myeusi au myeupe kama yamemwagiwa unga au chokaa.

Anasema hali ilivyo kilimo bila viuatilifu na mbolea kwa wingi kinaweza kisifanikiwe na kwamba njia za asili za kuangamiza wadudu kama vile majani yenye dawa ya muarobaini au minyaa au aloivera hazisaidii kuua wadudu hao wakali wanaozaliana kwa kasi zama hizi, ndiyo maana watu huogopa kulima.

Lakini pia, anaeleza kuwa ukame unaleta usugu wa vimelea vinavyosambaza magonjwa kwenye mazao mfano matunda yanashambuliwa na ukurutu mweusi unaosababishwa na fangas. Machungwa, ndimu, maembe na mafenesi ni miongoni mwa mazao yanayopata ukurutu huo ambao wakati mwingine hausikii dawa.

Wakulima wanahisi kuwa licha ya mahindi kuwa chakula kikuu cha Watanzania huenda hayastawi Dar es Salaam, ndiyo maana wanasita kupanda.

Wanasema wengi hawalimi kwa sababu wanakosa mahindi licha ya kutumia mbegu za kisasa, mbolea, dawa na nguvu nyingi.

Gazeti hili liliwatembelea wauza mbegu hasa za mahindi sokoni Kariakoo, katika mahojiano wanaeleza kuwa kila ukanda una mbegu zake na pwani zipo za kutosha.

Wauzaji hao wanasema pengine wakati umefika wa kuweka maofisa ugani kwenye ofisi za kata ili kuhamasisha kilimo Dar na pia kuelezea umuhimu wa kutumia mbolea za kupandia na kukuza mahindi.

“Ni kweli ni lazima kutumia mbolea kama DAP kupandia, lakini pia za kukuzia na ‘booster’ ambayo ni mbolea ya majani na CAN kuzalisha na kuimarisha mbegu. Tusisahau viuatilifu ili kuangamiza visumbufu,” anasema Vincent Ngomuo, anayeuza mbegu na pembejeo Kariakoo.

MVUA ZA KWANZA

Yusufu Msonde, mkazi wa Mitamba mkoani Pwani anasema wakulima hawajahamasika na dhana ya mvua za kwanza ni za kupandia.

“Wanahitaji msukumo mpya mvua zikinyesha ni lazima kupanda bila kujali uko Dar es Salaam au Dakawa. Tuendelee kuamini kuwa mvua za kwanza ni za kupandia si kutayarisha mashamba.

“Mvua ikinyesha tupande tusipoteze wakati tena uwe umeandaa ama hujatayarisha shamba anza kulima, mvua ya miezi nane haikutakiwa kutuacha Wanadar es Salaam na njaa.” Anasema mkulima huyo.

Anasema ni wakati kwa wakulima wa Dar kujua kuwa kuna ukame na joto kali hivyo watumie mbinu ya kilimo mchanganyiko mfano wapande mazao ya aina mbalimbali kwenye shamba moja.

“Tuchanganye mihogo, mtama, kunde, mbaazi , mahindi na choroko kwa kuwa hakuna uhakika iwapo mvua itaendelea hadi mwisho wa msimu ama kutakuwa na mabadiliko.” Anaongeza Msonde.

Habari Kubwa