INJINIA RAMSON “Ikifika 2020 narusha ndege ninayounda mwenyewe”

11Mar 2017
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
INJINIA RAMSON “Ikifika 2020 narusha ndege ninayounda mwenyewe”

UKIWA chini ya jua mwenye nguvu, afya na akili ni lazima uhakikishe unatimiza ndoto zako bila kuangalia ni vikwazo gani utakumbana navyo. Ndiyo msimamo na dhamira ya mhandisi ambaye sauti yake haijasikika wala kazi zake kupata sifa anazostahili.

Ramadhan Omary au Ramson.

Huyu ni Ramadhan Omary au Ramson, mkazi wa Manzese Dar es Salaam, anayeamini kuwa kusudio lake la kurusha helkopta aliyoitengeneza kwa mikono yake litatimia mwaka 2020 ikiwa anafikia miaka 49 , tangu alipoanza jitihada hizo.

Mwaka 2008, naweza kusema ulikuwa wa mafanikio ya ubunifu kwa Omary. Ndiyo wakati ambao alitengeneza helkopta ya kwanza na ya aina yake huko Manzese, lakini hakutoka kutokana na changamoto mbalimbali zilizomrudisha nyuma ikiwa ni pamoja na kukosa kibali cha kuirusha kutoka serikalini.

Chombo hicho kimebakia kuwa sehemu ya kumbukumbu ya ubunifu wake na makumbusho kwa wananchi wa Manzese.

Anasema kazi ya kuunda helkopta hiyo alimfikirisha kwa muda wa miaka mitatu na kwamba ilipofika 2010 ilikuwa imekamilika na kuanza harakati za kutafuta kibali ili aweze kuirusha kwa majaribio.

Anasema licha ya changamoto alizokutana nazo nyakati hizo hajakata tamaa pamoja na kwamba helkopta hiyo imeishia `kuwekwa juu ya mawe’ tena mbele ya baa moja huko Manzese na kuwa sehemu ya kivutio cha wateja wanaofika hapo, hajakata tamaa.

“Ndoto yangu ni kuirusha hewani helkopta ambayo nimeitengeneza kwa mikono yangu mwenyewe, sijakata tamaa ndiyo maana nimeanza kuunda helkopta nyingine ambayo itakamilika na kuanza kazi mwaka 2020. Nina miaka mitatu ya kukamilisha jukumu hili.”

“Helkopta ya sasa ambayo nimeanza kuiandaa mwaka jana,nikiilinganisha na ya awali naona kuna tofuati ya wakati huu ninatumia vifaa vya kisasa na ninaiboresha zaidi,” anasema.

Omary anasema helkopta ya sasa itatumia miaka minne kukamilika kwa sababu ya kukosa mfadhili. Ile ya mwanzo alipata msaada wa fedha uliomwezesha kutimiza ndoto hiyo.

Anasema kazi ya kutengeneza helkopta nyingine inafanyika mkoani Morogoro ambako anaamini hatapata vikwazo vya kuirusha kama ilivyokuwa hapo awali.

“Ile ya mwanzo niliitengenezea Manzese eneo ambalo lina makazi ya watu kwa hiyo haikuwa rahisi kuirusha na nilitumia vifaa ambavyo si vya kisasa kama hii ya sasa,” alisema.

Anaeleza kuwa ubunifu wa helkopta hiyo umefikia katika hatua za kujivua na anaamini ndoto yake itatimia kwa asilimia 100.

HISTORIA YAKE
Omary anasema alizaliwa mwaka 1956 na alimaliza kidato cha nne mwaka 1973 katika Shule ya Sekondari Dodoma Day, huku elimu ya msingi akiipatia katika Shule ya Iguguno iliyopo Iramba mkoani Singida ambako ndiko nyumbani kwake.

Anasema alibaini kuwa ana kipaji cha ubunifu tangu akiwa shule ya msingi ambako muda wa ziada akiwa nyumbani kwao, aliutumia kutengeneza magari ya ya watoto.

Aidha, anasema alikuwa akitumia bati, mbao na betri za simu za shirika la Posta na Simu (wakati huo halijavunjwa ili kuunda kampuni ya Simu TTCL na kulitenganisha kama ilivyo sasa) ambazo alizutumia kama magurudumu.

Anabainisha kuwa wazo la kutengeneza helkopta alilipata akiwa anajifunza ufundi magari.

“Mwaka 1971 nikiendelea kutumia muda wa ziada kujifunza magari, mjomba wangu Hatibu ambaye aliyekuwa fundi (makenika), mara kwa mara alikuwa akinisimulia kisa mkasa kilichompata baada ya kubuni ndege ndogo iliyomsababishia kwenda kujificha kwa hofu ya kukamatwa wakati huo,” anasema.

“Mjomba japo sasa ni marehemu, aliniambia mwaka 1949 alitengeneza ndege ndogo anayosema haikutumia mafuta lakini kwa kuhofia kukamatwa alikimbilia Mwanza kujificha.”

Anasema alianza kupata msukumo wa kutengeneza helkopta baada ya mara kwa mara mjomba wake kumsimulia ubunifu wake.

“Ingawa sikumshirikisha kwenye mipango hii pengine kama fundi na mshauri, niliaanza safari ya kutimiza ndoto yangu mwaka 2008 hadi naikamilisha mjomba wangu bado alikuwa hai na alikuwa akinitia moyo,” anasema.

NISHANI

Kazi yake ilipata kibali mbele ya watafiti wanaohimiza uendelezaji wa vipaji mwaka 2011 alipata nishani inayotolewa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ya Tanzania Award for Scientific and Technological Achievements (Tasta), aliipata kwa kutambua ubunifu wa helkopta hiyo.

Aidha, mbali na nishani hiyo, Omary anasema alizawadiwa Shilingi 5,000,000 zilizomsaidia kuendeleza ubunifu wake kwenye vitu vingine vya kieletroni.

“Pamoja na kuunda ndege, ametengeneza mtambo mdogo wa kutengeneza vipuri vya bodaboda na anaomba wahisani wamsaidie ili azalishaje vipuri nchini.

WITO SERIKALINI
Mbunifu huyo anaishukuru serikali kwa mikakati yake ya kufufua viwanda akisema:

“Wito wangu kwa serikali wakati hili linafanyika lazima wahakikishe ndani ya viwanda hivyo kunakuwa na wabunifu wazawa kama sisi ili haya tunayovumbua yaweze kufika mbali na siku moja Tanzania tujivunie vipaji vyetu.” .

Aidha, amezitaka taasisi za serikali zenye dhamana ya wabunifu ziendeleze vipaji hivyo kwa vitendo.

“Mbunifu anashindwa kutimiza ndoto kwa sababu ya kukosa msaada , naomba tuthaminiwe, nitakuwa Mtanzania wa kwanza kurusha helkopta ambayo nimeitengeneza mwenyewe,” anasema.

Habari Kubwa