Itapendeza wabunge wakiiga mfano wa Profesa Tibaijuka

06Dec 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Itapendeza wabunge wakiiga mfano wa Profesa Tibaijuka

HIVI karibuni mbunge wa Muleba Kusini mkoani Kagera, Profesa Anna Tibaijuka (CCM) alitangaza kuwa hatagombea tena ubunge mwaka 2020, na badala yake atatoa nafasi kwa vijana ili maarifa yake yaweze kutumika kushauri nini kifanyike ili kupeleka maendeleo mbele.

“Na kuaga nimeshaaga na wananchi wameniamini. Napenda tuwape nafasi vijana. Kuzeeka haimaanishi maarifa yangu yaondoke kwa sababu nimestaafu, tunawapa nafasi vijana washike nchi,” alisema na kuongeza:

 

“ Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema tung’atuke…na mimi nang’atuka ili maarifa yangu yaweze kutumika kushauri tufanye hivi ili twende mbele.”

 

Msomi huyu amekuwa mbunge tangu mwaka 2010 na anajiandaa kung'atuka akiwa ametumikia jimbo lake kwa vipindi viwili, tofauti na wabunge wengine wasio na mpango wa kustaafu ambao hufanya 'figisufigisu' kuhakikisha wanaendelea kushikilia nafasi hiyo.

 

Uamuzi wa Prof. Tibaijuka ni vyema ukaigwa na wabunge wote, kwani wapo baadhi yao ambao wameongoza majimbo kwa miaka mingi na hawana dalili za kung'atuka ili kuwaachia wengine wenye mawazo mapya.

 

Siyo kwamba wazee hawafai kuwa wabunge, bali mtu anapoongoza kwa miaka mingi anapaswa apumzike na kuachia wengine wenye mawazo mapya nao washike nafasi badala ya kung'ang'ania tu hata kama wananchi wamewachoka.

 

Katika mazingira haya ndiyo maana nashangazwa na kauli ya mbunge mmoja aliyewahi kukaririwa na vyombo vya habari akisema hawezi kuachia ubunge, kwa madai kwamba hajaona mtu wa kumwachia jimbo na yupo tayari kuwa king'ang'anizi kama Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe!

 

Wabunge wa aina hii kama wananchi wamewachoka dawa yao ni kuwanyima kura tu kwani kwa kawaida mbunge wa jimbo anachaguliwa na wananchi na hakuna utaratibu wa kujichagua. Kwanini aseme kuwa hajaona mtu wa kumwachia jimbo?

 

Kila mtu ana haki ya kuwania nafasi yoyote ya uongozi ili mradi ametimiza masharti na vigezo vinavyohitajika kulingana na nafasi anayoitaka, sasa iweje baadhi ya majimbo yawe ni milki ya watu fulani tu?

 

Binafsi ninachukulia nafasi ya ubunge au udiwani kama mbio za vijiti ambazo kwa kawaida ni kupokezana, lakini baadhi ya wanasiasa wamekuwa hawataki kuwaachia wenzao nafasi.

Kila unapofanyika uchaguzi unakuta wabunge ni walewale na wapo ambao wamedumu kwenye nafasi hiyo hata kwa zaidi ya miaka 20 na hawaonyeshi dalili au mpango wa kustaafu ili wawaachie vijana.

 

Bila kuwa na utaratibu wa kung'atuka mapema, wazee wataendelea kuongezeka bungeni huku idadi ya vijana wenye mawazo mapya ikizidi kuwa ndogo, kwani nakumbuka mwaka 2015 serikali ilikiri bungeni kuwa asilimia 20 ya wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni wazee wenye umri wa kati ya miaka 60 na kuendelea.

 

Waziri wa Nchi Katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama ndiye aliyesema hayo baada ya kuulizwa kuhusu wazee kupata uwakilishi katika vyombo vya maamuzi kama Bunge na maeneo mengine.

 

Uamuzi aliouchukua Prof. Tibaijuka wa kung'atuka ni mfano wa kuigwa kwani ametambua kuwa wapo vijana wenye mawazo mapya ambao mchango wao unahitajika kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii, hivyo itapendeza iwapo wabunge wengine watamuiga.

 

Niwakumbushe wabunge ving'ang'anizi kuwa mwaka 2005, mwanasiasa mkongwe nchini, ambaye kwa sasa ni marehemu, mzee Peter Kisumo aliwataka baadhi ya wagombea urais wazee kutogombea nafasi hiyo, badala yake wawaachie nafasi hiyo wagombea vijana.

Wakati mzee Kisumo alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na alitoa kauli hiyo alipokuwa akimsindikiza Jakaya Kikwete kutangaza nia ya kugombea urais.

 

Mwaka 2010, Kisumo alirejea kauli hiyo lakini akiwalenga wabunge na madiwani wazee ambao wameshikilia nyadhifa hizo kwa miaka mingi wasione nongwa kuwaachia vijana akisisitiza kutokana na mabadiliko ya sasa, kunahitajika damu changa.

 

Mdhamini huyo akasema kuwa wapo vijana ambao wamejifunza uongozi na wana sifa za kuiongoza nchi kwa uadilifu mkubwa, hivyo wanapaswa kupewa nafasi ili walitumikie taifa lao.

Mbali na kauli yao hiyo, akawapongeza mbunge wa Kwela, Chrisant Mzindakaya na Paul Kimiti wa Sumbawanga kwa kuamua kwa hiyari yao kutogombea tena ubunge akisema wameonyesha mfano na akawataka wazee wengine kuuiga.

 

Kauli kama ya mzee Kisumo ilikuja kutolewa baadaye na Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya nne, Mizengo Pinda pale alipowashukia wabunge ving'ang'anizi ambao wapo bungeni kwa miaka lukuki na kukataa kung'atuka.

 

Ilikuwa ni mwaka 2010 alipowashukia wabunge wa aina hiyo wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nchini na kugusia mambo mbalimbali ambayo yalikuwa yakiikabili nchi.

Waziri Mkuu Pinda akasema kuwa wakati umefika kwa wabunge ambao wamekaa kwa muda mrefu madarakani kuwapisha wengine kwani wapo wengi wenye uwezo wa kuongoza.

 

Kama hiyo haitoshi Waziri Mkuu Pinda akasema Tanzania imejaa watu walioelimika na ambao wanaweza kuwa wabunge mahiri na

kuwataka waige mfano wa marehemu Mzee Mfaume Kawawa, ambaye aling'atuka madarakani akiwa bado na umri mdogo.

 

Ushauri wa mzee Kisumo na Pinda hauna budi kufuatwa na wanasiasa wakitambua kuwa uongozi ni kuachiana kama ambavyo mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Prof. Anna Tibaijuka ametangaza kutogombea tena ubunge.