Jamii inavyohamasishwa dawa asili ili kuepuka maambukizi ya corona

25Feb 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Jamii inavyohamasishwa dawa asili ili kuepuka maambukizi ya corona

JANGA la virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-190 lilipotangazwa mara ya kwanza, dunia nzima ilitaharuki na hata wengine kudhani kuwa ndio mwisho wa maisha yao.

Hata hivyo, tangu kuibuka kwa janga hilo Aprili, mwaka jana, serikali za nchi mbalimbali, ikiwamo Tanzania zilichukua hatua kuhakikisha zijapambana na janga hilo.

Serikali ya Tanzania kwa upande wake, iliwataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi kwa kukaa umbali wa mita moja kutoka mtu mmoja hadi mwingine, kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka.

Sambamba na hiyo, iliwataka watu kujiepusha na mikusanyiko kama vile misiba, mikutano, ibada na maeneo yenye watu wengi kama vile sokoni na vituo vya mabasi. Kama vile haitoshi, ilichukua uamuzi mgumu wa kufunga kwa muda usiojulikana shule na vyuo.

Hatua zingine zilizochukuliwa ni kuwataka watu kujifukiza, maarufu kama nyungu, pamoja na kutumia dawa asilia katika kupambana na COVID- 19. Hilo ndilo limekuwa likisisitizwa na kupewa kipaumbele zaidi.

Mkurugenzi wa Kuratibu na Kukuza Utafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Paul Kazyoba, anazungumzia umuhimu wa matumizi sahihi ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza. Uhamasishaji huo umekuwa ukisisitizwa tangu kutangazwa kwa janga hilo ili kusaidia kuongeza kinga za mwili au kutibu maradhi.

Akizungumza na Nipashe katika mahojiano maalum yaliyolenga kufahamu matumizi sahihi ya tiba asili ili kupunguza madhara yanayoweza kutokea endapo zitatumiwa holela, Dk. Kazyoba anasema ni lazima wananchi wajiridhishe kwanza kabla ya kuzitumia.

Anafafanua kuwa ni lazima mtumiaji ajiridhishe tiba asili anayoitumia kama zimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na kuthibitishwa na Mkemia Mkuu wa Serikali. Anasema kuna idadi kubwa ya wataalam wa tiba asili nchini na miongoni mwao wako waliosajiliwa na wengi hawajasajiliwa na baraza.

“Kwa mfano kwenye dharura ya ugonjwa wa corona au mlipuko mwingine wowote, ukiangalia kuna dawa nyingi zimesajiliwa na baraza ili zitumike na kuna idadi kubwa ya watu wanajitangaza kuuza dawa zao,” anasema.

Hata hivyo, Dk. Kazyoba anasema matatizo wanayoyaona watafiti pengine na madaktari wanayazungumza kila mara ni kwamba tiba asili ni huduma yenye fursa duniani na watu hujipatia kipato, hivyo lazima kutakuwapo na wataalam wa tiba asili ambao ni ‘feki’.

“Wanajaribu kukopi (kunakili) dawa za wenzao na kuziwekea ladha nyingine na kuziweka sokoni ili wapate fedha. Hii ndiyo hatari kubwa ninayoiona.

“Jambo la msingi tunashauri watumaji kabla ya kuzitumia wapate maelezo ya kina kutoka kwa wataalam wa tiba asili au wauzaji. Hakuna dawa iliyotengenezwa na kutokuwa na maangalizo,” anasema.

Anasema kutoa huduma ya tiba asili inayozingatia vigezo au sheria ya tiba asili, tiba mbadala na miongozo ya Baraza la Tiba Asili, inabaki kuwa msingi katika kuhakikisha zinakuwa salama na tija kwenye kutibu magonjwa.

“Mambo wanayotakiwa kufanya ni kujisajili kwenye baraza ukisajiliwa vipo vigezo ambavyo vinaangaliwa, watakagua unakotengenezea dawa, uandaaji wake, namna unavyozifungasha na kuzitoa,” anasema.

Mtafiti huyo anasema kuna umuhimu wa wataalam wa tiba asili kusimama katika miongozo ya baraza na sheria ili kuhakikisha watumiaji wanakuwa salama.

Ili dawa ithibitike kuwa salama, mtaalam wa tiba asili anatakiwa aipitishe kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ili iangaliwe kemikali iliyomo kama ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Dk. Kazyoba anasema utafiti unaonyesha wagonjwa wengi walioonwa na wataalam wa afya mara nyingi hukutwa wanatumia dawa za kisasa na za tiba asili.

“Dawa za tiba asili zinatokana na mimea. Ni dawa chache ambazo kama zimetengenezwa kwa uaminifu na kuzingatia miti dawa ambayo ni salama zinaweza kuleta shida,” anafafua.

Mtafiti huyo anataja matatizo yaliyopo kuwa ni dawa nyingi za tiba asili hazijawahi kufanyiwa utafiti na kuona zikitumika na dawa za kisasa ni athari zipi zinaweza kutokea na kusisitiza kuwa ni vizuri mgonjwa kama amekwenda kwenye matibabu ya kisasa, amweleze daktari wake kama ana matumizi mengine ya tiba asili.

Dk. Kazyoba alitolea mfano dawa lishe ya NIMRCAF ambayo imetengenezwa na NIMR na kueleza kuwa mtu akiitumia na dawa yoyote ya kisasa kwa sababu asilimia 100 ni chakula, haina shida.

“Dawa hii ya NIMRCAF inapoingia ndani ya mwili kufanya kazi kwa haraka sana inawezekana ikaisaidia dawa yako. Ila ziko dawa nyingine ambazo zinatakiwa kuingia kwenye mfumo wa mwili taratibu, hivyo mtumiaji wa NIMRCAF lazima awe makini. Akinywa dawa yake akae saa moja au tatu ndipo anywe NIMRCAF,” anaelekeza.

Kwa mujibu wa Dk. Kazyoba, ziko dawa za kisasa ambazo mtumiaji akitumia hukaa kwenye mfumo wa damu muda mrefu, hivyo inapochanganywa na zinazofanya kazi haraka, huaribu mtiririko wa tiba.

Mtafiti huyo anabainisha kuwa kuna utafiti uliofanyika ambao ulilenga kuangalia kabla mtu hajaenda hospitalini huanzia wapi. Katika utafiti huo, anasema yako machapisho ya kisayansi yameonyesha kama una wagonjwa 100, asilimia 55 mpaka 60 ndio huenda hospitalini kupata tiba.

Anasema matumizi ya tiba asili na dawa za kisasa kwa mgonjwa imekuwa ni jambo la kawaida na kwamba yote bado yanahitaji utafiti wa kina ili kulisaidia Baraza la Tiba Asili kutoa miongozo.

WITO

Dk. Kazyoba aliwashauri wananchi kabla ya kununua dawa yoyote waulize maswali kuhusu usalama, tija ya dawa husika na kama baraza inaifahamu.

“Kama ni miti chakula dawa itakuwa salama lakini kama ni miti dawa inatakiwa ujiridhishe kwanza usalama wake, sheria ya tiba asili na tiba mbadala ya mwaka 2002 iliwekwa lengo ni kuhakikisha tiba asili inaendelezwa ili kuchangia kwenye sekta na pato la taifa lakini lazima usalama wa watumiaji usingatiwe,” anasema.

Anasema usalama unatakiwa kuzingatiwa kwa sababu tiba asili ni fursa na kwamba wapo watakoitumia kufanya utapeli kwa kutengeneza mchanganyiko na kuweka nembo na kuuza.

“Baraza limefanya kazi kubwa ya kuhamasisha na wamesajiliwa watu wengi ili kuhakikisha matumizi sahihi ya tiba asili Tanzania yanakuwapo na siziwe chanzo cha matatizo mengine,” anasema.

Mtafiti huyo anasema dawa za vimiminika zisipoandaliwa kwenye mazingira rasmi zina hatari kusababisha matatizo mengine kwa sababu ya vimelea vya bakteria na fangasi vinaweza kumea humo ndani kwa urahisi.

MATUMIZI KWA WATOTO

Dk. Kazyoba anasema kila dawa ina maelekezo na kama ziko zinazouzwa bila hilo ni tatizo.

“Haijalishi kama ni tiba ya asili au tiba ya kisasa lazima dawa iwe na maelekezo kwa mtumiaji ya nini afanye na nini asifanye, mfano NIMRCAF ina maelekezo watu wazima waitumiaje na watoto kuanzia umri gani inapendekeza wapewe vipi, dawa zote zinatakiwa kuwa na maelekezo na mwongozo wa baraza ndiyo unaelekeza hivyo,” anasema.

ATHARI KIAFYA

Dk. Kazyoba alikanusha kwamba siyo kweli matumizi ya dawa za tiba asili zinasababisha matatizo ya figo.

Dk. Kazyoba anasema ili kuondoa utata, eneo hilo linahitaji kufanyiwa utafiti ili kujiridhisha kama tiba asili inachangia matatizo ya figo.

“Kuchangia sikatai kwa sababu kama nilivyosema ndani ya sekta hii wajanja wajanja ni wengi ambao wanaweza kuchukua mti wowote akatengeneza dawa.

“Matatizo ya figo yanaweza kusababishwa na mambo mengi mfano ulaji wa dawa za kisasa ovyo ovyo usiothibitiwa.
Wataalam wenzangu lazima kufanyike utafiti inawezekana utumiaji dawa holela usiozingatia miongozo ya madaktari nao unaweza ukachangia kwenye matatizo haya tunayoyaona sasa hivi,” anasema.

Anasema upo utafiti ambao wanashirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kuangalia matatizo ya figo visababishi ni nini hasa.

Dk. Kazyoba anasema hayo ni mambo ambayo wanataka kuyafanyia utafiti kwa kuwa sababu ni nyingi ambapo zipo nyingine wanaziona lakini hawajui kama ndizo zinazochangia matatizo hayo.

Habari Kubwa