Janga dawa za kulevya

26Jan 2021
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Janga dawa za kulevya
  • *Chanzo maradhi yasiyoambukiza, ugaidi
  • *Kitisho uchumi, diplomasia, mazingira

DAWA za kulevya zinaendelea kuwaharibia maisha ya watumiaji kila kukicha na ndicho chanzo cha maambukizi ya maradhi yasiyoambukiza kama moyo, akili na figo wakati yanayoambukizwa ni kama Kifua Kikuu (TB) na homa ya ini.

Wanaojiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya wanakuwa hawajui, lakini linapokuja suala la kujiondoa kwenye uraibu, uhakika wa kufanya hivyo haupo.

Serikali kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, inatoa elimu kwa vijana jinsi ya kujikinga na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kueleza madhara ya matumizi yake.

Kamishna Msaidizi wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Dk. Cassian Nyandindi, anabainisha hayo katika mahojiano na Nipashe yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Anasema madhara ya matumizi ya dawa za kulevya ni makubwa yanayoweza kuainishwa katika makundi mbalimbali.

ATHARI KIAFYA

Anasema athari zake ni lukuki zikiwamo mtumiaji anazozipata papo kwa hapo na nyingine za muda mrefu.

Mtaalamu huyo anaeleza kwamba watumiaji wa dawa za kulevya wanachangia kueneza Virusi Vya Ukimwi (UKIMWI).

Ni kutokana na kupokezana vifaa vya kujidunga mfano sindano, anayetumia dawa akili yake inakuwa haipo sawa sawa, hivyo hata umakini wa kufanya mapenzi unakuwa mdogo bila kutumia kinga. Kwa kufanya, ngono zembe husababisha kusambaa virusi vya homa ya ini aina ya ‘hepatitis’ B na C inayoambukizwa kama UKIMWI kwa njia ya kujamiiana, kugusa majimaji za mwili na kujichoma sindano kama hizo.

Anaeleza kuwa watumiaji wa dawa za kulevya wanaathirika na magonjwa ya mapafu kama vile Kifua Kikuu (TB) kutokana na wengi kujificha sehemu zenye hewa kidogo, hivyo moshi wanaovuta unawaletea madhara ya magonjwa kama TB, lakini wakati mwingine watumiaji hao wanabadilishana sigara na kuambukiza maradhi yanayoshambulia kinywa na mapafu.

Dk. Nyandindi anasema: “Takwimu za mwaka jana zinaonyesha kuwa kila Watanzania 1,000 mmoja au wawili wana TB , lakini takwimu zetu katika kliniki za waathirika za dawa za kulevya zinaonyesha kuwa kwenye kila watu 1,000 wanaojidunga 65 hadi 110 wana TB.”

Anaeleza kuwa magonjwa ya akili yapo kwa kiasi kikubwa kwa waathirika wa dawa za kulevya na takwimu zinaonyesha kuwa wanaokuja kutibiwa kutokana na matumizi hayo karibu asilimia 30 hadi 35 wanakuwa na tatizo la akili.

“Mfano mtu anayetumia bangi mwanzoni anakuwa na akili nzuri, lakini baada ya matumizi ya muda mrefu anaanza kuwa kichaa. Dk. Nyandindi anasema na kuongeza kuwa watumiaji wa dawa za kulevya wanakumbwa na maradhi ya ngozi kwa sababu hawaogi wala kubadilisha mavazi.

Anabainisha kuwa magonjwa ya kinywa yanawakumba pia hususani ni wa mirungi kutokana na namna wanavyoijaza midomoni, wengi hawapigi mswaki na kwamba idadi kubwa wanakumbwa na vifo vya ghafla kutokana na namna wanavyochanganya dawa hizo.

 MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

“Magonjwa yasiyoambukiza ya ini, figo na moyo yameongezeka mno, idadi kubwa ni watumiaji wa dawa za kulevya kwa sababu dawa wanazozitumia zinakwenda kufanya kazi kwenye ini, figo na moyo. Uchakataji wake unategemea ini, figo …” anasema Dk. Nyandindi na kuongeza:

 “Mfano mtu akitumia cocaine, inachakatwa kwenye ini, utoaji wa uchafu unafanyika kwenye figo, madhara yake yanasukumwa na damu kazi inayofanyika kwenye moyo. Hata bangi hutolewa kwa njia ya mkojo na yote hufanyika kwenye figo,” anaeleza Dk. Nyandindi.

 ATHARI KIUCHUMI/KIJAMII

Kamishna Msaidizi wa Kinga na Tiba, anaeleza kuwa watumiaji wa dawa za kulevya wanaleta athari kiuchumi, kwa mfano, mtu wa kawaida anataka kununua nyumba kwa kiasi fulani cha fedha ambacho wameshakubaliana na muuzaji, lakini anatokea mfanyabiashara dawa za kulevya  kwa vile ana fedha nyingi anatoa kiasi kikubwa na kumzidi mnunuzi wa kwanza na kusababisha umaskini na hali duni kwa watu wenye kipato halali japo kidogo.

Akizungumzia athari kwenye jamii anasema familia nyingi zinasambaratika, kwa sababu mama asiyetumia dawa za kulevya hawezi kuishi na mwenza anayetumia mihadarati, hivyo ugomvi kati yao hauishi. Baba anampiga mama matokeo yake yanaweza kuwa vifo, kuachana, watoto wanasambaratika, yatima na wategemezi wanaongezeka.

Anasema endapo mama anayetumia dawa za kulevya akipata ujauzito, akijifungua watoto wanakuwa na upungufu, lakini maadili katika jamii yanapungua kutokana na matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vya uhalifu kama wizi, uporaji, ujambazi na utoro shuleni vinaongezeka.

 KIDIPLOMASIA/MAZINGIRA

Akizungumzia taswira ya nchi kimataifa Dk. Nyandindi anasema idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya ikiwa kubwa inachafua sura ya nchi kimataifa na kwamba raia wa nchi hiyo wanaposafiri kwenda taifa fulani, wakifika uwanja wa ndege wanadhaniwa wamebeba dawa za kulevya, wanapekuliwa sana kuliko abiria wengine, anasema Dk. Nyandindi.
 
Na kwa upande wa mazingira anasema matumizi ya dawa za kulevya yanaleta athari kimazingira, akitolea mfano wa namna bangi inavyolimwa sehemu zilizojificha zinasababisha kuharibu mazingira, vyanzo vya maji na uoto wa asili na kwamba wakulima wa mimea inayozalisha dawa za kulevya wanateketeza misitu, wanyama wanakimbia na kusababisha ukame na mmomonyoko wa ardhi.

“Watumiaji wa dawa za kulevya kwa kujidunga wanatupa ovyo sindano na mabomba na vifaa vingine vya kuandaa dawa hizo zikiwamo chupa.”

 UHALIFU, UKOSEFU USALAMA

 Anapozungumzia masuala ya uhalifu, Dk. Nyandindi anasema vijana wengi wanaojiingiza katika vikundi vya kigaidi vya kitaifa na kimataifa wengi wao ni watumiaji wa dawa za kulevya na kwamba hakuna mtu mwenye akili timamu anayejiingiza katika vikundi hivyo bila kutumia vichocheo kama dawa hivyo.

 Dk. Nyandindi anasema: “Kuna utafiti umewahi kufanyika unaoeleza kwamba vijana wa kikundi cha kigaidi cha Bokoharamu cha Nigeria asilimia 65 wanatumia dawa za kulevya”.

 UDHIBITI MAJUKUMU YA MAMLAKA

 Dokta Nyandindi anasema Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ina majukumu makuu manne yakiwamo kuzuia uingizaji, uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya. Aidha kuhakikisha jamii haiiingia katika matumizi ya dawa za kulevya kwa kupata elimu sahihi.

 Anasema jukumu jingine ni kupambana na kutokomeza madhara yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya, kuimarisha ushirikiano katika mapambano kuanzia ngazi ya kitaifa, kikanda pamoja na kimataifa na kwa kushirikiana na wadau wengine hutoa elimu juu ya madhara ya dawa hizo katika makundi mbalimbali ya kijamii ili isijihusishe na matumizi ya dawa hizo.

Anasema elimu hiyo hutolewa kupitia vyombo vya habari, machapisho, maadhimisho ya kitaifa, semina na makongamano:

“Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2019, mamlaka ilitoa elimu kwenye Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na Dawa za Kulevya Duniani kitaifa. Katika maadhimisho hayo elimu ilitolewa katika maeneo yaliyokithiri kwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya katika Jiji la Tanga, ambako vijana takribani 180 waliopo katika mazingira hatarishi ya kujihusisha na dawa za kulevya walipata elimu na kwa wale waliopata uraibu wa dawa hizo walihamasishwa kujiunga na tiba.”

Habari Kubwa