Jangalu; Mbaya wa Yanga tangu mchezaji hadi kocha

07Feb 2016
Lete Raha
Jangalu; Mbaya wa Yanga tangu mchezaji hadi kocha

KOCHA wa Coastal Union, Ally Jangalu, ndiye mtu anayejua namna ya kuigeuza sumu ya Yanga hadi ikawa maziwa.
Aliikuta Yanga ikiwa katika kiwango cha juu kabisa, ikifunga magoli itakavyo.

Mabingwa watetezi walikuwa hawajapoteza mechi hata moja katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Bara msimu huu, huku wakiwa hawajaruhusu goli hata moja katika mechi saba zilizopita. Ukuta wake ndiyo uliokuwa ukishikilia rekodi ya kuwa ukuta mgumu zaidi katika nusu ya kwanza ya msimu ukiwa umeruhusu magoli matano tu katika mechi 15 za kwanza. Ndiyo timu iliyokuwa ikiongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika ligi huku safu yake ya washambuliaji iliyoundwa na Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma ndiyo iliyokuwa ikiogopwa zaidi. Wawili hao peke yao walikuwa wamefunga jumla ya magoli 23, ambayo timu nzima ya Coastal haijaweza kuyafikia hadi sasa. Ni takwimu ambazo zisingekufanya ufikirie kwamba zingekuja kuvunjwa na Coastal iliyoonekana imepoteza mwelekeo ikiwa imeshinda mechi moja tu kati ya 15 za mzunguko wa kwanza. MJANJA WA YANGA Akiwa na Coastal ambayo katika siku za karibuni imekuwa ikipata matokeo mabaya, Jangalu aliiongoza timu yake kupata ushindi uliomstua kila mmoja wa mabao 2-0 dhidi ya vinara hao wa ligi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumamosi iliyopita. Lakini Jangalu hakuanza leo kuongoza mauaji dhidi ya Yanga. Mwaka 1988 wakati akicheza soka, aliifunga Yanga goli 1-0 na 1989 aliingia akitokea benchi na kuisaidia Coastal kushinda 3-1 dhidi ya Yanga. Anasema akiwa kocha mchezaji wa Coastal 1988 aliifunga Yanga bao katika ushindi wa 3-1 kwenye Uwanja wa Mkwakwani. "Wakati huo nilikuwa msaidizi wa kocha Joel Bendera, ambaye aliiongoza Coastal kwenye michuano ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati," anasema Jangalu ambaye siku chache baadae, akawa mwanafunzi wa Bendera aliyekuwa mkufunzi wake wa kozi ya kwanza ya ukocha kozi ya awali. “Mwaka 1989 pia niliiua Yanga kwenye mechi ya ligi ambayo ilichezwa Dar es Salaam. Nilicheza kwa dakika tano tu na kufunga goli moja kabla ya kuumia. “Nakumbuka niliingia katika mechi dhidi ya Yanga nikitokea benchi huku zikiwa zimebaki dakika 10 mchezo kumalizika. Nilicheza kwa kasi ya ajabu na kufunga goli, lakini ndani ya dakika 5 tu nikabanwa na msuli na hivyo nikatolewa.” SOKA LA SASA vs LA ZAMANI Kocha huyo anasema, “Soka la zamani lilikuwa ni soka la bure bure, nikimaanisha tulipambana bila kutegemea kulipwa. Wachezaji wengi kwa wakati huo walikuwa wana vipaji vikubwa tofauti na wachezaji wa kizazi hiki cha sasa. “Wengi wa sasa hawajitambui, wanaona soka ni kitu cha mchezomchezo. Mfano unaweza kushangaa kumwona mchezaji ametoka kwenye mechi ambayo wamepoteza, lakini utashangaa hana wasiwasi anaenda kubadili nguo na kwenda disko kufurahia.” Anasema kizazi cha zamani kilikuwa na wachezaji wengi nyota na wenye uwezo wa kweli na kwenye timu moja ungeweza kukuta wachezaji zaidi ya 10 wenye vipaji vikubwa sana, lakini leo hii kwenye timu moja, unaweza kuambiwa kuwa kuna staa fulani, lakini unapoenda unakuta ni mchezaji wa kawaida sana. “Kwa kizazi cha sasa ninafarijika na Mbwana Samatta tu, wengine wanatakiwa kumuiga.” UKOCHA COASTAL Jangalu amewahi kuifundisha Coastal katika mihula miwili tofauti huko nyuma kabla ya hivi sasa. Aliwahi kufanya kazi na Bendera, na miaka ya hivi karibuni alipewa timu hiyo akiwa na kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na Bahati Mgunda. MIGOGORO COASTAL Anasema, “Migogoro Coastal iachiwe viongozi huku kila mtu akiwajibika kwa nafasi aliyopo. Kama ni mchezaji acheze mpira na aache kujihusisha na migogoro kwani kwa kiasi kikubwa inachangia kwenye kuua kiwango." MALENGO YAKE Kocha huyo anasema, “Mimi kama kocha ningependa kujiendeleza na kuongeza kiwango kutoka leseni C hadi leseni B. Kimsingi nataka kuwa mwalimu bora kwani fursa ya kuwa hivyo ninayo. “Unajua zamani tulishindwa kusoma kwa kuwa Chama cha Soka (FAT) wakati huo kilikuwa kikichagua watu wa kusoma kozi za ukocha jambo ambalo lilikuwa likitupoteza wengine ambao tulikuwa na nia. Sasa hivi mambo ni mepesi, mtu yeyote anaweza kusomea, kinachohitajika ni fedha tu. MUUAJI MPYA YANGA Jangalu anasema, “Kuna wachezaji wengi Ligi Kuu lakini mimi namkubali zaidi beki wangu, Miraji Adam, kutokana na umahiri wake wa kusakata soka. “Anajifunza na kuelewa mambo haraka. Pia ni mwepesi na mwenye uwezo wa kupambana na mastraika wakali na wenye nguvu. “Ni fundi wa kupiga 'fri-kiki'. Kwenye mchezo wetu na African Sport alifunga kwa mpira wa adhabu kutokea umbali wa mita 18. Kwenye mchezo dhidi ya Yanga, Miraji alipiga pia 'fri-kiki' ya umbali wa mita 25 na kuwafunga (Jumamosi iliyopita) na hii ni kutokana na jinsi anavyojitunza na kupambana.”

Habari Kubwa