Japo corona ni balaa kwa wengine yawaletea neema

27Aug 2021
Jenifer Gilla
Dar es Salaam
Nipashe
Japo corona ni balaa kwa wengine yawaletea neema

AKIELEKEA kumaliza kuvuna mahindi katika shamba lake lililopo kilomita tano kutoka nyumbani kwake, Toba Athumani (60) haamini anachokiona. Anahakikisha kwa kuangalia mashamba ya majirani, kujiridhisha iwapo macho yake hayadanganyi.

Mahindi ya njano ni nafaka yenye kiwango kikubwa cha wanga na virutubisho ikilinganishwa na meupe. Jamii hii hulimwa kwa wingi maeneo ya Korogwe mkoani Tanga. PICHA: MTANDAO

Mkazi huyo wa Kijiji cha Kwakombo katika Halmashauri ya Mji Korogwe, mkoani Tanga anafurahishwa na wingi wa mavuno ni mara mbili ya mwaka jana, kwa kiasi kile kile cha mifuko nane ya mbegu ya mahindi kwenye heka moja.

"Miaka ya nyuma nilikuwa nikivuna magunia 35 ya mahindi kwa heka tano, wastani wa magunia saba kwa heka, mwaka huu nimepata magunia 75 kila heka moja nimevuna magunia 15, zamani nilikuwa nasomba mara mbili nikitumia trekta safari ni mara nne," anasema na kutabasamu.

Mkulima huyu mwenye familia ya mke na watoto wawili, anaona mfumo wa maisha yake ukibadilika kutokana na mazao mengi na kujihakikishia kipato kuongezeka mara mbili zaidi na kujiweka katika hali salama ya uhaba wa chakula.

"Mauzo yakienda vizuri ninategemea kupata takriban Sh. 3,000,000. Iwapo nitauza kila gunia kwa Sh.40,000, hela ninayoitumia kuihudumia familia yangu ikiwa ni pamoja na kulipa ada za watoto, tofauti na mwaka jana ambapo niliambulia Sh.1, 200, 000 kwenye magunia 30, "anasema Toba.

Siri ya matumaini mapya ya kilimo kwa Athumani ni matumizi ya mbegu za kisasa zinazohimili athari za mabadiliko ya tabianchi zilizoelekezwa kwa wanakijiji wa Kwakombo.

HALI ILIVYOKUWA

Rashidi Salim (55), ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwakombo chenye wakazi 1,700, ambao asilimia 90 wanalima mahindi kujikwamua kiuchumi, anakiri kuwa kilimo cha mahindi kilidorora.

“Kilimo cha mahindi kilikuwa kinakataa, hadi kufikia baadhi ya wakulima wakaacha, tukatoa taarifa kwa maofisa kilimo kwa sababu tuliona kijiji kinaelekea kupata njaa, tunashukuru Mungu mwaka huu wametutembelea kutuelekeza kuhusu mbegu za kisasa.

“Ofisa kilimo alituletea kilo 300 za mbegu ya DK 8031 na DK 9089, tukawapatia wakulima 75 wenye mashamba wanaolima kitaalamu tukampa kila mmoja mifuko minne inayotosha nusu heka. Kisha tukawaelekeza zinakopatikana ili wakanunue, walipanda mwezi Machi, mwaka huu na ndiyo wanavuna sasa", anasema Salim.

Mnufaika mwingine wa mbegu hizo, Athumani Ally anasema heka moja aliyoipanda mbegu ya DK 8031 ameona tofauti kubwa katika mavuno.

"Nilipewa mifuko minne nikaongeza nyingine ya ‘Tumbili nikachanganya nikapanda heka moja, nimevuna magunia 14 tofauti na mwaka jana nilipata matatu ambayo hayakutosha kwa chakula na kuuza,” anasema Ally.

KUKABILI COVID-19

Mbegu hizo za majaribio, ni msaada kutoka kampuni za Agricultural Council of Tanzania (ACT) na Dayer, uliolenga kuwasaidia wanakijiji kupambana na njaa katika kipindi cha janga la COVID-19 ukijulikana kama Covid Donation 2020.

Mkuu wa Idara ya Kilimo na Umwagiliaji Halmashauri ya Mji Korogwe, Ramadhani Sekija, anasema mradi huo ulilenga kusaidia Wilaya za Korogwe mjini na vijijini, ili kuongeza chakula kwa wananchi.

“Tulipokea mbegu tani 10, na kuzigawia Korogwe mjini na vijijini kila eneo tani tano na jumla ya wakulima 1,197 wa vijiji saba na mitaa 22 wamenufaika, huku taasisi 10 na maofisa ugani 33 pia walipata mbegu hizo” anasema Sekija.

Utambulisho wa mbegu hizo ulienda sambamba na elimu inayohusu umuhimu wa kutumia mbegu hizo, kwa mujibu wa Ofisa kilimo wa Kata ya Kwamsisi, Said Sharif, wanavijiji walielimishwa kuhusu changamoto iliyopo katika kilimo kwa sasa na umuhimu wa kuhamia kwenye mbegu za kisasa zinazohimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

"Walieleza kuwa moja ya mbinu itakayowatoa kutoka kwenye athari za mabadiliko ya tabianchi kwenye kilimo ni kutumia mbegu za kisasa. Tunashukuru wameelewa na mwamko wa kutumia mbegu za kisasa ni mkubwa " anasema Sharif.

WAKULIMA WAHAMASIKA

Elimu kuhusu matumizi ya mbegu za kisasa imetoa hamasa kwa baadhi ya wakulima waliokuwa wamekata tamaa na kushawishika kurudi tena katika mstari wa kilimo cha biashara kama anavyoelezea Fatuma  Mgolo (60).

“Nilishakata tamaa, walivyokuja kutuelimisha nikasema ngoja nijaribu, nikaenda kununua dukani nikalima heka yangu moja, aisee mazao ni mengi japo mvua zimekataa, msimu ujao nalima kibiashara kama zamani",  anasema
Fatuma.

MATATIZO YALIYOIBUKA

Ingawa mbegu hiyo aina ya DK 8031 inatoa mavuno mengi inalalamikiwa kushambuliwa na wadudu hasa vidudumuzi na viwavijeshi, anasema Toba Athumani.

“Tunaiomba serikali itusaidie viuatilifu kupambana na wadudu hawa wanaoharibu mazao, mhindi unaliwa na kubakia unga,”anaongeza.

UHAKIKA WA CHAKULA

Dokta Honest Kessy ni Mkurugenzi wa  Idara ya Usalama wa Chakula Wizara ya Kilimo, anayeihakikishia nchi kuwa ipo salama katika upatikanaji wa chakula na viini lishe lakini, anaonya haipaswi kuridhika na hali hiyo.

"Mfumo wetu wa uzalishaji upo vizuri,  mwaka jana tulikuwa na tani milioni 18.2,  mwaka huu tunapambana zaidi kwa kuhakikisha tunadhibiti visumbufu vya kilimo na kuhimiza kilimo cha kisasa kinachohimili mabadiliko ya tabianchi,  ili tuzalishe zaidi kipindi hiki cha corona, hata tukisema tujiweke ‘lockdowns’ tusiwe na shida ya chakula.

"Pia tunafanyia kazi upatikanaji masoko nje ya nchi, ili wakulima wetu wanufaike na wenzetu wawe na uhakika wa chakula hasa katika kipindi hiki. Mfano ule mgogoro wa Kenya kukataa mahindi ya Tanzania kuwa yana sumu kuvu tumeumaliza na wakulima wanaendelea na biashara, "anasema Dk. Kessy.
 
Anataja matatizo ya kilimo kuwa ni pamoja na ukame, maeneo mengi kukosa mvua za kutosha mfano mikoa ya Tanga, Arusha na Kilimanjaro.

Anataja ardhi kukosa rutuba na kuchoka baada ya kutumika muda mrefu na kuingia tindikali inayosababisha mimea kutofyonza mbolea.

MBINU ZA UFUMBUZI

Dokta Kessy anasema Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), imepata suluhusho la kuondoa tindikali kwenye udongo kwa kutumia chokaa inayomwagwa kwenye udongo kupunguza tindikali.

Baadhi ya maeneo yaliyofikiwa na chokaa hiyo ni Mbeya na Songwe ambapo wakulima wameitumia msimu huu wa masika na wamepata matokeo mazuri, anaongeza Kessy.

Ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) ya Matarajio ya Mazao na Hali ya Chakula (2020),inaeleza kuwa mataifa 32 kati ya 44 yanahitaji msaada wa chakula na nchi hizo ziko Kusini ya Jangwa Sahara, ikiwamo Tanzania.

Inafafanua kuwa ukame, mafuriko na majanga mengine yanaweza kuongeza upungufu wa chakula na kukwamisha kufikia lengo namba mbili la Maendeleo Endelevu (SDG 2) la kupunguza udumavu wa watoto kwa asilimia 50 ifikapo 2030.

Ripoti ya Shirika la Chakula Duniani juu ya Usalama wa Chakula, kipindi cha corona inaonyesha kuwa Tanzania ambayo ina idadi ya watu milioni 58, milioni 15 ni maskini.

Inaongeza kuwa watu 5,000,000 wanaishi chini ya mstari wa uhaba wa chakula kati yao milioni mbili wako mijini na kwamba kupungua kwa shughuli za uchumi na kijamii kutokana likizo ya COVID-19 , kutaathiri mapato na usalama wa chakula katika maeneo ya mijini.