Je, kushinda njaa njia sahihi ya kiafya kupunguza mwili?

15Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Je, kushinda njaa njia sahihi ya kiafya kupunguza mwili?

WATAALAMU wanasema, kujinyima chakula husababisha udumavu wa mwili.

Mpangilio sahihi wa chakula husaidia mwili kujitibu.PICHA: MTANDAO

Kuna njia nyingi za kupunguza mwili ambazo hutangazwa kwenye televisheni na mitandao ya kijamii.

Lakini njia salama na inayopigiwa chapuo na wataalamu wa afya, ni kufanya mazoezi ya viungo na kubadili mfumo wa ulaji kwa kuanza na mlo sahihi.

Katika kubadili mpangilio wa kula kuna mambo mengi, kwa kuwa kuna elimu mbalimbali zisizo rasmi zinazotolewa katika mitandao juu ya kupangilia mlo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mitandao mtu anaweza kupungua haraka endapo atafuata mlo anaoelekezwa.

Kuna mpangilio wa chakula wa siku saba, siku 10 mpaka siku 21. Na mtu anaweza kupungua kuanzia kilo tatu mpaka 15, inategemea kama atafuata kwa umakini maelekezo.

Supu ya kabeji, mlo wa kijeshi ama kwa kingereza ‘Military Diet,’ na mlo wa yai ama ‘Egg diet’ ni baadhi tu ya njia za haraka za mpangilio wa chakula au diet, ili kupunguza unene kwa haraka zaidi.

JE, WALIOFUATA MAELEKEZO WAMESAIDIWA?

BBC inaangazia safari ya kupunguza uzito ya Linda, mama wa mtoto mmoja na muuguzi nchini Tanzania. Anasema huwa anapungua na kuongezeka.

“Nina mwili mkubwa sana na siufurahii hata kidogo… natamani sana nipungue… nimejaribu hizi diet za kupungua haraka kwa miaka kama minne sasa sema ndio hivyo, napungua halafu nanenepa tena,” anasema na kuongeza:

“Mfano mwezi wa tisa mwaka jana, nilikuwa na shughuli ya kupunguza mwili wangu, yaani nilikuwa nakula mlo mmoja tu… sema nilipoacha nikaongezeka sana hadi aibu.”

Hata hivyo, mama huyu anaamini kuwa mwili wake ni wa kurithi kwa kuwa ndugu zake wengi ni wanene, hivyo kupungua kwake si kazi rahisi.

“Mie mwili wangu hauwezi kupungua kirahisi maana wazazi wangu pia ni wanene sana na mimi mwenyewe naelewa hilo, kwa sababu nishafanya sana hizi diet na ndio kwanza nimeambulia vidonda vya tumbo,” anasema na kuongeza:

“Hivyo, naamini ni mambo ya kijenetiki, nitapungua tu wakati ukifika.”

JE, NJIA HIZI NI SALAMA?

BBC imezungumza na daktari wa magonjwa ya binadamu aliyejikita kwenye magonjwa ya lishe na mwandishi wa vitabu vya afya ya jamii maarufu kama sayansi ya mapishi nchini Tanzania, Dk. Boaz Mkumbo.

Dk. Mkumbo anabainisha kuwa kutojua njia sahihi kunawafanya wengi kuangukia katika njia ya kujinyima kula, kitu ambacho ni hatari kwa afya.

“Kujinyima kula ili kupunguza uzito si njia endelevu… huwezi kujinyima milele,” anasema Dk. Mkumbo na kuongeza:

“Si watu wote wanaweza kujinyima chakula… daktari anaweza kumzuia mtu kula lakini hawezi kuizuia njaa…njaa si tendo la hiari, hivyo kujinyima sana huleta udumavu wa mwili… mtu unachakaa kwa sababu ya kukosa viini lishe.”

MADHARA YA KUJINYIMA KULA

Kimsingi, kukosa viinilishe katika mwili, husababisha udumavu na uchakavu wa mwili, yaani nuru kupotea, kisha kuwa kama mgonjwa.

Aidha, si watu wote wanaweza kujinyima kula kwa sababu huwezi kuizuia njaa.

Kuna uwezekano wa kukabiliwa na hatari ya kushuka kwa sukari ghafla au presha ikashuka ghafla, kwa sababu ya kukosa viinilishe muhimu.

Vilevile, si watu wote wanaweza kudhibiti uzito, ubaki palepale hata baada ya kupungua kwa kuwa si njia endelevu… huwezi kujinyima maisha.

Hata hivyo, Dk. Mkumbo amepinga vikali tabia ya watu kujinyima kula kwa sababu haina matokeo ya kudumu, sababu unapoacha kujinyima mwili utaongezeka.

“Kujinyima kula ili kupunguza uzito si njia endelevu… huwezi kujinyima milele. Njia nzuri ya kupungua uzito ni kuzingatia ubora wa chakula,” anasema.

Anabainisha kwamba katika sayansi ya mapishi kila chakula ambacho kinaingia mwilini, kina mwitikio tofauti.

“Mwili ukiupa sukari na vyakula vya wanga unamimina homoni nyingi za kunenepesha…lakini nikikupa mayai, samaki, parachichi na baadhi ya matunda ambayo yana sukari kidogo kama matango, mwili utaitikia,” anasema na kuongeza:

“Mwili utaitika kwa kumwaga homoni ya kunenepesha kwa kiwango kidogo sana…utapata virutubisho vyote na mwili hautafubaa wala kusinyaa.”

KITAMBI

Hata hivyo, Dk. Mkumbo anaenda mbali zaidi na kufafanua kuwa mtu kuwa na tumbo kubwa ama kitambi si ulafi.

“Kitambi hakisababishwi na ulafi wala uvivu, ukimwambia mtu ni ulafi atajinyima kula… ukisema uvivu atafanya mazoezi lakini hatoangalia ubora wa anachokula,” anasema.

Anabainisha kuwa siku hizi anashangaa kukuta mtu ametoka sehemu za mazoezi na kuanza kunywa soda bila ya kujua kuwa mwili wake unaenda kumwaga homoni nyingi za kunenepesha.

“Kitambi husababishwa na homoni… ili kudhibiti kitambi na mlipuko mkubwa wa magonjwa ya lishe, lazima tuzingatie ubora wa chakula ili tuweze kufikia malengo yetu ya afya na kuepuka homoni za unene kumwagika,” anasema.

Hata hivyo, daktari huyo anafafanua kuwa vyakula vya wanga, juisi za viwandani na soda ni baadhi tu ya vyakula ambavyo husababisha kumwagika kwa homoni za unene kwa wingi.

BBC