Je tunatambua vipaji vyetu na vya watoto wetu?-1

14Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Je tunatambua vipaji vyetu na vya watoto wetu?-1

KAMA kuna swali ambalo linahusu maisha binafsi ya mtu na limekuwa na majibu hafifu sana ni swali linalohusu kipaji.

Kuna idadi kubwa sana ya watu wanaomaliza maisha yao hapa duniani bila kufahamu ni aina gani ya kipaji walichonacho.

Wengine hata hawaamini kuwa wanaweza kuwa na kipaji. Kwa sababu hiyo wamefikiri kuwa kipaji ni kwa baadhi ya watu tu na swala hili haliwahusu wazazi na hata watoto wetu. Fikra hizo sio za kweli hata kidogo na ningependa nikueleze wazi kuwa hata wewe una kipaji cha pekee sana. Nasisitiza tena kuwa hata wewe una kipaji, ila hujakitambua na hujakitumia.

Kupitia  makala hii ndiyo itakuwa nafasi yako ya kuanza kufaidi matunda ya kipaji chako.

Acha kujivunja moyo kuwa umri wako umepita na huhitaji tena kusikia habari ya kipaji au habari ya kipaji ni kwa ajili ya watoto wadogo tuu.

Makala hii itakupa mwongozo wa kubadili mwelekeo wako katika kutumia kipaji chako bila kuathiri maisha yako.

MAANA YA KIPAJI
Neno kipaji sio neno geni masikioni kwetu hasa sisi tuliozaliwa katika miaka ya hivi karibuni. Limezoeleka sana kutokana na kuzungumzwa sana katika maeneo mbalimbali siku hizi.

Cha kusikitisha ni kuwa, Jinsi kipaji kinavyotamkwa ni tofauti kabisa na kinavyotumika. Kwa usemi mwingine naweza kusema kuwa kipaji kinatamkwa sana kuliko kinavyotumika.

Swala hili linafanya maana ya kipaji kupotea na hivyo jamii kuishi bila kutumia nyenzo hii muhimu ya asili.

Bila kujali ni kipaji cha aina gani. Kipaji ni uwezo au nguvu za asili anazokuwa nazo binadamu katika kutenda jambo Fulani kipekee bila kujali kiwango cha ujuzi alionao.

Uwezo huu unaweza kujitokeza katika kufikiri, kutamka, kutenda, kuhisi nk.

Kipaji si ile shughuli tuifanyayo bali ni ule uwezo wa asili tunaozaliwa nao na kujijenga ndani yetu kuwezesha kufanya aina fulani ya shughuli au kitendo kwa namna ya upekee sana kuliko watu wengine.

Uwezo huu huwa ndiyo mfumo asilia ndani ya vinasaba vya mtu ambao hauwezi kubadilishwa kwa kuzoelea kufanya mambo fulani fulani yasiyoendana nao.

Kwa mimi ninayeamini uwepo wa Mungu nasema hii ni zawadi ya pekee kwa kila binadamu kutoka kwa Mungu na kila mtu amejaliwa kwa namna yake ili sote tufaidiane.

DALILI ZA KUANZA KUONEKANA KWA KIPAJI

Mara nyingi vipaji vingi ambavyo ndiyo uwezo uliomo ndani yetu kuwezesha kufanya mambo kadhaa kiupekee, huanza kugundulika wakati muda umeshapita sana.

Sababu kubwa ya kutogundulika haraka kwa vipaji hivi (uwezo), ni kutokana na kipaji kujitokeza kwa namna ya mficho.

Hujitokeza kwa mfano wa faili lililofungwa na kuandikwa kwa nje  uwezo wa michezo, taaluma, ubunifu, au uimbaji bila kufafanua ni uwezo wa mchezo upi hasa au taaluma ipi au ubunifu wa nini au uimbaji wa aina gani.

Lakini kwa bahati mbaya ufafanuzi huo ni mpaka ufungue ndani. Kwa sababu hiyo hata wengi wa wanavipaji huishia kutumikia anwani za mafaili hayo mpaka wanakufa. 

Wanatumikia michezo wasijue uwezo wao ni juu ya mchezo gani hasa, wengine taaluma wasijue ni taaluma gani na wengine uimbaji wasijue uimbaji wa aina gani.

Kitu ninachoomba ukitambue ni kwamba kipaji huanza kwa namna ya wazo. Wazo hili huwa halisomeki sawa sawa kama ilivyo kwa faili lisilo na ufafanuzi. Nalo hukua taratibu kwa kadri mtu huyu anavyochukua hatua au kulifanyia kazi.

Kwa maana nyingine ningesema kulifanyia mazoezi. Mfano; kama wazo likiwa ni uwezo wa kitaaluma basi haliwezi kujitokeza na kujiweka wazi mpaka utakapochukua hatua ya kusomea au kufanya kazi katika taaluma hizo ambazo ule uwezo wako wa asili (kipaji) unajipambanua.

Kupitia shuleni huwa ni rahisi kiasi kwa sababu watoto hupewa uwanja mpana kidogo wa kujaribu kuonyesha japo vipaji vichache, haswa vya kitaaluma chini ya uangalizi fulani.

Lakini cha kusikitisha ni kwamba hata mashuleni bado  nafasi hiyo ni finyu sana kuonyesha na kukuza vipaji vyote vilivyopo duniani.

Vinavyokosa nafasi hiyo ni vile ambavyo viko nje ya mitaala kutokana na kutovitilia maanani hivyo kutengwa na mfumo wa elimu.

Katika maeneo maalumu ya kukuzia vipaji imekua rahisi kuvigundua. Kwa sababu watoto au wanafunzi hupewa nafasi ya kuonyesha wanachokiweza na kisha kuwaweka katika makundi maalumu.

Ni wajibu wetu kuendelea kuanzisha vituo hivi na kuwatia moyo wanaofanya hivyo. Lakini tufikirie kuanzisha vituo vitakavyoshughulika na aina nyingi za vipaji na sio aina moja tu ya kipaji kama ilivyo sasa. Kwa kuwa vituo vingi vinaendeleza vipaji vinavyoendana na michezo.

NANI ANA KIPAJI?

Ukweli ni kwamba kila mtu ana kipaji cha peke yake  ambacho kinamtambulisha yeye na kumfanya awe na mchango tofauti na mtu mwingine yeyote duniani.

Kosa kubwa tunalolifanya ni kwamba wengi tunaishi kwa kufuatana kuigiza vipaji vya watu wengine. Inawezekana ikawa ni wewe na pengine umefanya hivyo bila kufahamu.

Kwa maana nyingine ni kwamba watu wengi wanaishi kwa kutumia uwezo ambao haumo ndani yao.

Wanafanya shughuli ambazo haziendani na mfumo halisi uliojengwa  ndani yao.Wanaenda kinyume kabisa na namna mfumo wa  ubongo wao, ufahamu wao, na miili yao ilivyosukwa.

ITAENDELEA
Mwandishi ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Majengo- Moshi, Kilimanjaro. Anapatikana kwa simu namba 0674-513851, [email protected]