Je, unapolala Panakuvutia?

23Mar 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Je, unapolala Panakuvutia?

CHUMBA cha kulala katika nyumba ni miongoni mwa vitu muhimu kwa ustawi wa maisha ya binadamu.

Hili ni eneo muhimu ambalo linaweza kuweka akili sawa za binadamu na ikamsaidia kuendesha shughuli zake kwa ufasaha zaidi.

Kutokana na umuhimu wa chumba hiki katika maisha ya binadamu, kuna haja ya kupewa kipaumbele zaidi tofauti na ilivyo kwa vyumba vinginevyo, kwa kuhakikisha kwamba kinakuwa na vitu vya muhimu ambavyo kwa namna moja ama nyingine vinaweza kuimarisha utulivu wa akili.

Inafahamika kwamba chumba kilichokamilika lazima kiwe na sehemu ya ukuta, mlango, dari na dirisha lakini mbali na hivyo, vipo vitu vingine ambavyo vinaweza kukikamilisha zaidi.

Makala hii inaangalia vitu muhimu vinavyohitajika ndani ya chumba hicho cha kulala ambavyo vitakifanya kionekane kwamba kimekamilika.

Chumba ambacho kwa lugha yako mwenyewe unaweza kukipa heshima ya kipekee unayoona inafaa kwako. Ni vema kujenga taswira yako kichwani kwanza juu ya aina na namna unavyohitaji kiwe hata kabla ya kufanya uamuzi wowote ule.

Jambo la kwanza ambalo linapaswa kuzingatiwa katika chumba cha kulala ni kitanda na godoro.

Hili ni eneo muhimu kwa kuwa kabla ya kufanya uamuzi wa kununua na kuweka katika chumba unapaswa kutulia na kutafakari ni aina gani au muundo gani unahitaji kadri ulivyopangilia kukitengeneza.

Hakikisha haufanyi makosa katika kipengele hiki cha uchaguzi wa kitanda na gorodo.

Jambo la pili ambalo unapaswa kufanya ni uchaguzi wa aina ya mashuka na mito inayoendana na aina au muundo wa kitanda husika, fanya haya yote kwa kuzingatia picha au taswira ya aina ya chumba unachohitaji kutengeneza.

Si jambo baya kuwa na mito kuanzia miwili hadi sita au zaidi ya hiyo kulingana na ukubwa wa kitanda lengo ni kuigawanya kupata ya kutumia wakati wa kulala pamoja ya mapambo.

Zulia nalo katika chumba huongeza mvuto kwa kiwango kikubwa, hivyo katika muundo wako wa chumba unaweza kuangalia namna ya kuliwekea bajeti.

Kumbuka kwamba hakuna sakafu inayoweza kuburudisha miguu peku unapotoka kuamka asubuhi kuliko ya zulia, si vibaya kama hili nalo likazingatiwa na ili kutengeneza hatua ya mwanzo wa siku kuwa ya burudani.

Hata kama huwezi kununua zulia la kutosha chumba kizima, lakini unaweza kuweka hata nusu yake pembezoni mwa kitanda.

Jambo jingine ambalo linafaa kwenye chumba hiki cha kulala ni sehemu ya kuketi ambalo linaweza kusaidia kulitumia kuketi na kusoma kitabu au mazungumzo kabla ya kulala kitandani.

Eneo hilo linaweza kutumika pia kunyanyulia miguu wakati wa kuvaa soksi au nguo pamoja na kuwekea mapambo yanayotumika kupambia kitanda wakati wa usiku yanapotanduliwa badala ya kuweka chini.

Sanaa na picha katika chumba nayo ni muhimu japokuwa unatakiwa kuhakikisha unaweka zile muhimu na zinazokuvutia na kuepuka kuwa na mrundikano wa picha hizo.

Ni vizuri kukumbuka kwamba vitu vichache unavyovipenda eneo unaloviona kwa muda mrefu husaidia kuongeza furaha na utulivu wa akili na hata kupata usingizi mwororo.

Na kwa wale wanaopendelea kuamka usiku na kusoma neno la Mungu, si vibaya kuweka pembeni ya kitanda kunakoelekezwa kichwa, taa hafifu ambazo haziwezi kumsumbua mwingine hasa wenye wenza wao.

Taa hizi pia hutumika kama mapambo ya kupendezesha chumba kumbuka ili kikamilike, pia kinatakiwa kiwe na mapazia.

Ni muhimu kukumbuka kwamba chumba cha kulala kinahitaji kiwe cha faragha, kwa hiyo kinahitaji kuwekwa pazia sahihi kulingana na uhitaji wa kifaragha.

Habari Kubwa