Jeuri kiitikadi ‘sumu’ Bunge kusimamia mikataba

16Jul 2017
Ibrahim Mkamba
Nipashe Jumapili
Jeuri kiitikadi ‘sumu’ Bunge kusimamia mikataba

HIVI karibuni imepitishwa sheria ambayo, pamoja na mambo mengine, bunge limepewa nguvu kupitia mikataba ya kimataifa kuhusu rasilimali za taifa yakiwamo madini.

Nionavyo, ni hatari mikataba hiyo kupitia bungeni. Kwa sababu uhasama wa wabunge wanaoabudu itikadi za chama tawala dhidi ya upinzani unaweza kuitumbukiza nchi pabaya.

Inaweza kutokea vipengele hatari visivyotetea maslahi ya taifa vikapitishwa ili "kuwashinda waliotaka kuvikwamisha” hata kama havina tija kwa taifa! Baada ya hapo hasara ikawa kubwa kutokana na watunga sheria hao kupitia mikataba hiyo. Hakutakuwa na mamlaka ya kuhoji kwani bunge ambalo lingehoji na kukosoa nalo linakuwa sehemu ya uandishi wa mikataba hiyo.

Kwa bahati mbaya bunge si la nchi bali la vyama vya siasa. Kwenye kupitisha sheria mpya hivi karibuni, inaelezwa wakati wabunge wa upinzani wakitoa mapendekezo mengi ya maandishi ya marekebisho, wabunge wa CCM hawakupeleka hata rekebisho moja kutoka kwa wapinzani! Kimsingi, walijilazimisha kuona kila kitu kuwa sahihi kwa sababu tu kilitoka kwa serikali hata kama kilistahili marekebisho hii ndiyo demokrasia, ndiyo maslahi ya taifa!

Katika mazingira hayo, kukwama au kupitishwa kwa mikataba na bunge kutategemea wabunge wa CCM, ambao ni wengi,wameandaliwa vipi na wala siyo ubora wa mikataba hiyo. Hili litafakariwe na sheria husika irekebishwe mapema kwa maslahi ya nchi kwa kuwa kinachotakiwa kifanyike ni kulinda maslahi ya taifa siyo ya chama.

Hebu tukumbuke wale walioshangilia na kucheza kiduku ndani ya ukumbi wa bunge ilipopitishwa katiba inayopendekezwa, walishangilia upitishaji katiba bora au ushindi dhidi ya walioikosoa? Ni wazi shangwe hiyo ilikuwa ya ushindi dhidi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Warioba!

Itakuwaje kama kwenye kikao cha wabunge wa chama tawala ukajengwa msimamo wa kupitisha mkataba kwa sababu yoyote hata ukiwa na dosari? Watakaopinga kwa hoja na utafiti wa nguvu watashindwa tu kwa idadi yao ndogo.

Ukitaka kuiona hatari ya kupitishia mikataba bungeni, rejea hitimisho la mjadala wa mkataba wa Buzwagi mwaka 2007 kadhalika kile kilichojiri ndani ya Bunge Maalum la Katiba mwaka 2015.

Pia rejea wabunge wachache wa upinzani walivyopambana bila mafanikio kuonyesha dosari nyingi na kubwa za Sheria ya Mtandao huku wenzao wa CCM wakiwapinga kwa sababu tu muswada huo umetoka serikalini! Sheria ikapitishwa, ikasainiwa na leo hii hata wana CCM tunalalamikia baadhi ya vifungu vya sheria hiyo!

Hivyo ndivyo itakavyokuwa pale serikali itakapopeleka mikataba ya maliasili za taifa bungeni kujadiliwa. Kwa sababu itapelekwa na serikali inayoongozwa na CCM inaweza ikapitishwa na dosari zake kutokana na wingi wa wabunge wa chama hicho bungeni.

Ukweli ulio wazi ni kwamba kambi ya wabunge wengi ikijenga msimamo jambo liwe wanavyoshawishiwa liwe lazima litakuwa hata likiwa na makosa.

Kwani Sheria ya Madini iliyoipigiwa kelele kwa ubaya na hata sasa imeibua ya makinikia si ilipitishwa huko huko bungeni? Kwanza, kuna uhakika gani kama wabunge wetu wote husoma kifungu kwa kifungu cha sheria wanayotakiwa kuipitisha?

Kwa kuzingatia ukweli huo, bunge lisihusishwe na uandishi wa mikataba ya nchi ili libakishwe kuhoji dosari za kazi za kamati imara na makini zitakazoandika, kutathimi na kupitisha mikataba hiyo.

La msingi ni kuwepo kuchunguzana na kudhibitiana kwa maana ziwepo kamati za hatua tofauti za kutengeneza mikataba yetu.

Ya kwanza ya watu makini tupu ikishaandika, ya pili ya watu makini tupu pia inatathmini kwa kupitia na kuhoji mambo yenye utata na yasiyo na maslahi kwetu kisha inawasilisha mikataba iliyoboreshwa kwa kamati ya watu makini tupu wengine kuipitisha.

Ufuatiliaji wa ufanisi wa timu hizo uwe wa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Kwa utaratibu huo, bunge litabaki nje kuhoji mambo yoyote yatakayoonekana yamekosewa katika mikataba hiyo.

Ikiwa nayo imehusika kuandika mikataba hiyo, kwa njia ya kuipitia, na makosa kuwamo, suala la makosa hayo likijadiliwa bungeni, bunge litajilazimisha kutetea makosa kwani litakuwa limehusika kuyatenda. Hii ndiyo hatari niliyoiona. Mungu Ibariki Tanzania.

Habari Kubwa