JKT Tumaini Lisiloisha

15Feb 2020
Gaudensia Mngumi
Dar es Salaam
Nipashe
JKT Tumaini Lisiloisha
  • *Kumaliza rushwa, kukuza uzalendo kwa vijana

CHANGAMOTO kubwa inayotatiza Tanzania na hata dunia zama hizi ni kukosa watu, waadilifu na waaminifu.

Mawazo ya kuwa na tamaa ya kujitajirisha hata bila kufanyakazi, kuwa tajiri ambaye alilala maskini lakini kwa ulaghai na ujanja ameamka bilionea yanawalazimisha wengi kujiingiza kwenye rushwa, ufisadi na kupoteza uzalendo.

Hata hivyo kama taifa, Tanzania imechukua hatua mbalimbali kuwanusuru vijana ili kupunguza fikira za kujitumbukiza kwenye ufisadi, tamaa za rushwa na pia kuwafanya kuwa wazalendo Zaidi na wachapakazi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, anaeleza mbinu zinazotumiwa kuhakikisha vijana wanafinyangwa katika utaratibu unaowawezesha kuwa waadilifu na wazalendo.Aidha anataja mafanikio, changamoto katika utekelezaji wa masuala ya utawala bora.

Akizungumza na mtandao wa wanahabari wa uandishi wa taarifa za utawala bora jijini Dodoma hivi karibuni Mkuchika , anatoa angalizo kuwa mataifa mengi duniani yaliyofanikiwa kupambana na rushwa juhudi zilifanyika kuwafundisha watoto na vijana wake ubaya wa rushwa kuanzia shule za msingi hadi vyuoni, kuichukia rushwa.

Anasema walifundishwa maadili , kusimamia haki na uzalendo katika ngazi za chini na kwamba mataifa kama nchi za Asia zimefanikiwa na kufika mbali kwenye mapambano dhidi ya rushwa.

Akijibu swali, Tanzania inawaandaaje vijana kwenye masuala ya kuwa raia wema , waadilifu, wanaoheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora, wenye uzalendo na wachapakazi anasema:

“Kama taifa tumekuwa tukiwaandaa vijana kuwa wazalendo, wenye maadili, wafanyakazi na raia bora kupitia mpango wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ulioasisiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere baada ya Uhuru, ambao hata sasa umerejeshwa”.

Analitaja kuwa ndilo eneo Mwalimu Nyerere aliloliachia taifa kwenye kuwaandaa vijana kuwa watu bora wanaoheshimu haki za binadamu, wazalendo, wanaotii mri na maagizo, wenye ujasiri, wachapakazi na viongozi waadilifu.

Mkuchika anasema jitihada za kuwafundisha vijana zinaendelea hata leo kwa kuwaweka wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita katika makambi ya JKT japo ni machache kuliko idadi ya wahitimu wanaomaliza shule leo lakini serikali imeendelea kupanua mafunzo hayo.

“Sserikali ya awamu ya tano imeongeza makambi mengi zaidi . Nia ni kuwafundisha na kuwaandaa vijana kuwa wazalendo, wachapa kazi na viongozi bora. Imeona JKT ni chombo kikubwa na muhimu kiimarishwe ili kupata vijana bora.”.

Anakumbusha kuwa wakiwa JKT vijana wa hali tofauti wanafundishwa kukaa pamoja, kuheshimiana, kutii amri na maelekezo hata kama wanatoka familia za maskini na tajiri wote wanakaa, kula , kulala pamoja. Kuimba nyimbo za kimapinduzi na kuendeleza uzalendo na kutii majukumu wanayopewa.

VITA YA RUSHWA

Waziri akizungumzia mafunzo ya kukataa ufisadi na kuwa wazalendo anasema kwa Tanzania mitaala ya kufundisha shuleni na vyuoni ipo na kinachotakiwa ni kupanga na kuamua masomo gani ya kuingizwa kwenye mitaala hiyo.

“Wizara ya Elimu imeandaa na kutoa utaratibu wa mafunzo ya kupambana na rushwa. Mathalani kuna elimu ya uraia katika shule za msingi , Civics katika shule za sekondari na katika vyuo vikuu kuna kozi ya Development Studies (taaluma za maendeleo).

“Utaratibu wa masomo upo kinachotakiwa ni kuingiza kozi au kuamua ni mambo gani yakufundishwa kwa mfano maadili, uzalendo kuanzia elimu msingi hadi vyuo vya elimu ya juu na kwamba hata vitabu vya kufundishia vipo.” Anasema.

Anaongeza kuwa ili kuwahamasisha vijana kuchukua na kuepuka rushwa shule nyingi zimeanzisha klabu za kupinga rushwa ambazo huzungumzia masuala ya ubaya, udhaifu na fedheha inayotokana na rushwa kwa kushirikisha wanafunzi na wadau ikiwamo Taasisi ya Kuzia na Kupambana Rushwa (Takukuru).

MAFANIKIO UTAWALA BORA.

Waziri anapoulizwa kuhusu mafanikio ya utawala bora anasema ni mengi na yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za mfano barani Afrika kwa kutumia rasilimali kwa ufanisi na kwa tija kwa manufaa ya wote.

Anasema inasimika kwa mfano kutoa huduma za kijamii kuna vituo vipya vya afya vya kutolea huduma vilivyokarabatiwa kuanzia 2017 hadi 2019 vimefikia 487 kutoka 352.

Wakati hospitali mpya zimejengwa na nyingine kukarabatiwa na zahanati zilizokarabatiwa na kujengwa ni zaidi ya 1,000.

Juhudi zimefanywa kujenga miundombinu ikiwamo reli ya kisasa (SGR), kununua ndege za kisasa na kufufua shirika hilo, kujenga mradi wa kufua umeme wa megawati 2,100 kwenye Mto Rufiji yote haya yanaleta sura mpya katika utawala bora na matumizi ya rasilimali za taifa.

KUWEKA WATU NDANI

Waziri Mkuchika anataja kudhibiti vitendo vya wakuu wa Wilaya na Mikoa kuweka watu na watendaji ndani kwa saa 24 kuwa sasa vimedhibitiwa na kwamba ni masuala yanayohusu utawala bora.

Anasema yamefanyika baada ya kuwapa mafunzo ya uongozi wakuu hao na kuwaelekeza kwenye taratibu za kiuongozi.

“Ni lazima mtu yeyote akipewa kazi apate mafunzo awe Waziri, Mkuu wa Mkoa, Wilaya, Wakurugenzi hata polisi nao wamepata mafunzo kuhusu majukumu yao. Ndiyo maana hali imetulia. Maji yametulia mtungini.”

Hata polisi wanaokamatwa nao wamefunzwa kuwa kukamata na kuweka ndani si jambo la kufanyika bila kuzingatia sheria.

Wanaelezwa kuwa wanapokamata mwananchi waangalie kosa, wasikamate watu kinyume cha utaratibu na kuwaweka ndani bila kuzingatia sheria.

Anaeeleza kuwa hali hiyo imeleta utulivu ndiyo maana taarifa za watendaji na wananchi kuwekwa ndani na viongozi hazisikiki mara kwa mara.

CHANGAMOTO

Waziri Mkuchika anapoulizwa ni nini changamoto kubwa katika kutekeleza utawala bora, anasema shida kubwa inayokwamisha utekelezaji wa masuala ya utawala bora ni (umma) watu wengi kutoelewa haki zao za msingi.

Hata hivyo anasema kazi inafanyika na kwamba kinachoendelea ni watu kueleweshwe haki zao kila wakati, kwa mfano hospitalini wafahamu kuwa kutibiwa ni haki yao siyo lazima kutoa rushwa.

Taifa linahitaji kutoa zaidi elimu kwa umma ili wananchi waelewe haki za msingi ili wazipate bila kusumbuka.

“Ndiyo maana tumeamua na kutekeleza kwa vitendo kuwa katika mikusanyiko yoyote tuwaite Takukuru watoe semina kuelimisha jamii kuhusu ubaya wa rushwa. Na wamekuwa wakifanya hivyo.”

Watu walikuwa hawadai risiti lakini baada ya kupewa mafunzo na kuhamasishwa na serikali kuwa kwenye risiti kuna kodi za serikali wameanza kudai risiti na wamebadilika si kama zamani.

“Wananchi wanahitaji mafunzo kuhusu maadili, uzalendo, kutaa rushwa, dawa za kulevya . Yote haya yafanyike kuanzia shule za msingi hadi taasisi za elimu ya juu.”

Habari Kubwa