John Mwakangale: Swahiba wa Nyerere na mwenyeji wa Mandela Mbeya, 1962

14Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
John Mwakangale: Swahiba wa Nyerere na mwenyeji wa Mandela Mbeya, 1962

UNAPOZUNGUMZIA uhuru wa Tanganyika, hukosi kutaja baadhi ya majina ya waliokuwa begabega na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

John Mwakangale, akizungumza na wanawake wa UWT. Kushoto kwake ni Mama Maria Nyerere na kulia kwake ni Fatma Karume. PICHA: JBM MAKTABA

Hapo ndipo unapokutana na mojawapo, mwaharakati wa nchini na Afrika, aliyekuwamo katika orodha ya kumuunga mkono, John Benedict Mugogo Mwakangale.

Marehemu Mzee Mwakangale kama alivyozoea kujiita JBM, kwa kumaanisha ufupisho wa jina lake, ambalo aliitumia zaidi kama ufupisho na alama ya saini yake binafsi.

Wakati leo anakumbukwa Mwalimu Nyerere tangu kifo chake kutimia miaka 22, John Mwakangale anatimiza miaka 19, tangu alipofariki nyumbani kwake Nditu wilayani Rungwe, mkoani Mbeya,

Ni utangulizi wa dodoso la gazeti Nipashe, lilipongumza na mtoto wa marehemu John Mwakangale, ambaye sasa naye ni Mzee Stephen Mwakangale, nyumbani kwake Forest jijini Mbeya, namna baba yake alivyoishi kisiasa kwa uswahiba mkubwa kikazi na binafsi na Mwalimu Nyerere.

Pia, ndiye aliyekutana na kuwa mwenyeji wa shujaa na Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, hata wanasiasa wengine wa Afrika.

Mandela, kwenye kitabu chake kiitwacho 'LONG WALK to FREEDOM' amemwelezea John Mwakangale na namna alivyompokea mkoani Mbeya mwaka 1962, kabla ya kwenda Addis Ababa, Ethiopia kushiriki Mkutano wa Muungano wa Ukombozi Kusini na Mashariki mwa Afrika (PAFMECA).

Mazungumzo ya mwandishi wa Nipashe na mtoto huyo wa marehemu Mwakangale, Mzee Stephen, ana ufafanuzi kuhusu aliyohadithiwa na mazungumzo yao ya maswali na majibu. Fuatilia mazungumzo yao ya ‘ana kwa ana’:

Mwandishi: Unamtaja vipi Mzee Mwakangale katika siasa za Tanzania, kiserikali na wakati huo chama cha TANU, alikuwa nani?

Stephen: Kabla ya uhuru, baba alikuwa mwajiriwa na mwanataaluma katika mifugo, yaani daktari wa mifugo, ilikuwa fani yake. Baadaye aliamua kujikita na siasa na mwaka 1956 akajiunga na Tanganyika African National Union (TANU), akishika nafasi ya Katibu wa Mkoa (Mbeya).

TANU ilipozaliwa, kulikuwapo na wakereketwa wengi kisiasa akiwamo baba, Nyerere, Joseph Kizurira Nyerere (mdogo wa Baba wa Taifa), (Kanali Mohamed) Kissoky na wengine wengi ambao walijikita katika ukombozi hata Kusini mwa barani Afrika.

Alikuwa PAFMECA akishiriki harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika. TANU ilipoasisiwa alichaguliwa na kuonyesha mchango mkubwa kisiasa na harakati hizo ilimfanya kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (LEGCO) mwaka 1957.

Mwandishi: Mahsusi ukienda katika uhusiano wake na Nyerere, yepi unaweza kuyaorodhesha alivyotoa mchango wake kwa mwalimu na serikali yake, maana ni vigumu kutofautisha TANU, Nyerere na serikali yake?

Stephen: Uhusiano unakuwapo, kwa sababu ya shughuli walizofanya ziliendana, siasa kuwa mwana TANU, pia Nyerere hivyo hivyo na baada ya uhuru wa Tanganyika, Nyerere akawa Rais wa Tanzania. Aliendelea kumteua kwenye nafasi za kitaifa na mkoa mara kadhaa, akijua atamwakilisha vyema kwa wananchi.

Mwaka 1962, alikuwa Mkuu wa Mkoa Nyanda za Juu Kusini na mwaka uliofuata, aliteuliwa na Rais kuwa Junior Minister of Local Government and Housing (Naibu Waziri wa Serikali ya Mitaa na Nyumba). Pia akawa Mkuu wa Mkoa Dodoma mwaka 1964.

Mwandishi: Wewe ni mwanawe? Naamini unajua huku Mbeya walisema Nyerere alimtegemea sana Mwakangale kama mmoja wa watu wake muhimu. Unaelezeaje?

Stephen: Mikutano kadhaa, baba aliandaa maeneo tofauti ya Mbeya. Nakummbuka ambao ulifanyika Tukuyu na Mwalimu Nyerere, alihudhurua, wakiwamo viongozi kadhaa wa TANU.

Mwandishi: Je, kuna wengi waliokuwa kama Mwakangale hapa Mbeya, unawaelezeaje kabla na baada ya uhuru?

Stephen: Alishirikiana na Mohammed Kissoky, Fatma Mwashambwa, Binti Matola. Kwa ujumla Kusini mwa Afrika nchi kadhaa zilikuja Tanzania kabla na baada uhuru na baba akiwa mwenyeji wao na baadhi walilala nyumbani mwetu Makandana, Tukuyu (Mbeya). Kulikuwa na ‘cross borders’ (njia ya mkato), Malawi, Zambia, Afrika Kusini kote huko.

Mwandishi: Nyerere alipokuja Mbeya, unamkumbuka uhusiano wao ulivyokuwa?

Stephen: Nakumbuka waliishi vizuri hadi mwisho, marafiki wa kweli tangu ujana wao. Nakumbuka mwaka 1967 nikiwa likizo nikisoma chuoni Nairobi, baba akaniambia anatakiwa kuuza sehemu yake, nikamjibu “ikiwa kutoka moyoni unakubaliana na hilo na Azimio la Arusha, uza” na kweli akauza. Kwa hiyo alikuwa mkweli.

Kimsingi, alikuwa muwazi, mkali na msimamo. Alisimamia alichokiamini. Ndio maana walielewana na Nyerere na alimwamini.

Mwandishi: Ukimkumbuka baba yako, unadhani ni mambo yepi katika maisha yake binafsi na hata kisiasa wamefanana sana na picha ya Nyerere?

Stephen: Wanaweza kufanana kwa kile walichotaka kifanikiwe, ndio maana walielewana na kuwa kati ya marafiki wake wakubwa.

Mwandishi: Je, mama yenu alikuwa mwanasiasa au kuambukizwa na baba yako ule U-Nyerere?

Stephen: Mama hakuwahi kuwa mwanasiasa.

Mwandishi: Kumbuka matukio muhimu ya nchini, uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Tanzania ya chama kimoja, kisha Muungano wa mwaka 1964; Azimio la Arusha 1967; Azimio la Iringa mwaka 1972, Siasa ni Kilimo; na Azimio la Musoma, Siasa ni Elimu, pia mwaka 1974 kuanzishwa vijiji vya Ujamaa mwaka 1975 na kuzaliwa CCM (mwaka 1977), baba alivyoenda ‘kumsapoti’ Nyerere au baba kuadhimisha uhuru?

Stephen: Matukio kadhaa tumeyakuta hasa katika picha, kwa sababu kabla ya uhuru nilikuwa masomoni shule za bweni kwa muda mrefu. Pia, chuo kikuu nje ya nchi na baada ya uhuru, nilikuwa nafanya kazi mikoa tofauti.

Hivyo, nilijua baba alikuwa akifanya shughuli mbalimbali za chama na serikali, hata kama sikushuhudia ana kwa ana.

Pia, iwapo alikuwa mkoa fulani nilipokuwa nikifanyia kazi, nilifahamu zilikuwa shughuli zake za kichama na alifika nyumbani kutusalimia.

Mwandishi: Nasikia alikuwa mjamaa. Elezea alivyokuwa, mlo na mavazi yake?

Stephen: Mavazi alikuwa anavaa mchanganyiko suti ilikuwa vazi rasmi. Ila alivaa zaidi kaunda suti na zile kama za Mao (Chuoenlai), ni kama wote walikuwa na msimamo mmoja katika mavazi.

URAFIKI NA MANDELA

Kwenye kitabu chake, 'LONG WALK for FREEDOM', Shujaa wa siasa za Afrika Kusini Nelson Mandela katika sehemu ya kurasa za kitabu hicho, anaeleza namna alivyokwa Mbeya, akipokewa na mwenyeji wake, John Mwakangale mwaka 1962. Sehemu ya nukuu yake Mandela katika kitabu hicho, ni kwamba:

"Asubuhi yake tulitoka kuelekea Mbeya, mji wa Tanganyika uliopo mpakani mwa Kaskazini mwa Rhodesia (sasa Zimbabwe). Tukiwa juu angani rubani alijaribu kuwasiliana na Mbeya. Mbeya…Mbeya, Lakini hakujibiwa!

“Hali ya hewa haikuwa nzuri, mawingu...hatimaye anga likawa safi...tulifanya 'booking' kwenye hoteli ya kawaida (Mbeya Hotel) na kukuta umati wa Waafrika, Wazungu hasa katika varanda (barazani), wakiendelea na mazungumzo yao taratibu.

"Tulikuwa tukimsubiri Mr. Mwakangale wa Chama cha Tanganyika African National Union (yaani TANU), mbunge na bila ya kujua kwamba alikuwa amewasili (hotelini). Alikuwa akitutafuta..."

Pia, mwaka 1990 wakati Nelson Mandela alipozuru Tanzania mara baada ya kutoka kifungoni, alipowasili Dar es Salaam, John Mwakangale alikuwa miongoni mwa wageni wa kitaifa walioalikwa kumlaki Mandela, akiwa Rais wa Afrika Kusini ambaye aliliongoza taifa lake kwa muhula mmoja tu.

Kadhalika, mwaka 1999 wakati Nelson Mandela alipofika kuwaaga Watanzania mkoani Dar es Salaam, kati ya wageni waalikwa, Mandela aliomba awe na orodha ya wageni wake maalumu siku hiyo na kukutana nao kwenye hafla ya kumuaga, akiwamo John Mwakangale, akipewa mwaliko huo na mwanaharakati huyo akifahamika zaidi kama 'Madiba' kutoka Afrika Kusini, aliyeacha historia na alama kubwa ya ukombozi duniani.

Pia John Mwakangale alisafiri na ujumbe wa Rais Nyerere hadi Zimbabwe, wakati huo ikiongozwa na Rais Reverend Banana huku Robert Mugabe akiwa, Waziri Mkuu, muda mfupi baada ya kupata uhuru Aprili 1980.

KIFO CHAKE

Mnamo Januari mwaka 2002, John Mwakangale, alifariki dunia nyumbani kwake Nditu, wilayani Rungwe, ikiwa ni miaka mitatu na miezi mitatu tangu kifo cha rafikiye, Mwalimu Nyerere.

Ni tukio lililomgusa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa, aliyetuma salamu za rambirambi na barua kwa familia kuwafariji.

Kijijini Nditu ni umbali zaidi ya kilomita 10 kutoka Katumba, eneo la umbali mfupi kutoka Tukuyu mjini, penye barabara inayoelekea Mashariki maeneo kama Mwakaleli na Lwangwa, ambako sasa ni Wilaya ya Busokelo. Pia, pana umbali mfupi kuelekea kijiji jirani cha Suma anakotokea, Profesa Mark Mwandosya.

Mkoa umemheshimu kwa siasa zake hapo na kitaifa, ambako jijini Mbeya kumetengwa viwanja maalum vilivyobeba jina lake – Viwanja vya John Mwakangale.

Habari Kubwa