Kamati za Walimu , Wazazi zapandisha nidhamu shule za msingi

10Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kamati za Walimu , Wazazi zapandisha nidhamu shule za msingi

KAMATI za Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) katika Shule za Msingi za Serikali nchini zimechangia kwa kiasi kikubwa kudhibiti utoro, kuongeza nidhamu na kuinua hamasa ya kufanya vizuri kwa baadhi ya Wanafunzi katika shule hizo katika mitihani ya kumaliza Elimu ya Msingi.

Mwaka 2015 Serikali kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania ( Education Quality Improvement Programme –Tanzania -EQUIP-T ), ilianzisha Kamati za Umoja wa Walimu na Wazazi ( UWW ) katika shule za msingi nchini, kwa lengo la kujenga uhusiano mzuri kati ya walimu na wazazi ikiwa njia mojawapo ya kuinua ubora wa elimu.

Kamati hizo, zilipewa jukumu la kufuatilia maendeleo ya Kitaaluma kwa wanafunzi, kubuni miradi mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya shule na kubuni klabu mbalimbali zitakazowashirikisha wanafunzi ili kujadili masuala ya kijamii hivyo kuwavutia wanafunzi kupenda masomo.

Mpango huo ,awamu ya kwanza ulianza katika mikoa ya Dodoma, Kigoma, Lindi, Mara, Simiyu, Shinyanga na Tabora, umeleta mafanikio makubwa kimaendeleo ya kitaaluma darasani, kuongezeka kwa nidhamu na kudhibiti utoro mazingira ambayo pia yameongeza ufaulu katika mitihani yao ya elimu ya Msingi.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Uhelela,wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Dankan Kamwela, akiuzugumzia mpango huo anasema kwamba, umepata mafanikio makubwa katika shule yake kwa kufanikiwa kupunguza utoro kutoka wanafunzi 127 sawa na asilimia 30 kwa siku mwaka 2015 hadi wanafunzi 12, sawa na asilimia nane kwa siku mwaka 2016.

Kwa kuitumia Kamati ya Umoja wa Walimu na Wazazi (UWW) alibainisha kwamba, wamekuwa wakifanya vikao mara kwa mara kwa kuwashirikisha wazazi na wanafunzi ili kujadili maendeleo ya shule na wajibu wa walimu, wazazi, na wanafunzi kwa ujumla.

Kufuatia vikao hivyo, kwa mujibu wa Mwalimu huyo, ilibainika kuwa, kuna haja ya kuweka mikakati itakayosaidia kurekebisha kasoro zote zilizoonekana kuchangia kushuka kwa maendeleo ya kitaaluma, utoro na nidhamu ambavyo kwa pamoja vinasababisha wanafunzi wasifanye vizuri katika mitihani yao kwenye shule za Kata hiyo.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Mkoa wa Mara,.Hamis Lissu amesema, ufaulu wa darasa la saba mkoani humo umekuwa ukipanda mwaka hadi mwaka, kuanzia mwaka 2014.

Mwaka huo mkoa wa Mara ameeleza, ulikuwa nafasi ya 25 kati ya mikoa 25, mwaka 2015 ulishika nafasi ya 17 kati ya 25 na mwaka 2016 umeshika nafasi ya 13 kati ya mikoa 26.

Mratibu Elimu Kata wa Chamwino, Chitema Simango amesema kuwa, Kamati hiyo imewezesha kwa kiasi kikubwa ushiriki wa wazazi katika maendeleo ya shule.

Kabla ya kuanzishwa Umoja huo, walimu walikuwa wakiachiwa ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi pamoja na shule, lakini kwa sasa wazazi na walimu wanashirikiana katika kufuatilia maendeleo ya wanafunzi na shule kwa ujumla.

Kama hiyo haitoishi, amesema kuwa UWW umeleta uwazi katika mapato na matumizi ya shule kwa kuyabandika katika mbao za matangazo za shule husika na wazazi wanapewa nafasi ya kuhoji kuhusu mapato na matumizi hayo.

Ametoa ushauri kwa maofisa elimu, Waratibu Elimu Kata na Walimu Wakuu katika mikoa ambayo haijaanzisha Kamati za UWW katika shule zao, kuanzisha ili kuleta mabadiliko ya uendeshaji wa shule za msingi za Serikali kwa kuishirikisha jamii.

Kimsingi kupitia UWW, Walimu na Wazazi wanajadiliana kwa pamoja na kukubaliana namna ya kuboresha taaluma ya Wanafunzi katika shule husika, hata katika kusimamia miradi ya shule.

Pia amesema kuwa, wazazi wanaposhirikiana na walimu husababisha Wanafunzi kuwa na nidhamu ya hali ya juu kutokana na mwanafunzi asiye na nidhamu au mtoro anakosa pa kukimbilia kwani mwalimu na mzazi wamekuwa kitu kimoja.

Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (Education Quality Improvement Programme –Tanzania- EQUIP-T ) ni mpango unaosimamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kudhaminiwa na Serikali ya Uingereza. Mpango huu ni wa miaka minne ulianza mwaka 2014 katika mikoa ya Dodoma, Tabora, Simiyu, Shinyanga, Kigoma, Mara na Lindi.

Mpango huo umejikita katika kuinua ubora wa elimu katika shule za msingi katika nyanja mbalimbali na kutoa mafunzo kwa walimu wa madarasa ya awali hadi la tatu ili kuwajengea uwezo wa ufundishaji, utoaji wa vifaa vya kufundishia, uanzishwaji wa kamati za walimu na wazazi pamoja na mafunzo ya uongozi kwa walimu wakuu, kamati za shule na umoja wa walimu na wazazi.

Habari Kubwa