Kambaya anavyowasikitikia vijana, ataka waandaliwe kutwaa uongozi

28Jul 2021
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Kambaya anavyowasikitikia vijana, ataka waandaliwe kutwaa uongozi

VIJANA ni taifa la leo na wanatakiwa kujengwa katika misingi ambayo itawafanya wawe viongozi wa baadaye, lakini pia wawe wazee wenye busara na hekima ambao ni hazina kwa vizazi vijavyo.

Abdul Kambaya ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi CUF Taifa. PICHA: MTANDAO

Ushiriki na mchango wao unahitajika katika uhai wa taifa, na kwamba kinyume cha hapo, nchi inaweza kukosa viongozi makini wa baadaye kadhalika kuwa na wazee wasio na manufaa kwa jamii zao, anasema Abdul Kambaya, Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la CUF Taifa.

Anasema ni kutokana na umuhimu huo, serikali inapaswa kuandaa mazingira rafiki kwa vijana ili waweze kushiriki katika masuala ya kisiasa, kwa kuwa hiyo ni miongoni mwa mambo yanayofanikisha kupata viongozi bora wa baadaye.

Kambaya anasema hayo katika mazungumzo na gazeti hili jijini Dar es Salaam na kudai kuwa vijana nchini hawawekewi mazingira ya kuandaliwa kuwa viongozi wa taifa kwa siku sijazo.

"Lakini kwanza nifafanue kuwa, vijana wanapoandaliwa kuwa viongozi, si lazima wawe wanasiasa, bali wanaweza kuongoza taasisi za umma za binafsi na hata za kijamii na kufanikisha kufikiwa makusudi na malengo tarajiwa," anasema Kambaya.

Anaongeza kuwa vijana wanatakiwa kuchangia maendeleo ya nchi yao, na kwamba hali ilivyo sasa, inaonyesha kuwa huenda wakakosekana viongozi wa baadaye na kupata wazee ambao itakuwa vigumu kuchota busara kwao kama mambo yataachwa kubaki kama yalivyo.

VIJANA MBUMBUMBU

Kambaya anasema, kwa sasa kuna baadhi ya vijana hawajui kinachoendelea katika nchi yao, pia hawatoi maoni na hata linapotokea jambo ambalo wanatakiwa kuchangia mawazo na mikakati hukaa kimya.

"Vijana wengi mijini unawakuta kwenye mitandao ya kijamii, wakiigiza maisha, kuandika mambo ambayo hayana umuhimu na pia wanafuatilia masuala yasiyo na maana kwao wala kwa taifa lao. Lakini idadi kubwa iko vijiweni haina kipato, kazi wala fikra za kimaendeleo," anaonya mjumbe huyo.

Anasema, wapo baadhi yao wanaoishi kwa kujipendekeza kwa viongozi, na kwamba wanaona ni jambo la kawaida bila kufanya juhudi zozote za kuwawezesha kuandaliwa kuwa viongozi wa baadaye.

"Ukifuatilia, utagundua kuwa, kwa sasa wapo baadhi ya vijana hawajui hata kuhusu corona, hawana taarifa za chanjo yake, hawafahamu kuwa Tanzania imeagiza chanjo tena hawana habari ya katiba inayowaongoza wala mahitaji ya katiba mpya," anasema Kambaya.

Anaonya kuwa nchi ikishakuwa na vijana ambao hawajui hayo na badala yake wanaishia kusoma magazeti ya udaku, mambo ya mitandao yasiyokuwa na tija, kukimbia kazi, masomo na kuishi vijiweni huku wakipuuza mambo ya msingi, miaka ijayo nchi inaweza kuingia gizani.

"Kiongozi wa nchi husaidiwa kiuchumi, kifikra na vijana, hivyo wanatakiwa kuandaliwa vyema ili waondokane na mambo yasiyokuwa na tija na serikali iwajibike kuhakikisha vijana wanakuwa sehemu ya maendeleo ya nchi hii,”

HATUA ZA KUCHUKUA

Mjumbe huyo anasema, si katika siasa tu, bali serikali inatakiwa kuwafanya vijana kuwa sehemu ya maendeleo ya uwekezaji, biashara na uchumi, badala ya kubaki watazamaji na ni vyema iwekeze kuanzia kwenye elimu na afya kwa vijana ili kulinda au kuwa na mtaji wa watu wenye siha na weledi kuliko ilivyo sasa.

Anasema, moja ya changamoto iliyopo kwenye elimu kwa mtazamo wake ni mitaala na madaraja kushindwa kumuandaa kijana kuwa na ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri kwa vile muda wote huwa darasani na kila anapofaulu kwenye daraja unakuwa msingi wa kwenda kwenye jingine.

Mfano, akitoka shule ya awali anakwenda shule ya msingi, baadaye sekondari na katika vyuo vya ufundi na vikuu lakini viwango vyote hivyo vya elimu, havimpi mwanafunzi ujuzi na maarifa ya kujiajiri zaidi ya kutegemea kuajiriwa, lakini pia haajiriki.

"Ni vyema sasa kwa serikali kuwa na mitaala itakayobaini chaguo na vipaji vya wanafunzi na kisha kuwapa elimu na ujuzi wa kujiajiri kutokana na chaguo lao na vipaji vyao kuliko kuwaacha waendelee kama walivyo," anasema.

MIFANO YA KUTAZAMA

Kambaya anatolea mifano ya vipaji vya michezo na sanaa kutoka kwa Mbwana Samatta, Simon Msuva ambao ni wacheza soka wa kimataifa, wanamuziki Diamond na Ali Kiba kuwa kama kungekuwa na mitaala ya kutambua vipaji , soko la uwekezaji na biashara kwa vijana lingekuwa kubwa nchini.

"Lakini kwa vijana waliofanikiwa kupata elimu ya vyuo mbalimbali na hata wale waliokosa elimu, serikali ina mipango gani ili kuhakikisha inawezesha  kuingia kwenye soko la uwekezaji na biashara ili wawe sehemu ya maendeleo ya uchumi wa nchi hii? Anahoji Kambaya.

Kambaya anasema, sera zinaweza kuwa nzuri, lakini zikakosa utashi wa kisiasa wa utekelezaji, au zinaweza kuwa si rafiki kwa vijana nchini kwa mukhtadha wa uwekezaji na biashara.

"Mfano, vijana wetu wawe na elimu wasiwe nayo, kupitia miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na kufua umeme wa maji kwenye Bwawa la Nyerere inadaiwa kuwa imekuwa na malipo madogo lakini pia inawanufaisha zaidi wageni kuliko Watanzania," anasema.

Anafafanua kuwa Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ni vyema utambue umuhimu wa 'mtajiwatu' katika kuutekeleza na kukuza pato la taifa kwa kuwekeza na kutenga fedha kwa ajili ya kuwanyanyua vijana.