Karatini ya kipindupindu Zanzibar yatishia mfungo

19Jun 2016
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Karatini ya kipindupindu Zanzibar yatishia mfungo

KIPINDUPINDU Zanzibar kimeibua mjadala mkubwa ukiwamo wafanyabiashara kupigwa marufuku kutoa huduma za vyakula pamoja na kuzuiwa mikusanyiko ya futari katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani mjini Zanzibar.

waumini wa dini ya kiislamu wakifuturu.

Utamaduni wa watu au familia Zanzibar kufutari pamoja umekuwepo miaka mingi lakini mwaka huu umepigwa marufuku kutokana na maradhi hayo yaliyodumu kwa miezi nane sasa.

Kabla ya kupinga marufuku mikusanyiko ya futari ya pamoja iwe msikitini au nyumbani, Wizara ya Afya Zanzibar ilichukua hatua ya kukataza chakula cha mikusanyiko katika harusi, Maulidi au sherehe.

Mfumo wa biashara Zanzibar umeathirika kwa kiwango kikubwa na kuvuruga mzunguko wa fedha na waathirika wakubwa ni wananchi wanyonge ambao maisha yao yanatokana na biashara ndogo ndogo ambao ni mama lishe wakiwamo wajane na vijana walioamua kujiajiri kwa kuanzisha migahawa na maduka ya chips.

Mbali na wafanyabiashara hao, wapo wachuuzi wa nyama na wauzaji viazi mviringo na viungo ambao nao wameathirika kutokana na soko kupungua katika Manispaa ya mji wa Zanzibar.

Pamoja na ugonjwa wa kipindupindu kuwamo visiwani humu, wafanyabiashara kisiwani Pemba wameendelea kutoa huduma za vyakula kama kawaida katika migahawa na maduka ya chips licha ya kuwepo kwa waathirika na waliopoteza maisha kutokana na maradhi hayo.

Licha ya uamuzi wa Wizara ya Afya kuzuia kufanyika biashara za vyakula katika migahawa sasa kumeibuka biashara ya magendo ya chakula kabla ya mfungo wa Ramadhani ambapo watu wanapelekewa kwa siri vyakula katika maeneo yao ya kazi.

Biashara hiyo ya magendo inalazimika kufanyika kutokana na familia nyingi hazina njia nyingine ya kutafuta mahitaji ya familia zaidi ya kujituma kwa kufanya biashara kupunguza ukali wa maisha.

Hata hivyo, takwimu za maradhi hayo zinaonyesha watu 60 hadi wiki iliyopita wamepoteza maisha kwa kuungua kipindupindu katika visiwa vya Unguja na Pemba kutoka kuibuka ugonjwa huo Septemba mwaka.

Bado harakati za usafi si za kuridhisha katika makaazi ya watu na huduma za kijamii mfano masoko.

Mbali na vifo watu 4,150 wameungua na kutibiwa katika vituo saba Unguja na Pemba lakini wagonjwa wapya 22 wameripotiwa kati ya Mei 29 na Juni 4 mwaka huu, ambapo mtu mmoja alipoteza maisha kati ya waathirika hao.

Maradhi hayo yanaelezwa na wataalamu wa afya akiwemo Mkurugenzi wa Kinga Zanzibar Dk. Mohamed Dahoma, kuwa kasi ya maambukizi imepungua kutokana na uwelewa na kupiga marufuku utoaji wa huduma za vyakula, pamoja na usafi wa mazingira visiwani hapo.

Pamoja na nia njema ya serikali ya kuzuia kufanyika biashara za vyakula bado kuna umuhimu pia wa kuangalia athari zinazoendelea kujitokeza kwa wahusika waliokuwa wakitegemea maisha ya ujasiriamali huo kwa kila siku. Kama biashara walizokuwa wakifanya zimekwama wanaishije?.

Kama serikali imekuwa ikifanya juhudi za kuwataka wananchi kujiajiri ili kufanikisha Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini kwa Zanzibar (Mkuza) serikali imezingatia vipi mpango wa mafanikio yake.

Mafanikio ya watu wazima na vijana yaliyokuwa yameanza kuonekana kwa kujiajiri na kunufaika na mikopo kupitia asasi za kiraia kutokana na biashara walizokuwa wakifanya lakini sasa wamegeuka wapiga soga vijiweni na kukwama kurejesha mikopo yao.

Serikali isitazame matatizo haya kwa upande mmoja kama safari ya treni lazima iangalie faida na madhara yake na hatima baada ya kutofanya biashara kwa muda wa miezi mitatu.

Wakati muafaka ukifika umma unategemea kuona Wizara ya Afya kueleza kazi ya usafi wa mazingira katika makazi ya watu, mitaro ya kuhifadhi maji machafu imefanikiwa kwa asilimia ngapi tangu kuibuka kwa maradhi hayo pamoja na juhudi zilizofanyika za usafi katika maeneo wanayotoka wagonjwa wa kipindupindu.

Hakuna njia ya mkato ya kumaliza tatizo la kipindupindu Zanzibar zaidi ya mamlaka kuimarisha usafi wa mazingira na kusimamiwa vizuri kanuni za afya katika maeneo ya biashara.

Kama asilimia 70 ya wananchi wanategemea biashara ndogo ndogo katika kukamilisha mipango ya sikukuu baada ya kukamilika mfungo wa mwezi wa mtukufu wa Ramadhani itakuwaje katika matayarisho yake, kama watoto wakiwa wamekuzunguka wanasubiri mahitaji yao wasipate mkate?

Mbali na wafanyabiashara waliokwama kurejesha mikopo katika asasi za kiraia pamoja na michezo ya kukopeshana kama upatu kutokana na kukwama kwa biashara zao na kulazimika kuanza kutumia mitaji kwa mahitaji ya nyumbani na familia, mambo yatakuwaje baada ya ugonjwa kuisha?

Suala la kuimarisha usafi wa mazingira na kanuni za afya lazima uwe utaratibu wa kudumu katika maisha kupambana na kipindupindu badala ya watu kuzuiwa kufanya biashara.

Habari Kubwa