KARDINALI PENGO: Wanasiasa mna ujasiri wa Nyerere kusema ukweli?

13Nov 2019
Raphael Kibiriti
Dar es Salaam
Nipashe
KARDINALI PENGO: Wanasiasa mna ujasiri wa Nyerere kusema ukweli?
  • Mwalimu alikiri kwenda Bagamoyo!

JUMATANO Oktoba 30, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliongoza Adhimisho la Misa Takatifu iliyokuwa imeandaliwa na Umoja wa Wanamawasiliano Wakatoliki wa jimbo hilo (UMAKADA).

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.PICHA: MTANDAO

Umoja huo uliandaa adhimisho hilo kama shukrani kwa ajili ya maisha ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ikiwa ni sehemu ya Kumbukumbu ya miaka 20 toka alipofariki Oktoba 14, 1999, kwenye Hospitali ya Mtakatifu Thomas, nchini Uingereza.

Mwalimu alikuwa vilevile muumini wa kanisa hilo, sasa akiwa na hadhi ya Mtumishi wa Mungu, katika taratibu za kanisa hilo.

Mwandishi alikuwa mmoja wa waliohudhuria adhimisho hilo na katika mahubiri ya Kardinali Pengo, aliguswa zaidi na kipengele kilichoangazia ujasiri wa Mwalimu wa kusema ukweli juu ya nafsi yake kwa gharama yoyote.

Pamoja na mengine, kipengele hicho kilimgusa mwandishi kwa sababu taifa sasa linaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 4 mwaka huu, ambapo wananchi watachagua viongozi wao katika ngazi ya serikali za mitaa.

Viongozi watakaochaguliwa ni pamoja na wenyeviti wa vitongoji, vijiji, mitaa na wajumbe wa serikali za mitaa.

Aidha, mwakani (2020), taifa litaingia kwenye uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani, pia Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani, kwa upande wa Zanzibar.

Chaguzi hizo ambazo pamoja na wengine, zinawahusisha vilevile wanasiasa kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere.

Kimsingi wanasiasa hawa, lakini raia wengine kutoka kada tofauti za maisha, wana la kujifunza kutokana na mahubiri hayo ya Kardinali Pengo, hususani juu ya kipengele hicho cha ujasiri wa kusema ukweli aliokuwa nao Baba wa Taifa.

Ujasiri ambao haukujali hofu juu ya nafsi yake au nafasi yake ya uongozi wa kisiasa, kijamii, kiuchumi hata wa imani yake.

“Mfano wa mwisho wa uinjilishaji wa Mwalimu ambao ningependa kuutoa jioni ya leo ni huu…juzijuzi nilikuwa namsikiliza Mwalimu katika yale anayoongelea, akaongea kwa uwazi kabisa jinsi alivyokuwa Bagamoyo na wazee,” anasema na kuongeza akimunukuu Mwalimu:

“Majority (wengi) ya wale pengine wote waliokuwapo walikuwa ni Waislamu, isipokuwa mimi tu ndiyo Mkristo au labda kama alikuja John Rupia, alikuwa ndiyo Mkristo mwenzangu tuliyekwenda pamoja naye.”

Kardinali Pengo akaendelea kunukuu alichosema Baba wa Taifa akieleza jinsi walivyochinja mbuzi, kumwaga damu ili kummaliza (Edward) Twining na wazee kumwambia aruke.

“Haya, Mwalimu anayaeleza vizuri kabisa, sasa sijui wengine kama mnaweza kuona jambo la uinjilishaji katika hilo, sijui… mimi kwangu sitaki kutoa hukumu juu ya yale aliyofanya Mwalimu na ametueleza mwenyewe kwa uwazi,” anasema na kuongeza:

“Sitaki kutoa hukumu, lakini swali langu ni hili, je yeye (Mwalimu Nyerere) ni mwanasiasa peke yake aliyekuwa anakwenda Bagamoyo? na mpaka leo hatuna wanasiasa Wakatoliki wanaokwenda huko!”

Kardinali Pengo aliendelea kusaili katika mahubiri yake hayo juu ya hili la wanasiasa na wengine hasa katika kipindi hiki taifa linapoelekea kwenye chaguzi za kupata viongozi wake.

“Na kwa nini nauliza hilo, nauliza wengekuwapo, au wapo hawa waenda huko Bagamoyo au mahali pengine, wengine wanasema Sumbawanga, sijui wapi kwenda kujipatia uwezo wa kupata kura nyingi na kupita, wapo wangapi wanaokwenda huko wangekuwa tayari kutamka kama Mwalimu alivyotamka juu ya nafsi zao? hilo ndilo swali langu kubwa.”

Askofu huyo Mstaafu anaendelea kuhoji iwapo hawapo wanasiasa wanaoenda Bagamoyo ama mahali pengine na kama wapo anasaili kama miongoni mwao wangekuwa tayari kuwa na ujasiri wa kueleza hayo.

“Kuhukumu juu ya madhambi ya mtu ni Mungu anajua, lakini kuwa na ujasiri wa kutamka ukweli mimi nilienda Bagamoyo, wakachinja beberu, nikaruka kaburi lake…nilikuwa peke yangu mkristo, sijui wangapi leo wanaweza kuwa na ujasiri wa kusema ukweli huo juu ya nafsi zao,” anasema na kuongeza:

“Na ninapouliza hilo siyo kwamba labda ni wanasiasa tu, huenda siyo wanasiasa tu, je inawezekana labda wakawepo mapadri wanaokwenda huko… tuseme mimi kama nitakwenda huko, nitakuwa na ujasiri wa kuja kuwaeleza kama mwalimu alivyokuwa na ujasiri wa kueleza hilo.”

Aliwasisitiza wanasiasa na wengine kuwa tayari kusema ukweli hata kama ni kwa gharama ya nafsi zao kisiasa, kijamii, Kiuchumi na kiimani kama Mwalimu Nyerere alivyofanya enzi ya uongozi wake.

PAULO RUPIA

Kabla ya adhimisho hilo la Misa, ambalo lilihudhuriwa pia na watu wa kada mbalimbali wakiwamo viongozi wastaafu wa serikali, ambao baadhi yao walifanya kazi kwa karibu na Baba wa Taifa, kuliendeshwa Mada kumhusu kiongozi huyo wa Tanzania.

Mada hizo zilizoongozwa na Padre Vitalis Kasembo, Mkurugenzi wa Utume wa Walei wa jimbo Kuu, ziliangazia nafasi ya Mwalimu Nyerere kama Mwinjilishaji katika jamii, vilevile nafasi yake kama mwanamawasiliano katika Jamii.

Akichangia mada hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu enzi za utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, Balozi Paul Rupia, alisema Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi mwenye maono ya mbali kwa ajili ya ustawi wa Tanzania.

“Toka mwanzo Mwalimu alitoa kipaumbele katika masuala mazima ya usawa, haki, kutooneana katika jamii na alifanya hivyo akiongozwa na dhana ya upendo, nia yake ikiwa wote twende pamoja,” anasema na kuongeza:

“Hivyo leo hii kama taifa tunapovuna amani tuliyonayo nchini, ni mbegu ya upendo aliyoipanda wakati ule, hivyo tunapaswa kama nchi tumuenzi, tumuishi kwa kuitafsiri vizuri amani tuliyonayo.”

PADRE JOSEPH MASENGE

Akizungumza katika adhimisho hilo, mbali na kushukuru kwa mahubiri yake, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mlezi wa UMAKADA, Padre Joseph Masenge, alimuomba Mwadhama aendelee kuwamegea Watanzania yenye ustawi aliyoyonayo kila fursa inapojitokeza kama alivyofanya siku hiyo.

Habari Kubwa