Kariakoo ya 'Hapa Kazi' ilivyofyeka deni la kutisha, yageuka rafiki TR

06Dec 2019
Maneno Selanyika
Dar es Salaam
Nipashe
Kariakoo ya 'Hapa Kazi' ilivyofyeka deni la kutisha, yageuka rafiki TR
  • *Soko jipya, mageuzi makubwa yaja

UNAPOTAJA Kariakoo kwa Kiswahili cha mitaani 'ni jina kubwa mjini'. Hicho ni kitovu cha Jiji la Dar es Salaam ambacho kimeteka biashara si kitaifa tu, bali Afrika Mashariki na Kati.

Lango la kuingia soko kuu. PICHA: MTANDAO

Hapo unataja wateja wa bidhaa zaidi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa uchache unawataja watu kutoka Malawi, Zimbambwe, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Umaarufu wa Kariakoo kibiashara si wa jana wala juzi, bali unaenda sambamba au hata zaidi ya uhuru wa nchi unaotarajiwa kusheherekewa Jumatatu ijayo.

Hilo ndilo chimbuko la aliyekuwa Rais wakati huyo, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kuchukua hatua za makusudi katikati ya Kariakoo yenyewe, akaipa kandarasi Kampuni ya Ujenzi ya Mwananchi (MECCO) kujenga soko la kisasa ambalo kwa wakati huo halikuwa na mpinzani.

Jengo la aina yake ambalo halina kingo za kawaida zilizozoeleka katika majengo yaliyotapakaa kila mahali, chini yake kukiwa na eneo lililobuniwa, maarufu kwa jina la 'shimoni' ambako ndiko kulikuwa soko kuu la jumla.

Mfumo mzima wa soko hilo linalopambwa na masoko madogo nje yake, mwaka 1974 baada ya kukamilika, serikali ililiundia taasisi inayodumu hadi leo inayoitwa Shirika la Masoko Kariakoo.

MENEJA MKUU

Hetson Msalale, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, anasema shirika hilo lenye miaka 45 hivi sasa lina historia ndefu ya kupitia vipindi mbalimbali vya uhai wake, tangu lilipozinduliwa rasmi na Rais Nyerere Desemba 8, 1975.

Baada ya kuwa kioo cha biashara kilichotamba kwa miaka mingi ndani ya jiji na kimataifa, pia limekutana na milima na mabonde ya kibiashara, ikiwamo mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini mwaka 1985 yaliyofungua mlango huria na kasi kubwa ya ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam.

Leo hii, shirika hilo lililobahatika kupitia mikono ya awamu zote za uongozi wa nchi, isipokuwa miaka 13 ya kwanza ya uhuru, liko chini ya uongozi wa Rais John Magufuli.

Meneja huyo anataja mambo kadhaa yanayohusu mafanikio ya shirika, ikiwamo kupata safu na muundo kamili wa uongozi kisheria baada ya kulegalega kwa miaka 16, kati ya mwaka 1999 hadi 2015.

Msalale anafafanua muundo huo ni kuundwa kwa Bodi ya Wakurugenzi yenye mwenyekiti, pia kumteua mtendaji mkuu, ambaye ni meneja mkuu, ikiwa ni kati ya uamuzi mkubwa wa awali uliofanywa na Rais Magufuli akiwa na wastani wa mwezi mmoja madarakani.

Anataja sehemu ya madhara yaliyotokana na kukosekana kwa uongozi kamili wa shirika na kuyumba kiutendaji, hali iliyochangia deni kubwa lililofikia Sh. bilioni 1.3, kutokana na madai kama ya kodi za mishahara na ardhi.

BIASHARA IKOJE?

Msalale anasema shirika hadi sasa limefanikiwa kuongeza wigo wa mapato yake, kupitia kuongezwa kwa maduka mapya madogo 99, maarufu 'Vigoli' kuzunguka jengo kuu la soko.

Anaainisha mustakabali wa bajeti ya Shirika la Masoko Kariakoo, likiwa na ongezeko la asilimia 32.4, akimaanisha ni kutoka Sh. bilioni 2.5 mwaka 2015/2016 ilipoundwa bodi hadi bajeti iliyoko sasa ya Sh. bilioni 3.7. Ni ongezeko la mara moja na nusu.

“Ukuaji huu wa bajeti ya shirika umekuwa ni kwa wastani wa asilimia 8.1 kila mwaka,” Msalale anasema na kufafanua kwamba, mradi wa maduka umeongeza wastani wa mapato kutoka Sh. milioni 48.263 kwa mwezi.

Kuhusu madeni, meneja huyo anasema hamasa na mwongozo unaoanzia kwenye bodi mpya, imewezesha kukombolewa deni la Sh. milioni 800, ambayo ni wastani wa theluthi mbili ya deni iliyolikuta (asilimia 61.5).

Sambamba na kukombolewa deni, anasema shirika hivi sasa 'halilazi' madeni stahiki ya kisheria kwa Mamlaka ya Mapato (TRA), akitaja mfano mojawapo wa makato ya kodi ya mshahara ya Lipa Kadri Unavyopata (PAYE).

“Haya ni mafanikio makubwa ndani ya shirika chini ya uongozi wa Rais John Pombe Joseph Magufuli, tangu alipoingia madarakani," anasifu.

MIRADI MIKUBWA

Msalale anasema kwa sasa, shirika lina mpango mkakati wa kuboresha jengo la soko lake dogo, kuligeuza katika mhimili mkubwa na wa kisasa, likikadiria kutumia zaidi ya Sh. bilioni 23.

Vilevile, meneja huyo anataja mpango mwingine ni upembuzi unaoendelea wa kujenga soko lingine la kisasa nje ya Jiji la Dar es Salaam, katika Manispaa ya Kinondoni unaokadiriwa kugharamu zaidi ya Sh. milioni 500 na uwekezaji kama huo katika eneo lake lingine la Tabata katika Manispaa ya Ilala.

Kwa mujibu wa meneja huyo, ndani ya miaka hiyo minne, limetoa ajira 27 na kuanzisha maeneo mapya maeneo mapya ya biashara kwa wajasiriamali 300.

KUPANUKA MTAJI

Msalale anasema tathmini ya shirika hadi Juni mwaka huu, inaonyesha kwa sasa linamiliki mali zenye thamani ya Sh. bilioni 56 kutoka Sh. bilioni 53.2 za miaka mitano iliyopita. Ni ongezeko la Sh. bilioni 2.8 na linajiendesha kwa kutumia mapato yake.

Anafafanua wigo wa mafanikio yake kwamba, kwa mwaka wa fedha uliopita, Shirika la Masoko Kariakoo ni miongoni mwa asasi za umma zilizowasilisha mchango wake serikalini, akitaja kiwango cha Sh. milioni 50.

Meneja Mkuu anaendeleza wigo wa majivuno yake, akitaja kuwapo maslahi bora kwa watumishi wa asasi hiyo kwa kutumia mapato ya ndani ambayo kwa sasa hayayumbi.

Habari Kubwa