KARIBU MWANAMFALME: Jionee twiga, tembo, simba na maajabu ya Tanzania

23Sep 2018
Gaudensia Mngumi
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
KARIBU MWANAMFALME: Jionee twiga, tembo, simba na maajabu ya Tanzania

TANZANIA yapendeza inavutia na inaalika wageni kutoka pande zote nne za dunia. Kwa zama hizi vijana wanasema Tanzania inatisha. Hicho ndicho kinachoweza kuzungumzwa wakati huu wa ujio wa Mwanamfalme wa Uingereza Prince William.

 Mwanamfalme William.

Akiwa Balozi wa kupinga ujangili, William anakuja nchini kuanzia wiki ijayo kwa mujibu wa taarifa zinazotolewa na Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC.

Ni miongoni mwa watu mashuhuri na wa kuheshimika wanaotembelea nchi hii. Anaungana na waheshimika wengine walioizuru Tanzania ambao ni pamoja na Barack Obama, Rais wa zamani wa Marekani, Waziri Mkuu mstaafu wa Israel Ehud Barak, Rais wa Uswizi na wote hawa wamekuja , wamefurahia kukaa na kuisifu Tanzania kuwa ni nchi ya kipekee duniani.

Tanzania nyakati hizi imepokea pia watalii ambao ni watu mashuhuri wakiwamo wacheza mpira maarufu kwa mfano wanakandanda wa timu ya Liverpool, amefika pia David Beckham nyota wa zamani wa Manchester United wanamichezo wote hao ni kutoka Uingereza.

Kitabu cha picha na maandiko kuhusu vivutio vya moja ya maajabu ya dunia hii, kiitwacho Ngorongoro cha Reinhard Kunke, neno la utangulizi linaandikwa na mstaafu Benjamin Mkapa, anayeitaja Tanzania kuwa ‘cradle of humankind’

Mkapa anaisifu nchi yake kuwa ‘Cradle of Humankind’ kwa sababu ndilo chimbuko la maisha ya binadamu wa kale na mabaki  na visukuku vyake (fossils) yaibuliwa baada ya utafiti na kazi iliyofanywa na familia ya Mary na Dk. Louis Leakey, huko Olduvai Gorge, mkoani Arusha.

Mkapa wakati huo akiwa Rais, anaeleza kuwa Tanzania ni ‘hall mark of human kind’ kwamba ndiko kwenye alama rasmi za kuthibitisha kihistoria na kisayansi kuwa, ardhi hii ni makao ya mwanzo ya binadamu, akiifananisha na Bustani ya Edeni.

Anaeleza kuwa japo amezoeleka kwa wengi kuwa ni Amiri Jeshi Mkuu, yanapokuja masuala ya uhifadhi wa maliasili na vivutio vya kihistoria , malikale na rasilimali zote za taifa hili yeye ni Mhifadhi Mkuu. .

Leo hii Tanzania imeendelea kuheshimika kama ‘Cradle of Humankind’ ndiyo maana Mwanamfalme William anakuja kushuhudia ukweli huo na kuiona nchi yenye kuvutia na vivutio vya kipekee kuanzia wanyama wa kila aina ndani ya hifadhi za taifa takribani 16.

Si hivyo tu kuna maajabu matatu ya dunia kati ya saba. Hayo ni pamoja na Bonde la Ngorongoro ambako wanyama pori na wanadamu huishi pamoja kwa utaratibu unaokubalika kiikilojia.

Pia, maajabu mengine ni kuwapo paa la Afrika au Mlima Kilimanjaro ulio mrefu kuliko yote Afrika (‘the roof of African’). Ni wa pili duniani kwa urefu.

Lipo ajabu la tatu ambalo ni mbuga ya wanyama ya Serengeti yenye mfumo wa wanyama kufanya utalii kati ya Tanzania na Kenya. Wanyama hao wanakwenda kwa matembezi ya muda nchini Kenya na kurudi kuendelea kuishi Tanzania kwa utaratibu unaoitwa ‘the great migration.’

Kwa ujio wa Mwanamfalme William kuja Tanzania ni jambo jema la kufurahisha linalothibitisha kuwa nchi hii inajulikana na inavyokubalika kimataifa kwenye uwanja wa utalii.

UJIO UNACHUKULIWAJE?

Geoffrey Meena wa Bodi ya Utalii (TTB) anapozungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam kuhusu ujio huo anasema hili ndio lilikuwa swali la kwanza la kumuuliza.

“ Ni jambo la kufurahisha kila mmoja, Mwanamfalme ni kiongozi mashuhuri na anayefahamika na kuheshimika dunia nzima siyo Uingereza pekee hata mataifa mengine, yakiwamo ya Jumuiya ya Madola.

“TTB tunaupokea ujio wake kwa fruraha kubwa, kwani ni fursa muhimu ya kutuonyesha kuwa utalii wa Tanzania unafahamika duniani na pia tutamtumia kutangaza utalii wetu zaidi huko Uingereza ambayo ni ya pili kwa kuleta watalii wengi nchini. Ni moja ya tatu bora ya kuleta watalii Tanzania,” anasema Meena.

Anaeleza kuwa hiyo ni fursa ya kipekee na William amekuja nchini kama Balozi wa Kupinga Ujangili , lakini pia kutambua na kuthamini juhudi zinazofanywa na Mhifadhi Mkuu , Rais John Magufuli, kukabiliana na ujangili wa tembo na mauaji ya wanyama pori.

NINI CHA KUMTANGAZIA MWANAMFALME

Meena anapoulizwa ni nini kitakachokuwa kipaumbele kwa Mwanamfalme ili kuitambulisha Tanzania kimataifa, anasema utambulisho mpya wa Tanzania kwenye utalii sasa ni “Unforgettable Tanzania” au Tanzania isiyosahaulika’

Kauli mbiu hii ni tangazo tosha kwamba kuna vitu vingi mno kuanzia ukarimu wa watu kwa wageni wanaotembelea Tanzania, kwa mujibu wa maelezo yake.

Vivutio vya ajabu na vya kipekee mfano Mlima Kilimanjaro, mrefu kuliko yote Afrika, Ziwa Tanganyika lenye kina kirefu kuliko yote. Ziwa Victoria kubwa kuliko yote Afrika. Kadhalika mbuga ya Selous yenye ukubwa kuliko zote Afrika ni mambo anayotakiwa kuyaona.

Hivyo, mgeni yeyote anayefika Tanzania hawezi kuisahau kutokana na wingi wa vivutio vikiwamo pia utalii wa kitamaduni na kimazingira, anasema Meena.

“Pamoja na vivutio kuna wakati tulifanya utafiti kuangalia kile kinachowafurahisha zaidi wageni wetu. Wengi walituambia kuwa ni ukarimu , upendo na utulivu wa Watanzania. Wengi hawakukimbilia kutaja Ngorongoro, bali watu wanavyowapokea, kuwafurahia, kuwahudumia na hali ya usalama kwani wanasafiri na kurudi salama wakiwa kwenye vivutio mbalimbali wanavyotembelea,”

TTB inasema kwa ujumla kuna vivutio ambavyo hakuna anayeweza kuvizidi kwa mfano maajabu makuu saba ya dunia matatu yapo nchini nayo ni Mlima Kilimanjaro, kuhama wanyama na Bonde la Ngorongoro.

MWALIKO

Je Mwanamfalme amealikwa kuja nchini? Ni swali ambalo Ofisa wa TTB , analijibu kuwa , kiongozi huyo anachagua nchi mwenyewe, licha ya kwamba Ubalozi wa Uingereza na Wizara ya Mambo ya Nje ndiyo wanaoratibu ziara hiyo.

Kwa mujibu wa BBC Mwanamfalme William anatarajia kufanya ziara ya karibu wiki moja barani Afrika kuanzia kesho. Pamoja na kuitembelea Tanzania atazizuru Kenya na Namibia.

Hata hivyo Nipashe ilishindwa kuthibitisha ujio wake kwani maofisa wa Ubalozi wa Uingereza jijini Dar es Salaam, walipoombwa kuzungumzia suala hilo hawakuwa tayari badala yake waliagiza kutafutwa kwa simu za mezani.

Lengo la Mwanamfalme ni kufuatilia juhudi za kukabiliana na ujangili na uhifadhi wa wanyama pori kwani ni Rais wa Mashirika yanayotetea Uhifadhi wa Wanyama maarufu kama United for Wildlife na Tusk Trust, kwa mujibu wa BBC.

Aidha, ni mlezi wa shirika la Royal African Society linalolenga kukuza uhusiano kati ya Afrika na Uingereza na pia ni mdau mkubwa wa juhudi za kukabiliana na ujangili.

UJIO UONGEZE HAMASA

Ujio wa Mwanamfalme William na mstaafu Obama, unaonyesha kuwa Tanzania inafahamika zaidi kwa mataifa yenye utamaduni unaofanana kwa vile Uingereza na Marekani ziko karibu kiutamaduni na kiuchumi.

Je TTB ina mikakati gani ya kuvutia vigogo kama Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na viongozi mashuhuru kutoka mataifa yanayozungumza Kifaransa kama Emmanuel Macron?

Meena wa Idara ya Masoko ya TTB, anasema juhudi zinafanyika kupitia balozi za mataifa mengi kwa mfano Ufaransa hivi karibuni walikuja wawekezaji ambao wanalenga kwenye viwanda na uchumi, hivyo kwa kuhamasisha wawekezaji pia wanaalika watalii kuzuru vivutio mbalimbali.

“Ni dhahiri jitihada zaidi zinafanywa kupitia mabalozi kuwafikia watu karibu pande zote muhimu za dunia, wakiwamo watalii kutoka Ujerumani. Hata hivyo Rais wa Uswisi alishaizuru Tanzania,” anasema Meena na kuongeza kuwa kuna watu mashuhuri ambao wanakuja kwa usiri mkubwa na hawataki kufahamiki wala kutangazwa.

Anasema kuwa nchi zinazoleta watalii wengi nchini ya kwanza ni Marekani , Uingereza, Italia na Ujerumani na kwamba mataifa kama Italia na Ujerumani yamo ikiashiria kuwa juhudi zimefanywa na zinaendelea kufanyika kuwavuta.

Anaeleza kuwa mbia na mdau mwingine kwenye utalii ni India ambaye mwaka 2016 ilipaa na kuwa taifa la pili kwa kuwa na idadi kubwa ya watalii walioizuru Tanzania.

India mwaka 2017 inaendelea kuwa kwenye orodha ya 10 bora kiutalii na kwamba kuna mipango wa kufikia soko la India na kuhakikisha kuwa inaleta watalii zaidi.

Jitihada zinalenga kutumia ndege yaTanzania ya Dreamliner kwenda India katika jitihada za kujiunganisha na kuwa sehemu ya kuendeleza utalii

“Juhudi zinafanyika za kukuza utalii kwa kuwa na mwakilishi wa TTB India atakuwa anahusika na utalii na uwekezaji. Kazi yake kubwa ni kuitangaza Tanzania kwa India na kushughulikia uwekezaji  na pia kusafiri kwa kutumia ndege za ATCL.”

Habari Kubwa