Kasa kutamia, ngadu mitini, ni maajabu hifadhi baharini

02Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kasa kutamia, ngadu mitini, ni maajabu hifadhi baharini

NI kawaida kuona hifadhi za wanyama pori, mapori tengefu na ardhi oevu vyote vikiwa vimehifadhiwa na kulindwa na serikali vyote vikiwa juu ya ardhi.

Mnyama dugong, papa potwe na ngadu wanaotoboa minazi ni moja ya vivutio maarufu ndani za hifadhi bahari, PICHA ZOTE: MTANDAO.

Lakini ni kwa nadra kusikia au kuona hifadhi ya viumbe bahari kama ilivyozoeleka kwa wanyama pori walioko Serengeti au Mgorongoro.

Hata hivyo, chini ya bahari nako zipo hifadhi za viumbe bahari, kuanzia mimea, wanyama, ndege na wadudu wa aina mbalimbali, ambao pengine hawalindwi na askari wa wanyama pori kama ilivyoeleka kwenye hifadhi za ardhini.

Tanzania Bara inaelezwa kuwa na hifadhi za viumbe bahari 18. Sehemu hizi kitaalamu huitwa Marine Protected Areas (MPAs), kwa mujibu wa Dk. Albogast Kyamukuru, mtaalamu wa elimu ya viumbe maji.

Dokta Kyamukuru ambaye alifanya utafiti wa shahada za uzamivu katika kisiwa cha Mafia ambayo ni moja ya hifadhi maarufu ya bahari duniani, kwa miaka mingi kabla ya kustaafu alikuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akizungumza na Nipashe kuhusu hifadhi za bahari anasema hifadhi hizo ni Kisiwa cha Mafia maarufu kama Mafia Island Marine Park, kuna kisiwa cha Nyororo, Mbarakuni na Shungimbili vyote viko wilayani Mafia mkoa wa Pwani.

Kamukuru anataja hifadhi nyingine kuwa Mnazi Bay Ruvuma inayopatikana Mtwara, wakati mkoani Tanga ziko kadhaa kama oelacantha iliyoko Muheza na kuna Kisiwa cha Mwewe.

Jijini Dar es Salaam, msomi huyu wa viumbe bahari anasema kuna hifadhi ya kisiwa cha Bongoyo, Fungu Yasini, kisiwa cha Mbudya, Pangawee, Sinda, Kendwa na Makatube.

“Mafia Island Marine Park ndiyo kubwa kuliko zote hapa Tanzania. Ilianzishwa mwaka 1995 kufuatia sheria ya kuhifadhi viumbe bahari iliyotungwa mwaka 1994. Ina eneo kubwa kuanzia rasi ya Chole (Chole Bay) na eneo la hifadhi ya matumbawe ya Kitutia ( Kitutia Reef marine reserves…)” anaeleza.

UMUHIMU WA HIFADHI

Mtaalamu huyu anasema hifadhi ya bahari ni muhimu kwani ndilo eneo linawezesha kupatikana taarifa za kiikolojia ya bahari na viumbe hai.

Lakini, pia kuna ekolojia ya mimea ya mwambao mikoko , matumbawe, mimea ya bahari, (sea grass) na kadhalika misitu ya mwambao.

“Kuna viumbe bahari wa kipekee kwenye hifadhi ya Mafia yuko mnyama bahari aitwaye ‘dugong’ anayeishi kwa kula nyasi. Ni miongoni mwa wanyama walio kwenye hatari ya kutoweka dunia akitajwa na shirika la kutetea wanyama waliokatika hatari ya kutoweka la CITES.” Anasema mtaalamu.

Anaongeza kuwa hifadhi ya Mafia imejaa aina tano za kasa (kobe wa bahari) wenye viota ambao hutamia mayai kwenye mchanga ufukweni.

“Whale shark au potwe ni miongoni mwa samaki wakubwa wenye zaidi ya mita 12 ambaye anapatika kwa misimu kwenye hifadhi ya Mafia . Ndiyo maana hifadhi hii ya bahari ni muhimu kwa taifa na duniani pia.” Anaeleza.

Anasema kitaaluma wasomi na watafiti wanatumia hifadhi hii kujifunza masuala ya bayoanuai za bahari na kuchangia elimu na utaalamu zaidi wa kuendeleza sayansi za viumbe bahari.

Aidha, Dk Kamukuru anasema kuwa Kisiwa cha Mafia kinachangia kiwango kikubwa cha samaki wanaouzwa soko la Ferry jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa wataalii ni sehemu inayofikiwa na watalii wanaozuru viumbe adimu vya bahari, kuogelea na kuangalia papa potwe ‘whaleshark,’ kuvua na kwa ujumla ni eneo linalovutia wageni, watafiti na wawekezaji.

HIFADHI D’SALAAM

Dar es Salaam nayo ina hifadhi za Bahari za Dar es Salaam (DMRS) zinahusisha visiwa saba vya Bongoyo, Pangavini, Fungu Yasin, Mbudya Sinda, Makatobe na Kendwa.

Kwa mujibu wa mtandao hifadhi hizo zina sifa lukuki mojawapo ni uwapo wa ndege weupe wanaoonekana sehemu mbalimbali jijini, mwambao na ndani ya bahari.

Ndege hao mara nyingi jioni hurejea kwenye viota vyake visiwani humo.

Kwenye visiwa ndiko yaliko makazi na mazalia ya ndege hao wenye rangi nyeupe na shingo ndefu zenye ufito mweusi unaoambaa hadi kichwani.

Ndege hawa wakati mwingine huruka kwa makundi juu ya bahari na wanaweza kutumiwa na wavuvi kuainisha sehemu yenye samaki wengi.

Aidha, kuna viumbe bahari kama kaa maarufu kama ‘coconut crab’, ambaye hujishikiza kwenye minazi, aidha wapo kasa na mimea mingi inayopatikana mahsusi maeneo eneo hayo licha ya kwamba ni sehemu zenye hoteli na miundombinu ya kuvutia watalii.

Kwa ujumla hifadhi za Dar es Salaam zinafikika lakini za Mafia licha ya uzuri wa kipekee zina changamoto ya usafiri.

Mafia kuna vivutio vya kipekee na hifadhi bahari hiyo inayotembelewa pengine kuliko za Dar es Salaam kwa miaka mingi haifikiki kwa urahisi kwa vile hakuna boti ya uhakika ya kuwafikisha watalii na wasafiri wengine kisiwani humo.

Njia pekee ya kufika Mafia ni kwa kutumia ndege ambazo wakati mwingine ni za kukodi, hivyo uzuri wa eneo hilo unabakia kusikika zaidi kuliko kuonekana hasa kwa wasioweza kumudu gharama.

Licha ya kuwapo wanyama na viumbe bahari wa kipekee ni sehemu yenye nazi nyingi zenye ladha ya mujarabu , na samaki wengi wakubwa, pweza, ngisi na kamba wakiwamo koche (lobsters) na ‘prons’ hata hivyo licha ya kufikishwa Dar es Salaam na mikoani bei zake ni kubwa kutokana na gharama za usafiri inayochangiwa na ukosefu wa miundombinu hasa meli na barabara.

Wakazi wa Mafia wanatumia mitumbwi na majahazi kusafiri kutoka kisiwa kimoja kwenye kingine.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Mafia Shaibu Nnunduma, tatizo la usafiri linaelekea kufikia ukingoni wakati wowote kuanzia sasa.

Akirejea ahadi ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, ambaye mwishoni mwa mwaka jana alitangaza kuwa wilaya hiyo Februari mwaka huu ingepata meli anasema usafiri utakuwa wa uhakika.

Anasema meli hiyo itasafirisha abiria na shehena kutoka bandari ya Nyamisati iliyoko wilayani Kibiti hadi kisiwani Mafia.

Abiria wakifika Nyamisati watasafiri maeneo mengine kwa kutumia barabara inayoelekea mikoa ya Lindi na Mtwara
Nnunduma anaeleza kuwa jitihada zinaendelea na meli hiyo huenda ikiaanza kazi wakati wowote mwezi huu.

Habari Kubwa