Kasi shinikizo damu, miaka mitano ongezeko ni mara mbili ya zamani

25May 2023
Yasmine Protace
DODOMA
Nipashe
Kasi shinikizo damu, miaka mitano ongezeko ni mara mbili ya zamani

MAGONJWA yasiyoambukiza, sasa yanasumbua rika zote, kukitajwa shida kama za kansa, kifafa, moyo, kisukari, pumu na presha.

Waziri Ummy Mwalimu, akifanya vipimo katika maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu, Jijini Dodoma. PICHA: YASMINEM PR0TACE.

Ni magonjwa yanayochangiwa na mfumo wa mlo na kuna wengine wanayarithi katika uhusiano kimaumbile. Kwenye mlo kunatajwa vyakula vyenye mafuta mengi, mwili kutofanya mazoezi na wengine inatokana na uzito uliokithiri.

Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa jamii jinsi ya kujilinda dhidi ya magonjwa hayo na mtu anapochelewa kupata matibabu, huweza kumletea ulemavu au kupoteza maisha kwa kutegemea ukubwa wake.

Hicho huifanya jamii iwajibike kujenga utaratibu wa kuchunguza afya zao na wanapobainika kuwa na magonjwa yasiyoambukiza, iwe rahisi kupata matibabu haraka.

Ni hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema shinikizo la juu la damu wagonjwa wake wameongezeka kutoka 688,901 nchini mwaka 2017 hadi 1,345,847 mwaka 2021, sawa na ongezeko asilimia 95.4 katika miaka mitano.

Waziri Ummy anatamka hayo jijini Dodoma, katika maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani, akifafanua: “Takwimu hizi zinatuonyesha kwamba wagonjwa hawa wenye shinikizo la damu wameonekana kuongezeka takribani mara mbili zaidi kwa kipindi cha miaka mitano.”

Ummy anafafanua, magonjwa yasiyoambukizwa yameongezeka kwa asilimia 9.4 na kwa miaka iliyopita 2017 hadi 2021 kwenye vituo vya afya nchini. Wagonjwa hao wameongezeka hadi kufikia 3,440,708 kwa mwaka 2021.

Anafafanua, takwimu zinaonyesha watu watatu hadi wanne kati ya 10, wana shinikizo la juu la damu, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa kwenye mikoa ya Pwani, Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Zanzibar, Iringa na Dar es Salaam.

Waziri Ummy anataja mikakati ya kutatua, wizara imeruhusu dawa za kukabili shinikizo la juu la damu katika ngazi ya msingi kuruhusiwa dawa mpya aina tatu, akizitaja ni; Losartan, Amlodipine na Hydralazine, zitumike katika kituo cha afya na dawa mbili; Nifedipine na Frusemide, kutumika zahanati.

"Mpango wa serikali kupitia Wizara ya Afya, ni kutoa mafunzo ya utoaji huduma za magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo huduma za ugonjwa wa shinikizo la damu, kwa watoa huduma 2400 kutoka vituo vya afya vyote 600 katika mikoa yote 26," anasema.

Anataja aina mbili za shinikizo la juu la damu, la asili, pia linalosababishwa na magonjwa mengine. Hapo anaeleza: “Inakadiriwa asilimia 90 hadi 95 za watu wanaathiriwa na shinikizo la juu la damu la asili, yaani wana ugonjwa huu bila kuwa na chanzo cha kisayansi kinachofahamika.”

Anasema shinikizo la juu la damu linalosababishwa na magonjwa mengine hutokana na magonjwa ya figo, mapafu, mfumo wa homoni huathiri asilimia tano hadi 10 na iliyobaki ya watu wenye shinikizo la juu la damu.

Waziri Ummy anawakumbusha Watanzania, umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha, kwa kuzingatia mazoezi, kuepuka tabia bwete, kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake na kupunguza vilevi.

“Tuzingatie ulaji unaofaa wa mlo kamili wenye mboga mboga na matunda ya kutosha ili kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa, kupunguza matumizi ya chumvi, sukari na vyakula venye mafuta mengi, pamoja na kuzingatia unywaji wa maji ya kutosha angalau kiasi cha lita 1.5 ya maji kwa siku.” anashauri.

 

 

 

 

 

Bottom of Form