Katiba inayopendekezwa ina umuhimu wake

28Jun 2017
Sabato Kasika
Dar es salaam
Nipashe
Katiba inayopendekezwa ina umuhimu wake

MIEZI ya hivi karibuni Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilifanya mabadiliko ya Katiba yake kwa lengo la kuwa na CCM mpya na Tanzania mpya, ambayo haina uozo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Katika mabadiliko hayo CCM ilifuta baadhi ya vyeo, ikapunguza idadi ya wajumbe katika vikao vyake na mambo mengine, ambayo yalibainika kuwa hayana faida kwa chama hicho tawala.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa walibeza hatua hiyo wakidai kuwa uozo uliojaa katika Katiba inayotumika kuendesha nchi ni ndoto ya mchana kuipata Tanzania mpya kwa kutumia Katiba ya CCM.

Wakadai kuwa mabadiliko yanayotakiwa ni kuwa na Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maana ya kuruhusu mchakato wa Katiba inayopendekezwa ili ipigiwe kura.

Binafsi ninakubaliana nao kidogo halafu ninatofautiana nao pia kwani ninaamini kwamba kilichofanywa na CCM ni kujisafisha chenyewe kwanza ndipo kitoke nje kwa ajili ya mambo mengine ya msingi kwa taifa, likiwamo hilo la mchakato wa Katiba inayopendekezwa.

Ikumbukwe kuwa mabadiliko ya Katiba ya CCM yanaweza kuwa ni mwendelezo wa kuwapo kwa kasi ya kusukuma mbele mchakato wa kurejesha mezani Katiba inayopendekezwa ili iweze kupigiwa kura.

Hivyo, siyo rahisi CCM ambayo ni chama tawala kusimamia Katiba mpya wakati ikiwa na makandokando, ndio maana mchakato wa mabadiliko umeanzia ndani ya chama hicho na unaweza kuja hata kwenye Katiba inayopendekezwa.

Kwa namna nyingine ni kwamba mabadiliko kama hayo yasiishie ndani ya chama tu bali wayavushe hadi kwa Watanzania wote ili Katiba iliyopendekezwa na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ipigiwe kura.

Ninasema hivyo kwa sababu tayari Rais John Mafuguli alishatoa msimamo wake kuwa anataka anyooshe nchi kwanza ndipo suala la Katiba inayopendekezwa lifuate baadaye, lakini hatua hiyo inapingwa na wanasiasa.

Miongoni mwao ni Tundu Lissu ambaye anaamini kuwa hawezi kunyoosha nchi bila kuwa na Katiba mpya, kwa madai kwamba ile iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikuwa ni kiboko ya mafisadi.

Anaamini kuwa Katiba ya sasa imekuwa ikitumiwa na wajanja kama kichaka cha kujificha na kufanya mambo yao wanavyokata bila woga, hivyo ili rais aweze kufanikiwa malengo yake hana budi kuhakikisha analeta Katiba inayopendekezwa.

Wanasiasa hasa wa upinzani wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kunyoosha nchi huku kukiwa na Katiba inayoendana na wakati huu kwa vile ndio dira na sheria mama na ni msingi na muhimili mkubwa wa sheria za nchi.

Lakini kikubwa zaidi ninachoamini ni kwamba mabadiliko yaliyofanyika ndani ya CCM huenda yakawa ni mwendelezo wa rais wa kuwarejesha Watanzania kwenye Katiba inayopendekezwa.

Kwani kama imewezekana ndani ya CCM, itashindikana vipi kwenye Katiba ya nchi?

Binafsi ninamini kwamba CCM mpya chini ya mwenyekiti wake wa taifa, Rais Magufuli itasaidia kumshauri aangalie uwezekano wa kurejesha mezani mchakato wa Katiba inayopendekezwa ili ipigiwe kura na Watanzania.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilikuwa imeshasema kuwa baada ya Katiba inayopendekezwa kupigiwa kura na Bunge Maalum la Katiba hatua iliyokuwa inafuata ni kuitisha kura ya maoni, lakini ilishindikana baada ya kuingiliana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Hata hivyo, wakati anatimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani, Rais Magufuli alitoa msimamo wake kuhusu Katiba inayopendekezwa na kusema kuwa anataka aachwe anyooshe nchi kwanza ndipo suala hilo litafuata baadaye.

Historia inaonyesha kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 ilitokana na Tume ya Rais iliyokuwa na wajumbe 20 kutoka upande wa Muungano, ikiongozwa na Sheikh Thabit Kombo na katibu wake akiwa Pius Msekwa.

Kwa mujibu wa historia, tume hiyo ilianza kwa kutunga Katiba ya CCM, ambayo ilizaliwa baada ya kuungana kwa vyama vya siasa vya ASP na TANU, Februari 5 mwaka 1977.

Inaelezwa kuwa Tanzania haijawahi kuwa na Katiba yenye maoni ya wananchi na kwamba iliyopo haikuwahusisha bali ilihusisha viongozi wachache, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na Katiba inayotokana na matakwa ya wananchi itakayoendana na wakati uliopo.

Wakati huu ambao Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo imefanyiwa marekebisho zaidi ya mara 10, ni vyema kuangalia uwezekano wa kuwapo kwa mchakato wa kupigia kura Katiba inayopendekezwa.

Kwanza wataalamu wa sheria wanaweka wazi kuwa Katiba ni mwongozo wa kisheria wa nchi, chama, kikundi, familia au jamii fulani na ni lazima ikubalike na kuheshimiwa na watu ambao inawaongoza.

Hata mtu binafsi anahitaji kuwa na katiba yake kama mwongozo wa maisha yake na kwamba katika nchi yoyote msingi wa uendeshaji wa nchi unategemea Katiba.

Katiba ni sheria kuu au sheria mama katika nchi yoyote na pia sheria nyingine zote zinategemea au zinatungwa kwa mujibu wa katiba.

Mtaalamu wa sheria Profesa Issa Shivji alishawahi kutoa ufafanuzi kuhusu Katiba kuwa hutafsiriwa kama mkataba wa kijamii kati ya watawala na watawaliwa, kwa maana ya makubaliano ya wananchi husika.

Makubaliano juu ya jinsi taratibu na kanuni za uendeshaji wa mambo mbalimbali katika nchi yao unapaswa kuwa.

Na pia ni mwafaka wa kitaifa juu ya misingi mikuu ya kuendesha nchi.

Habari Kubwa