Kauli hizi zizingatiwe kufanikisha uchaguzi wa serikali za mitaa 2019

16Jan 2019
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Kauli hizi zizingatiwe kufanikisha uchaguzi wa serikali za mitaa 2019

DESEMBA 14, 2014 Watanzania walipiga kura kuchagua viongozi wao wa serikali za vitongoji, vijiji, mitaa na wajumbe sita wa serikali ya mtaa na wajumbe wa viti maalum wa mitaa na vijiji.

Makamu wa rais, Samia Suluhu Hassan.PICHA: MTANDAO

Uchaguzi huo ulifanyika huku ukigubikwa na changamoto mbalimbali zilizosababisha kuahirishwa kwenye baadhi ya vijiji na mitaa.

Miongoni mwa changamoto hizo zilikuwa ni za baadhi ya vifaa kutopatikana ndani ya muda kwenye vituo vya kupigia kura, lakini pia karatasi za kupigia kuwa chache kuliko idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura.

Baada ya miaka mitano kupita, sasa utafanyika mwingine mwaka huu wa 2019, na kisha kufuatiwa na Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba mwakani.

Kama ilivyo kwa uchaguzi mkuu, huu wa serikali za mitaa nao hufanyika kila baada ya miaka mitano kupita, ambapo mara ya mwisho ulifanyika Desemba mwaka 2014.

Sasa nchi inaingia tena katika uchaguzi mwingine wa serikali mitaa huku kukiwa na kilio cha wadau wa siasa cha kudai tume huru ya uchaguzi, ambapo Watanzania bila kujali itikadi za kisiasa wamekuwa wakiombwa kupaza sauti kudai tume hiyo huru.

Lengo la kutaka tume huru ni ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki. Wadau hao wanaamini kwamba kushiriki uchaguzi chini ya tume ya sasa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.

Hayo ni miongoni mwa malalamiko, ambayo yamekuwapo kwa muda mrefu tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, pamoja na mengi mengineyo kutoka vyama vya upinzani.

Lakini pamoja na mapungufu hayo yanayotajwa, bado upinzani umeweza kupenya kwa kupata ushindi katika nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na hata katika uchaguzi mkuu.

Nimegusia hayo kidogo lakini lengo langu ni kutaka kuzungumzia kile ambacho kimewahi kusemwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu, ambacho ninaamini kina uzito mkubwa.

Kauli za viongozi hawa, ambazo wamewahi kuzitoa kwa nyakati tofauti, zinalenga kuwafanya Watanzania kuchagua viongozi bora wenye uwezo wa kusaidia kusukuma mbele maendeleo ya nchi na si bora viongozi.

Mbali na viongozi hao, Rais John Magufuli naye anatia neno kwa ajili ya uchaguzi huo, lengo ni kutaka kuhakikisha unafanyika kwa amani.

KAULI YA MAKAMU WA RAIS

Kuelekea kwenye uchaguzi unaofanyika mwaka huu, Samia anawataka Watanzania kuchagua viongozi walio wepesi wa kufuatilia maendeleo na kwenda mbio na siyo ‘mazezeta na mananga.’

Makamu wa Rais anaamini kwamba njia hiyo itasaidia kuepuka kuchagua watu wazito, wezi na mafisadi na badala yake viongozi watakaojenga nchi.

“Mkichagua viongozi wazuri wataondosha kasoro zilizopo haraka lakini mkichagua wazito, hapa watazama tuu chini kunyanyuka hawanyanyuki, kutembea hawatembei,” anasema na kuongeza:

“Wanasema mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe, mimi nikija ninaona kasoro zilizopo nitakwambieni kuna kasoro, lakini warekebishaji ni ninyi na viongozi mtakaowachagua.”

Kauli hii ya Makamu wa rais ni ya Oktoba mwaka jana wakati akihitimisha ziara yake ya siku sita katika mkoa wa Pwani, ambapo aliwataka Watanzania kuzingatia hayo katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu.

KATIBU MKUU WA CCM

Mwishoni mwa Desemba mwaka jana, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Ally alikutana na wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya za Muleba na Biharamulo mkoani Kagera na kuwapa maelekezo kuhusu uchaguzi huo.

Anasema mwana CCM atakayejihusisha na vitendo vya rushwa katika mchakato wa chama hicho wa kusaka wagombea kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, atapoteza sifa za kugombea.

“Makatibu wa CCM kila ngazi hata nyie msiwe wa kupokea rushwa wala kupitisha majina ya wagombea wasiokuwa na sifa, lazima kiongozi afuate miiko na ahadi za mwanachama,” anasema.

Anabainisha kuwa kila mwana CCM atakayejitokeza kugombea uenyekiti wa kijiji au mtaa, lazima awe mwaminifu na mwadilifu.

Anafafanua kuwa baadhi ya wagombea hutumia majukwaa kupinga rushwa licha ya kuwa wanajihusisha nayo, ikiwa ni pamoja na kukiuka maadili ndani ya chama.

RAIS JOHN MAGUFULI NA AMANI

Desemba 21 mwaka jana, Rais Magufuli aliliagiza Jeshi la Polisi kuimarisha nidhamu kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu wa 2019.

Alikuwa katika mahafali ya kuhitimisha mafunzo ya Maofisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi, na kusema kuwa kuna baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakilituhumu jeshi hilo kwa vitu ambavyo si vya kweli.

“Mwaka 2019, tunaingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa, nawaomba Jeshi la Polisi mkasimamie nidhamu. Watu wasiokuwa na shukrani ndio watawasema vibaya,” anasema na kuongeza:

“Lakini sisi tunaotambua na kuthamini mchango wenu katika ulinzi wa taifa hili, tunatembea kifua mbele... huu ni ukweli usiofichika kuwa jeshi la polisi mnafanya kazi nzuri.”

Habari Kubwa