KAWA: Mubashara wa huba, mahaba na mipasho!

11Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
KAWA: Mubashara wa huba, mahaba na mipasho!

KAWA ni pambo la kifahari linalopendwa kutumiwa katika maeneo ya ukanda wa pwani.

Matumizi ya pambo hili ni pamoja na kupamba nyumba kwa kuweka ukutani,kufunika na kuhifadhi chakula kikishapakuliwa, kiendelee kuwa cha moto.

Lakini raha ya kawa ni ujumbe wa maneno na maua yanayochorwa, kwani wengi pambo hilo, huwasilisha hisia zao kwa wapenzi wao au jamii inayowazunguka.

Kwa mfano, mke anapomuandalia mume wake chakula, anaweza kufunika kawa lenye ujumbe “Kula bwana, ufurahie mapenzi”, “Ndoa ni heshima na uvumilivu” au “Nimekupata sitamani kukupoteza.”

Kwa wale wanaopenda ujumbe wa mafunzo utakuta kawa limeandikwa “Sili kwako, maneno mengi ya nini?, “Wastara moyo wangu, uvumilivu dira yangu,” au “Mmenitafuta hamnipati, ya undani hamuyapati”

Wakazi wa pwani hasa mikoa ya Pwani, Zanzibar, Dare s Salaam na Tanga huvutika zaidi pambo hili na wanaona stara kufunika misosi,

Mgeni anapoingia kwenye nyumba hawezi kujua nini kimehifadhiwa ndani ya kawa kiwe pilau, chapati, mkate, ugali au wali, kinachogonga kwenye akili yake ni kwamba juu ya meza kuna ‘mpunga’ umeandaliwa kwa ajili yake.

Visiwani Zanzibar kwa muda mrefu kawa zinatumika mjini na vijijini ikiwa ni kama ni sehemu ya vyombo vya nyumbani kama zilivyo nyungo, vikapu na masinia.

Kwa upande mwingine mbali na kuhifadhia chakula, zinatumiwa kupamba nyumba na sehemu za biashara zikinin’ginizwa ukutani na wapo wanaozitumia kusutana na kurushana roho.

Maneno yanayoandikwa ndani ya kawa hizo yanakuwa na ujumbe kama kwenye kanga hivi hutoa fursa ya kupashana habari.

Kwa ujumla baada ya mabadiliko ya teknolojia dunia vitu vingi vya asili vimekuwa havina kipaumbele badala yake jamii huvutiwa na mambo ya kisasa zaidi kuanzia mapambo hadi vyombo vya ndani.

Kwa mfano kuna baadhi ya vyombo vya asili kama vyungu, mtungi, kata, mkungu wa tano na mkeka hivyo ni miongonii vya vitu asilia ambapo kwa kiasi kikubwa hivi sasa vimeachwa.

Afrika mashariki ni eneo lenye mapambo mengi ya asilia, hivyo ni wakati wa kuhimiza matumizi ya vitu vya asili kwa kila nchi mwanachama kwani kuna upungufu mkubwa wa utumiaji wa rasilimali hizo.

Nchi za Kenya,Uganda,Burundi,Rwanda na Tanzania kawa zimetumika kwa shughuli mbalimbali.

Kwa upande wa visiwa vya Zanzibar ambavyo vimezungukwa na bahari imelazimika kutumia kawa kwa sababu mbalimbali ambazo waliona kifaa hicho kitasaidia kutunza chakula.

Leo kawa inaelekea kuwa historia inapotea, hii inaonyesha wazi kuwa jamii imekosa ufahamu wa umuhimu wa kutumia vifaa hivyo vya asili na kusababisha kizazi kijacho kukosa kuvijua.

Hii si habari njema kwa vifaa vya asili ambavyo ndiyo utamaduni, huenda mambo yakabadilika ikasababisha vijana wa sasa na wa vizazi vijavyo kushindwa kufahamu matumizi ya vitu hivyo.

Lakini watengenezaji wa vitu vya kitamaduni watakwama kuendeleza utamaduni huo, mfano kufinyanga, ususi, uchoraji na uchongaji.

Utamaduni ni pamoja na mambo ya asili ukiwamo sanaa za ususi ukihusisha kawa na mara nyingi utengenezaji wake ni kazi za mikono ya wanawake wajasiriamali na malighafi ya bidhaa hizi ni jamii za ukindu.

Matumizi ya kawa pamoja na vitu vyigine vya asili yangeendelezwa bila shaka ajira zingepatikana kupitia kazi hizo na soko la utalii lingekuwa na kuipa Tanzania heshima kwenye bidhaa za ususi, ushonaji, usokotaji na uchongaji wa vitu mbalimbali vinavyofanywa na kinamama.

Hii ni njia ya kujikomboa kiuchumi na kiutamaduni.

Wanawake hususan wa Zanzibar kwa asilimia kubwa hujishughulisha na kazi za mikono, ikiwamo ushonaji, ususi, ufinyanzi na ufumaji. Hata hivyo, kazi hizo zimekosa muendelezo na husababisha kinamama hao kukata tamaa.

Inaelezwa kuwa zipo sababu mbalimbali za kurudi nyuma katika harakati hizo kutokana ukosefu wa soko la bidhaa hizo.

Utamaduni uliozoeleka kwa makabila mengi ambao pia unaurithishwa kutoka kwa mabibi na mababu, mwanamke anapoolewa anapewa vitu ambavyo huenda navyo nyumbani kwake kuanza maisha mapya kwa matumizi ya nyumbani.

Huku Zanzibar kawa hazikosekani kama ambavyo wengine hupewa miko, ungo na vikapu vya vyakula, lakini hivi sasa utamaduni huo unaondoka.

Asilimia kubwa ya wanawake wanaolewa hivi sasa huwa hawana vyombo vya asili kama kawa, badala yake huwa na vitu vya kisasa mfano seti vya vyombo kama sufuria, vizuia joto ‘hotipoti’ , bakuli kubwa na ndogo, mabeseni na vyombo vingine ambavyo malighafi yake ni plastiki, vigae au bati.

Vyombo hivyo vina nafasi yake kulingana na nyakati lakini ni vyema pia kuwa na vifaa vya asili.

Japo kawa inaweza kuonekana pengine si ya thamani, lakini ina mvuto kwa mlaji kuwa na hamu ya kufunua ili ajue kilichomo chini ya hifadhi hiyo.

Rangi za kili aina na maneno ya kuvutia yaliyozinakishi na ususi humshawishi mtu kuyasoma na hata kumpa ujumbe wa kumkaribisha na kumkirimu.

Anapokula hupenda kuufunua na kuuzungusha ili kufurahia na kugundua ujumbe mubashara anaokutana nao.

Kwenye ‘hotpoti’ hakuna mwaliko wala mfuniko haukusemeshi unapokula jamani.

Chombo kama ‘hotpot’ hakiwezi kuwa na sifa za aina hiyo.

Kwanza kawa hauvunjiki hata ikianguka, hauchafuki ili kila mara upate kuoshwa lakini pia unapendeza kwa kumwalika mlaji kwa maneno matamu.

Kina mama wasusi wana kila sababu ya kuendelea na sanaa ya utengenezaji makawa na vitu vya asili ili kudumisha utamaduni.

Lakini pia,kama taifa linahitaji msuko wa kuhimiza matumizia ya bidhaa za asili na kudumisha utamaduni wa Mtanzania.

Habari Kubwa