Kazini Rashid Kawawa na nyumbani mpinzani wa bao, Mzee Nyang’ombe

14Oct 2021
Peter Orwa
Dar es Salaam
Nipashe
Kazini Rashid Kawawa na nyumbani mpinzani wa bao, Mzee Nyang’ombe

NAAM, kilele cha miongo miwili na ushee kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, kila mahali ni maadhimisho ya kitaifa.

Rais Julius Nyerere (kulia) alipoongozana na viongozi wenzake wa awamu ya kwanza, akiwamo Waziri Mkuu, Rashid Mkuu Rashid Kawawa, (watatu kutoka kulia). PICHA: MTANDAO

Ni wiki hiyo yote kuna mengi yanazungumzwa kuhusu maisha yake na miaka mingi ameendelea kujadiliwa kuhusu maisha yake.

Nyerere amekuwa na wasifu mmoja kwamba, licha ya kuwa na wadhifa wa juu kimataifa, lakini marafiki na mfumo wake maisha amekuwa akiishi wa kawaida zaidi. Eneo mojawapo ni marafiki aliyokuwa nao.

Kimsingi, falsafa na maisha yake binfasi yaliangukia kwenye itikadi ya Ujamaa na falsafa yake ya kuishi katika hulka ya Kiafrika na kupenda haki. Historia ya maisha yake inaonyesha hakuwahi kutoka nje ya mstari huo.

Kama binadamu yeyote, alikuwa na marafiki alioshirikiana nao. Katika mtazamo wa tafsiri ya maisha yake marafiki wengi waliangukia maisha ya kawaida mno, katika makundi makuu matatu: Ofisini na kisiasa: aliyoishi nao nyumbani; na kutoka jumuiya mbalimbali za kijamii kama vile makanisani.

Historia yake mwalimu inamwonyesha katika kila kundi la marafiki, aliishi nao kwa namna yao, kadri ya mahitaji yalivyokuwapo.

Kuna jambo la kipekee jamii nyingi zikiwamo waliokuwa watoto tangu zama hizo walidiriki kufananisha urafiki kwa mfano wa ‘Nyerere na (Rashidi) Kawawa.’

Hata ikakumbukwa, kuna wakati Mwalimu Nyerere, alipopewa kauli ambayo hakufurahia kutoka kwa mwanasiasa wa upinzani, dhidi yake na Kawawa, alionyesha kugadhabika akitishia kumshtaki kwamba kilichomuudhi sana ni hatua kumdhihaki Rashidi, kwa maana ya Kawawa ilimkera sana, huku kejeli kwake aliziita ‘ni upuuzi tu’.

Ni jambo lililozua swali kubwa kutoka kwa umma, ni kiasi gani anamthamini Mzee Kawawa ambaye haijawahi kutokea historia yake ya madarakani zaidi ya miaka 30 kabla na baada ya uhuru, ndani ya TANU na serikali hawakukwazana.

Mwandishi wa makala katika faragha na Mzee Kawawa nyumbani kwake Madale, Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kifo cha Baba wa Taifa, kwanza hakuficha urafiki wao wa ‘damudamu.’

Kawawa anasema binafsi aliguswa na Nyerere akiwa Mwalimu na yeye mwanafunzi, pale Baba wa Taifa alipoandamana na mwalimu mwenzake (Balozi) Tibandebage kusimamia mjadala wa wanafunzi (debate).

Kawawa anasema, alikoshwa na stadi zao za lugha na hasa kutoka kwa Nyerere, kuanzia sauti, ubora wa lugha na alivyojenga hoja zake, bila Nyerere kujua.

Baada ya kuhitimu masomo, Kawawa alijikita katika harakati za haki za wafanyakazi akiwa katika iliyokuwa Shirikishi la Wafanyakazi wakati huo TFL. Kazi nzuri ya kuitikisa serikali ya mkoloni nayo ikamgusa Mwalimu Nyerere wakati huo mwaka 1955 akiwa amejikita katika harakati za TANU.

Nyerere aliiomba faragha naye washirikiane katika harakati na daima waliungana kuwa maswahiba wa kikazi hadi majumbani hadi kuzikana.

Palishuhudiwa hata kimataifa, hasa katika zama za miaka ya 1970, Tanzania ikiwa na urafiki wa juu na China wakati Nyerere alikuwa karibu sana na Rais Mao Tse Tung, Kawawa alikuwa sambamba na Waziri Mkuu mwenzake, Chuo Enlai, hata wakafika kuvaa aina ya mashati waliopenda yasiyo na kola, maarufu ‘Chuoenlai.’

Mjane wa Mwalimu Nyerere, anaifafanulia Nipashe kijijini Butiama mwaka mmoja baada ya kukutana na Kawawa, akisema hata kuwa watoto wengi kutoka familia ya Kawawa kufika katika maziko ya Baba wa Taifa kijijini Butiama, ni kwamba walimtafsiri ni baba yao, kwa maana ya uhusiano wa karibu kifamilia na waliishawahi kuishi majirani.

MZEE NYANG’OMBE

Unapofika kijijini Muryaza, umbali wa kilomita saba Kaskazini Mashariki ya Butiama, penye barabara kuu iendayo Ikizu kutoka Nyamuswa, alikuwapo Mzee Nyangombe Warioba, ambaye sasa ni marehemu.

Akiwa na umri tofauti ya miaka saba mdogo kwa Nyerere, Mzee Nyango’mbe alitokea kuwa rafiki wa karibu mno wa Mwalimu Nyerere, tangu utoto wao na ukachukua wastani wa miaka 70.

Moja ya sifa za urafiki wao, ulikokuwa katika mchezo wa bao (soma ukurasa 14) wakibishana sana. Hata katika maisha yake, Mzee Nyang’ombe alimfahamu vyema Nyerere kitabia, mlo na hata kumuiga sauti kwa ufasaha, iwe katika hali ya tabasamu hata kukasirika, alikuwa mithili ya ‘google’ inayomhusu Nyerere.

Anasimulia kwamba, hata mara moja hawakuwahi kuweka urafiki wao katika siasa, lakini ‘walishibana’ na Mwalimu kuna wakati akimwandalia usafiri kutoka kijijini kwake hadi Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Nyangombe, pindi alipofika Dar es Salaam alipatia heshima zote za mgeni rasmi wa kifamilia, akikaa Ikulu na Mwalimu katika makazi yake Msasani.

Hata hivyo, anasema kila ilipofika jioni, alituma usafiri kwenda Msasani ambako waliongea na kubishana katika mchezo mpaka usiku sana.

Anasimulia, licha ya Nyerere kumjengea nyumba kijijini kwake Muryaza, kazi walipewa Jeshi la Magereza baada ya kustaafu muda wote Nyerere alimhamisha rafiki yake huyo kukaa naye Butiama.

Alipata nafasi kurudi kwake Muryaza, pindi tu Mwalimu amesafiri na anapotua kijijini Butiama, alituma gari kumpeleka Butiama, ambako walichuana sana katika mchezo bao.

Pia lingine walikuwa na shamba la pamoja, walilima huku wakipeana michapo shambani wakarudi kula pamoja na mapumziko jioni wako wote katika bao.

Pia Nyang’ombe anamtaja mtumishi wa nyumbani Butiama, ambaye alikuwa kijana pia, alikuwa rafikiye mkubwa Mwalimu wa Katibu.

Anakumbuka hata wakati dakika chache kabla hajaanza safari ya kwenda kutibiwa Uingereza, Baba wa Taifa alimnong’oneza kuna jambo anataka kumwambia pindi angerudi tu, lakini halikutimia, alifariki.