Kenya inaposhtukia sasa corona Tanzania iliIng’amua mapema

04Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Kenya inaposhtukia sasa corona Tanzania iliIng’amua mapema

NCHI ya Kenya imekuwa katika taharuki kubwa tangu kutangazwa kwa kisa cha kwanza cha Covid-19 mwezi Machi, mwaka huu.

Baadhi ya malori yakiwa yamesongamana mpakani wakati wa mapambano ya corona

Serikali ya nchi hiyo, imechukua hatua kali katika kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona, ikiwamo kuweka sheria ya kutotoka nje kwa baadhi ya maeneo, kuendesha upimaji wa nyumba kwa nyumba na kufunga mipaka yake kwa baadhi ya nchi jirani.

Katika kutekeleza hatua hizo, mara kadhaa kumeibuka migogoro ya mipaka kati ya Tanzania na Kenya, baada ya kuwazuia madereva kutoka Tanzania kwa kuhofia kusambaza ugonjwa huo.

Mgogoro huo uliposhika kasi, viongozi wakuu wa pande mbili, yaani Rais Dk. John Magufuli wa Tanzania na mwenzake wa Kenya, Uhuru Kenyatta, waliingilia kati kwa kutaka kuwapo na utulivu, huku utaratibu rafiki ukiandaliwa kwa ajili ya kuvusha bidhaa kutoka kila upande.

Hata hivyo, bado kulikuwapo na malalamiko  ya uonevu  kwa madereva kutoka Tanzania, ambao walilazimishwa kupimwa corona licha ya kuwa na vyeti vinavyoonyesha tayari wamepimwa na kuonekana hawana virusi vya corona.

Pamoja na mvutano huo, Tanzania, iliendelea kushikilia msimamo wake, kwamba haitafunga mipaka yake wala kuweka sheria za kuwazuia ndani watu kama njia ya kupambana na Covid 19, kwa sababu ugonjwa huo upo kwenye jamii na utaendelea kuwapo kwa muda mrefu.

Katika hotuba zake tofauti, Rais Magufuli, alisisitiza hawezi kuzuia shughuli za uchumi, akisema njia hiyo sio suluhu ya kupambana na virusi vya corona.

Mara kadhaa, Rais Magufuli, aliwatoa hofu wananchi na kuwahimiza wachape kazi mara dufu kwani virusi hivyo ni sehemu ya maisha ya kila siku, hivyo kumuamini Mungu na kufuata kanuni za afya ndio suluhu.

 

WAKENYA WENGI WANA CORONA

Pamoja na kuchukua hatua kali, ripoti mpya inaonyesha Wakenya milioni 2.6 tayari wana virusi vya corona, baada ya kupima damu zao.

Kulingana na ripoti hiyo,  wanasayansi wamegundua hilo baada ya kupima damu iliyotolewa kwa ajili ya protini inayotumika kwenye mfumo kinga.

Protini hiyo (antibody) hutengenezwa na mwili kwa ajili ya kushambulia virusi na bakteria, na uwepo wake kwenye damu unaashiria kuwa mtu huyo hakuwahi kuwa na maambukizi.

Watafiti kutoka Taasisi ya utafiti wa tiba ya nchi hiyo, (kemri) wamechunguza sampuli za damu kutoka kwa watu waliochangia damu katika kampeni iliyofanyika nchi nzima kati ya miezi ya Aprili na Mei.

''Kupimwa kwa antibodies kumeonyesha kuwa Wakenya wengi tayari wamepata maambukizi, kuliko ilivyokuwa ikigundulika katika upimaji nchini humo,'' ulieleza utafiti huo.

Unaeleza baadhi ya watu inawezekana waliathirika mapema mwezi Machi, kutokana na protini hizo zinazopambana na virusi zinaweza kuwa kwenye damu kwa miezi kadhaa.

Kemri inakadiria kuwa karibu watu 550,000 jijini Nairobi na karibu 100,000 mjini Mombasa, tayari wameugua virusi hivyo na kupona na pengine kupata kinga.

Idadi hiyo inaonesha kuwa Wakenya wameshuhudia idadi kubwa ya watu waliopata maambukizi pamoja na vifo.

Taasisi hiyo ya utafiti ikikisia kuwa takriban watu 6,000 watakuwa wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Covid-19 katika nchi hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la The Standard media, sehemu ya ripoti ya taasisi ya Kemri ilisomeka kuwa katika mji kama Nairobi, idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa wakati utafiti ulipokuwa ukifanyika ni 2,732 ikilinganishwa na idadi ya 550,000 wanaokisiwa kuwa na maambukizi. Mombasa  katika takwimu ya sasa inaonyesha ni watu 1,368 waliopata Covid-19, lakini watu 100,000 wanakisiwa kuwa na maambukizi kutokana na utafiti huo.

''Namna nzuri ya kupima ili kujua walioambukizwa miongoni mwa raia wa Kenya ni kutembelea maeneo ya makazi kwa ajili ya kukusanya na kupima sampuli za damu''. Inaongeza kusema taarifa hiyo.

Hata hivyo, upimaji wa aina hiyo haujaleta matokeo mazuri kwasababu ya masharti yaliyopo kutokana na hali ilivyo hivi sasa.

Mkurugenzi wa masomo ya sayansi na teknolojia kutoka Chuo kikuu cha Nairobi, Dk. Ayah, anasema kuwa idadi ya sampuli hizo ni ndogo kutathimini mwenendo wa maambukizi ya Covid-19.

RAIS MAGUFULI ALIKUWA SAHIHI

Kulingana na matokeo ya utafiti huo, msimamo wa Rais Magufuli, wa kukataa kuweka mazuio kwa baadhi ya miji na kuzuia shughuli za kiuchumi ulikuwa sahihi.

Kiongozi huyo aliona hatua ya kuwazuia watu kufanya kazi na badala yake kuelekeza nguvu katika kupambana na virusi vya corona ni sawa na kuweka nchi katika hatari ya kuangamia na majanga mengine kama njaa na magonjwa.

Habari Kubwa