Kiama cha mwezi mmoja ujao dhidi ya maabara bubu mitaani

08Apr 2021
Yasmine Protace
Dar es Salaam
Nipashe
Kiama cha mwezi mmoja ujao dhidi ya maabara bubu mitaani

PANAPOKUWAPO maabara sehemu yoyote, huwa kuna maana ya kuwahudumia wananchi wa hapo au kutoka maeneo mengine.

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba katika Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Grace Magembe, akiongea na wamiliki wa maabara (hawapo pichani). PICHA: YASMINE PROTACE.

Maabara zimekuwa msaada tosha na kimbilio pale ambapo mtu anakwenda kwa ajili ya kupata huduma za kiafya.

Zipo maabara ndani ya zahanati, vituo vya afya na hospitali na zingine ambazo hazipo huko, ziko huru zinajitegemea.

Mkurugenzi wa Huduma na Tiba kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Grace Magembe, sasa anazitaka  maabara zilizojengwa katika makazi ya watu, kuwa na tahadhari ya kiafya, kwa jamii zinazozizunguka.

Anasema, serikali inazitaka kuwaangalia kwa karibu jamii jirani na na hasa watoto, kwani wanaweza kuchezea taka hatarishii, sambamba na wanajamii, kuwa makini na watoto wanaoweza kuchezea taka kujikuta wanakumbwa na magonjwa makubwa.

Kiongozi huyo anasema hadi sasa kuna kila sababu ya jamii kuwa makini na michezo ya watoto wanaocheza jirani na maabara, akitaja maabara kuna vipimo vingi vinavyochukuliwa kwa wagonjwa na taka zisipohifadhiwa vizuri, watoto wanaweza kupata magonjwa.

Hivyo anasema, maabara zinatakiwa kuwa katika maeneo ambayo hayataleta changamoto kwa wananchi wanaozunguka katika maeneo hayo.

Tahadhari yake ni kwamba maabara zinapofunguliwa katika makazi ya watu, ziko katika hatari ya kueneza madhara kwa watoto, kwani wanapenda kuchezea vihatarishi vya afya.

Kwa mujibu wa Dk. Grace, nia mojawapo bora ya kujihami na hatari hiyo ni maabara kujengwa mbali na makazi ya watu, kwani ujenzi au uzalishaji maabara mitaani, ni hatari iliyo jirani na umma.

MAABARA BUBU

Pia, Mkurugenzi ana dhamira ya pili, katika haya ya kupambana na maabara bubu, zinazotoa huduma na hatia ya sasa, serikali imezitaka hadi kufikia mwisho wa mwezi huu tarehe 30, ziwe zimesajiliwa na kama zitakuwa hazijasajiliwa, hatua kali dhidi ya wamiliki zitachukuliwa.

Dk, Grace  akizungumza katika mkutano na wamilikiwa maabara binafsi za Mkoa wa Dar es Salaam, anawataka wamiliki wa maabara bubu nchini ambazo hazijasajiliwa, wamepewa kipindi cha mwezi mmoja Aprili 30 wawe wamesajili ili kuepuka kufungiwa.

"Kumekuwapo maabara mitaani ambazo hazijasajiliwa na zinaendekeza kutoa huduma. Kinachotakiwa ni kuzisajili mpaka mwishoni mwa mwezi huu.

“Nimetoa maelekezo kwa Mratibu wa Maabara Mkoa wa Dar Es Salaam, kuhakikisha maabara zote ambazo hazijasajiliwa zipewe nafasi ya kusajiliwa hadi kufikia tarehe 30 mwezi Aprili.

“Kinyume na hapo zitafungiwa na wahusika kuchukuliwa hatua kwa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria,” anaagiza mkurugenzi huyo.

Dk. Grace, pia anakumbusha huduma za maabara kuwa nyeti na zinazohusika moja kwa moja na afya ya mwanadamu, hivyo pale zinapotoa majibu yasiyo sahihi, zinaweza kuhatarisha maisha ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa.

Mkurugenzi huyo anasema hadi sasa kuna baadhi ya maabara zisizo na wataalamu wenye vigezo vinavyotakiwa au kuwa na upungufu kulingana na kazi zilizopo.

Kutokana na uhalali huo, pia ameziagiza ndani ya mwezi mmoja unaotimu Aprili 30, wamiliki wa maabara hizo wawe wameshapata wataalamu wanaostahili kuwafanyia kazi hizo.

Dk. Grace anawataka viongozi wa ngazi mbalimbali za mitaa, vijiji na vitongoji kutoa taarifa kwenye mamlaka husika, endapo wataona kuna maabara zimeanzishwa katika maeneo yao ambazo hazijasajiliwa.

Msajili wa Maabara Binafsi, Dominic John, amesema lengo la mkutano huo ni kuwaleta wataalamu na wamiliki wa maabara wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja, ili waweze kupata miongozo na namna ya kuendesha maabara zao kwa usahihi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Habari Kubwa