Kichaa cha mbwa kinavyobaki janga la jamii mahali kote iliko

10Oct 2019
Yasmine Protace
Dar es Salaam
Nipashe
Kichaa cha mbwa kinavyobaki janga la jamii mahali kote iliko
  • Mbwa anayezurura hatari iliyojificha
  • Unapokuwa na jeraha kaa mbali naye
  • Kina miaka 87 nchini; tiba yake ni tishio
  • Nusu hadi theluthi ya watoto wagonjwa

KILA mwaka inapofika, tarehe 28 ya mwezi Septemba ni maadhimisho ya ‘Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani na kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Kichaa cha Mbwa: Chanja ili kukitokomeza.”

Mbwa wanaozurura ovyo mitaani ni hatari wa kichaa cha mbwa. PICHA: MTANDAO.

Huo ni ugonjwa ulioathiri maeneo mbalimbali duniani, hususan Bara la Asia na Afrika. Chanzo chake kinatajwa ni virusi kutoka jamii inayoitwa ‘lyssa’ ambavyo hukaa katika mate ya wanyama jamii ya mbwa walioathirika; mbwa, paka, mbweha na fisi wanaangukia kundi hilo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema kuwa maambukizi pale anapoumwa na mnyama aliyeathirika, huingia kupitia jeraha analopata.

Ummy anataja takwimu zilizopo kwamba, zinakadiria kiwango cha maambukizi ya kichaa cha mbwa duniani kinafikia vifo 59,000 kila mwaka, kati yake asilimia 36 ya athari hiyo inaangukia barani Afrika.

Pia, kuna makadirio mengine ya takwimu kimataifa kwamba, wastani wa kati ya asilimia 30 nusu ya waathirika wa kichaa cha mbwa ni watoto wenye umri chini ya miaka 15.

"Ugonjwa wa kichaa cha mbwa hauna tiba. Pamoja na kusababisha vifo, ugonjwa huo unaleta athari kubwa kiuchumi, kwani gharama ya chanjo kwa binadamu ni kubwa,” anasema Ummy.

Anafafanua: “Takriban Sh. 150,000 kwa mgonjwa kwa Bara la Afrika, ambayo ni sawa na asilimia sita ya mapato ya taifa katika bara hilo."

Waziri anarejea historia ya nchini Tanzania (tangu zama za Tanganyika), kwamba ugonjwa wa kichaa cha mbwa uliripotiwa kwa mara ya kwanza kati ya miaka ya 1932/33 na matukio yake yamedumu hadi sasa, ikiwa ni wastani wa miaka 87.

Hali ilivyo.

Mwaka huu 2019, kuanzia mwezi Januari hadi Agosti mwaka huu, kuna jumla watu 16,290 walioripotiwa kuumwa na mbwa na vifo vinane viliripotiwa kutokana na kichaa cha mbwa.

Ummy anasema, tatizo la kichaa cha mbwa ni kubwa zaidi ya takwimu hizo, kwani hazijumuishi vifo vinavyotokea nyumbani na waathirika wasiofika katika vituo vya kutoa huduma za afya.

Utafiti uliofanyika mwaka 2002 nchini Tanzania ulibainisha kulikuwapo takriban vifo 499 kwa mwaka, kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Anasema, tafiti zimeonyesha waathirika wakuu wa ugonjwa huo ni watoto chini ya miaka 15, kwa sababu ndio wanaokuwa karibu zaidi na mbwa anayefugwa, pia wanapenda kuchokoza mbwa wasiofahamu.

"(Virusi vyake) kichaa cha mbwa kinapoingia katika jeraha hushambulia neva (mishipa) za fahamu kutoka katika eneo la jeraha, kuelekea katika uti wa mgongo na hatimaye kuathiri ubongo," anasema.

Anaongeza kwamba, dalili za ugonjwa kichaa cha mbwa huanza kuonekana baada ya kuathirika kwa mfumo wa kati wa fahamu na baadaye ubongo.

Hapo ndipo mgonjwa anatawaliwa na dalili za kuwashwa sehemu ya jeraha, homa, kuumwa kichwa, maumivu ya mwili, kuogopa maji na mwanga, kutokwa na mate mengi mfululizo, kuweweseka (kushtuka mara kwa mara na kuogopa), kupooza na hatimaye kupoteza maisha.

Ummy anasema, kuna wakati watu huhusisha dalili hizo na imani za kishirikina, haloi inayowafanya wasiende katika vituo vya kutoa huduma za afya na wanaishia kutibiwa kienyeji hadi kupoteza maisha wakiwa majumbani.

Mlipuko & Kampeni

Anasema, Aprili mwaka jana, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro ilipata mlipuko wa ugonjwa huo na kusababisha vifo vya watu sita walioumwa na mbwa na kati yao, wanne walichelewa kwenda kupata chanjo ya kuzuia maradhi hayo na wakapaoteza maisha.

Waziri anaeleza udhibiti wake, tatizo hilo Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (OIE) na Shirika la Chakula Duniani (FAO), walishirikiana na serikali kupitia Dawati la Uratibu wa Afya Moja, ikatoa chanjo 33,700 kwa ajili ya kampeni ya kuchanja mbwa.

Kampeni ilifanyika tarehe 29 Aprili hadi 3 Mei, 2018, ambapo mbwa 15,314 na paka 1,057 walipatiwa chanjo katika wilaya hiyo.

Sambamba na hilo, elimu ya afya, ilitolewa kuhusu utoaji huduma ya kwanza kwa mtu aliyeumwa na mbwa na umuhimu wa kuwahi kupata chanjo.

Aidha, anasema mwaka huu ulitokea mlipuko mwingine katika Halmashauri za Wilaya za Ulanga na Malinyi ambao watu 292 waliumwa na mbwa na kati yao, wanne walipoteza maisha.

Katika kudhibiti mlipuko huu, kupitia Dawati la Afya Moja, Wizara ya Mifugo ilipata chanjo 16,000 kwa ajili ya kuchanja mbwa. Zoezi la kuchanja mbwa lilitekelezwa Mwezi Aprili hadi Mei, 2019.

Aidha, elimu ya kujikinga dhidi ya kichaa cha mbwa ilitolewa kwa shule za msingi na viongozi wa kata, ili kujikinga na kichaa cha mbwa.

Namna ya kujitibu, ni hatua ya kwanza muhimu ni kuosha jeraha kwa dakika 10 au zaidi kwa maji mengi yanayotiririka na sabuni na baada ya hapo kidonda kisifungwe.

Hatua inayofuata, inaelezwa ni kwa mgonjwa kupelekwa haraka katika kituo cha kutoa huduma za afya, ili kupata chanjo ya kichaa cha mbwa kwa kupatiwa dozi kamili.

Anafafanua kwamba, hadi sasa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inafafanua kwamba imekwishatolewa maagizo kwa mikoa na halmashauri kuhakikisha chanjo hizo zinakuwapo katika vituo vya huduma za afya, kwa wananchi wahitaji.

Ummy anasema, wanyama jamii ya mbwa na paka, daima wasiruhusiwe kulamba vidonda vya binadamu, kwani mate yao yana hatari ya kuambukiza, kwa waathirika.

Hatua muhimu

Rai yake ni kwa wamiliki kuzuia maradhi hayo mara moja kila mwaka na kupatiwa cheti cha chanjo na mbwa wadhibuitiwe na wasiachwe kuzurura ovyo, kwani wanapozurura, inakuwa rahisi kwamba kupata maambukizi kutoka kwa wanyama wenzao wanaoumwa.

Agizo la waziri linaenda mbali, kutaka watoto wapewe elimu stahiki na wakatazwe kuchokoza mbwa wasiowajua njiani, kama vile tabia ya kuwavuta mkia, masikio uya hata masihara ya kuwapandia mgongoni.

Ummy anasema katika utekelezaji mikakati ya pamoja kwa sekta zote zinazohusika kudhibiti ugonjwa huu, wizara yenye dhamana na afya nchini, inashirikiana na WHO, shirika la OIE na asasi zisizo za kiserikali kupitia uratibu wa dawati liitwalo ‘Afya Moja’ kuandaa
mkakati wa kitaifa wa kudhibiti kichaa cha mbwa wenye lengo kuu la kutokomeza ugonjwa huo nchini ifikapo mwaka 2030.

Ummy anasema, mkakati unasisitiza ushirikiano wa sekta mtambuka kitaifa kudhibiti kichaa cha mbwa, ikijumuisha hatua kama kuwachanja mbwa, kuhakikisha chanjo ya binadamu inapatikana katika vituo vya huduma za afya na elimu kwa umma inayozingatia dhana ya kujikinga.

Habari Kubwa