Kijana aliyeshangaza kuacha kazi ghafla, kajiajiri na kuajiri wengine

23Jul 2021
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Kijana aliyeshangaza kuacha kazi ghafla, kajiajiri na kuajiri wengine
  • Sifa yake; alithubutu zama ya corona

RICHARD Steven, kijana wa Kitanzania mwenye umri miaka 30. Kitabia, huwa ana uthubutu na ubunifu unaomuwezesha kutoa ajira kwa vijana saba, huku lengo lake ni angalau kutoa ajira 50,000 itakapotimu mwishoni wa mwaka huu.

Mizigo ikiwa ofisini, Sinza, Dar es Salaam. PICHA: FRANK MONYO.

Ni namna gani alianza ‘kuikokotoa’ fursa hiyo, katika kipindi cha mwanzo cha janga la corona, baada ya kubuni njia mbadala ya kuingiza kipato kwa kusafirisha mizigo midogo na mikubwa majumbani kwa wanaotuma na kutumiwa kutoka nje ya jiji la Dar es Salaam na hata nchi, akitumia usafiri wa mabasi. 

‘Dar Delivery’ ndio kampuni husika, ambayo mbali na kusafirisha mizigo, pia inasambaza kadi za harusi, chakula ndani ya Dar es Salaam na nakala za kiofisi kwa kutumia pikipiki.

“Msukumo wa ubunifu wangu ulikuja zaidi baada ya kukutana na changamoto ambayo kwangu nilichukulia kama fursa iliyotokea katika kampuni ambayo nilikuwa naifanyia kazi, ambayo ni kubwa Tanzania na Afrika Mashariki, na hapo nilikuwa nalipwa mshahara mkubwa,” anadokeza.

Richard anasema, mwanzoni hapakuwapo mtu aliyemuelewa sababu za kuacha kazi yenye maslahi makubwa, akijielekeza kwenda mtaani na wakati huo mazingira ya jamii kukabiliwa na janga la corona iliyojitokeza wakati huo.

Anasema, baada ya watu wengi kupunguza mizunguko kwa kuhofia maambukizi ya corona kipindi cha maradhi hayo, ndipo wazo jipya lilipozaliwa.

Richard anasimulia: “Nilikuwa na wazo, nikamshirikisha rafiki yangu wa karibu. Tukaamua kuanza kuishi kwenye wazo letu baada ya kuona fursa ni kubwa wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa corona, wananchi walipopunguza mizunguko na kukaa nyumbani (Lockdown).

“Wakati wa corona, watu walishindwa kutoka majumbani hapo ndipo lilikuja wazo la kuleta huduma ya ‘delivery’ (usambazaji). Baada ya majadiliano, tukaja na jina la Dar Delivery.

“Pia, tulifanya utafiti na kugundua kuwa mbali na ‘lockdown’ (vizuizi nyumbani), Dar es Salaam watu wengi wapo ‘busy’ (wametingwa) sana, tukasema huduma pekee tunayoweza kuwarahisishia ni suala zima la muda.

“Kwa hiyo, sisi ‘Dar Delivery’ tunatoa huduma mbalimbali, yaani mtu anaweza kutuagiza bidhaa yeye akaendelea na majukumu yake, sisi tukamletea hadi alipo,” anasema Steven.

AJIRA ILIVYO

Anasema kwa sasa kampuni hiyo ina wafanyakazi saba ambao kila mmoja amekabidhiwa pikipiki yake na kwa mwezi wanatumia zaidi ya Sh. milioni 2.3 kulipa mishahara ya vijana hao.
 
“Tulivyoanza tofauti na sasa. Awali tulikuwa tunakodisha pikipiki kwa ajili ya kusafirisha mizigo ya wateja wetu, lakini kwa sasa tunamiliki pikipiki ambazo vijana wetu wanazitumia kutoa huduma kwa wateja ndani ya Dar es Salaam,” anasema.

Anaongeza: “Mpaka sasa ukiachilia matumizi mengine, mishahara kwa wafanyakazi wa ‘Dar Delivery’ ni zaidi ya milioni 2.3, jambo ambalo tunajivunia kuweza kutoa ajira kwa vijana wenzetu,” anasimulia
 
SAFARI INAKOELEKEA

“Dar Delivery itafika mbali sana, kwani malengo yetu ni makubwa sana. Tunatamani kutoa ajira zaidi ya 50,000 kwa vijana hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu. Tuna mpango wa kumiliki ofisi yetu kubwa, kuwa na ‘Apps’ (Applications) ya ‘Dar Delivery’ ambayo itamsaidia mteja wetu kutuagiza mizigo yake wakati wowote,” anasema Steven.

Anasema gharama za kusafirisha mizigo zinategemeana na umbali ambao mteja yupo, ingawa anasema walichozingatia ni kuweka gharama ndogo ambazo hazitamuumiza mteja.

“Lengo letu ni kuwarahisishia watu kwenye hii huduma hasa suala zima la muda na ndio maana hata gharama zetu sio kubwa.

“Mfano, kuchukua mzigo mdogo Shekilango (Sinza – Dar es Salaam) kwenda Kariakoo ni Sh.4, 000 tu na hizi bei mara nyingi inategemea umbali na aina ya mzigo, mfano kuchukua simu Kariakoo hadi Mbezi Beach ni Sh. 5,000 tu,” anaeleza.

USAMBAZAJI KADI

Richard anasema huduma ya kusambaza kadi za harusi imetokea kupendwa na watu wengi, kwani ina tija kwa mahitaji yao.

“Unajua kwenye vikao vya mwisho vya harusi, changamoto kubwa ni watu kufika na kukabidhiwa kadi ya ukaribisho wa sherehe ya harusi. Sisi kazi yetu ni kuomba kazi hiyo ya kutumwa kusambaza, wanatupa namba ya simu ya mhusika na mahali alipo, sisi tunazifikisha kwa gharama nafuu,” anasema.
  
Msisitizo wake ni kwamba gharama za usambazaji kadi za harusi inategemea na idadi ya kadi na umbali wa eneo ambako inatakiwa kufikishwa ndani ya Dar es Salaam.

“Gharama huwa inategemea na idadi ya kadi, kwa hiyo kadi zikiwa nyingi gharama inapungua zaidi, ila zikiwa chache gharama inakuwa ya kawaida. Mfano mtu akiwa na kadi 200, tunasambaza kila kadi moja kwa Sh. 500 tu na hicho ni kiwango ambacho tunapendelea kusambaza,” Richard anaeleza.

Msisitizo wake ni kwamba kwa sasa wana mtandao mkubwa na washereheshaji ambao huwa wanawasiliana nao na kuwapa kazi, pamoja na kutembelea vikao vya harusi kwa lengo la kuomba kazi hiyo ya usambazaji.

Habari Kubwa