Kijiji kilichojitunuku na staili Utawala Bora wajinufaishe kwa uchumi

31Jul 2020
Beatrice Philemon
Tunduru
Nipashe
Kijiji kilichojitunuku na staili Utawala Bora wajinufaishe kwa uchumi
  • • Hifadhi misitu, mavuno yake kujenga kijiji
  • • Hujuma za wafugaji, wakulima bado shida

MIAKA 15 na ushee iliyopita, Tunduru ilikuwa wilaya ya mafichoni mkoani Ruvuma na penye hali duni kimaendeleo.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Mohamed Said, akionyesha ghala lililojengwa na kijiji cha Mindu, kwa ajili ya kuhifadhi mazao. . PICHA: BEATRICE PHILEMON.

Leo hii ikirejeshwa tamko hilo, mtu anapaswa kutafakari mara kadhaa ukweli huo, maana kuna kila sababu ya kuguna, ile kuwa historia.

Mkombozi nani?... Barabara ya lami!

Hapo ndiko kunapatikana kijiji cha Mindu, umbali wa maili 40 (kilomita 24.86), kutoka mjini Tunduru akiwa na wasifu wa kubarikiwa utajiri wa misitu ya asili, katika Msitu wa Hifadhi uliogeuka mzizi wa mapato kwa ajili ya maendeleo ya wanakijiji.

Pia, shambani kuna mazao ya biashara kama ufuta, choroko, mbaazi na korosho, vyote vikiwafanikishia kupata zahanati, shule ya msingi na sekondari .

Ni namna gani juhudi za kujiongeza zinafanyika mahali hapo kugeuza utajiri huo kuwa mali ya asili? Darasa linaanzia katika mafunzo ya utawala bora kijijini, ambayo sasa yanawaletea mabadiliko makubwa kiuchumi na kijamii na manufaa kujumuishwa hata kwa Halmashauri ya Wilaya Tunduru.

KATIBU KIJIJI

Mwandishi wa Nipashe aliyezuru kijijini hapo hivi karibuni alikutana na Katibu wa Maliasili ya Kijiji cha Mindu, Angelelus Macha, anayetamka: “Bila utawala bora, kijiji hakiwezi kutumia rasilimali za misitu au fedha za kijiji kwa faida ya umma, vinginevyo kutakuwa na ubadhirifu.”

Anasema, mafunzo ya utawala bora waliopata kutoka Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), umewafanikisha kutumia vyema rasilimali msitu yao.

Kutokana na matumizi mazuri ya fedha , hivi sasa wamefanikiwa kujenga ghala la kuhifadhi mazao ambalo hivi sasa limeanza kutumiwa na vyama vya ushirika vya msingi vya mazao (AMCOS), wanaovuna mazao na kupitia ghala lao, kijiji kinapata fedha kutokana na ushuru wa kuhifadhi mazao.

Mpango ulioko hivi sasa ni kwamba wanajenga shule ya sekondari ya kata, ambayo tayari ina vyumba vitano vya madarasa, ofisi moja na matundu sita ya choo.

Msitu wa Hifadhi ya Kijiji Liwina, kilichoko katika ndani ya kijiji Mindu kilichoanzishwa mwaka 1974 katika zama za ‘operesheni vijiji’ nchini, kina jumla ya wanavjiji 1867 una hekta 3,713 ya misitu ya asili.

Macha anasema kuwepo uwazi kwenye mapato yanayotokana na mazao ya misitu na vyanzo vingine vya kijiji, taarifa zake za mapato na matumizi, husomewa wanakijiji kila baada ya miezi mitatu, kupitia Mkutano Mkuu wa Kijiji kwa wananchi.

“Sisi kama kijiji tuna vyanzo vingi vya mapato ikiwamo ushuru wa minara ya simu, ruzuku kutoka halmashauri na faini zinazotozwa kwa wafugaji wanaoingiza mifugo ndani ya msitu wa hifadhi ya kijiji kwa ajili ya malisho na makazi,” anasema Macha.

Anaeleza, wamefanikiwa katika suala la usimamizi na hifadhi misitu, ila bado wanakwama katika mikasa ya ng’ombe wanaoingizwa msituni, wakilalama faini na wanazotozwa wafugaji na baadhi ya matukio kupotosha haki ya kijiji.

Malalamiko yake ni kwamba hivi sasa wanavijiji wa Mindu, Namakambale na Songambele wanafanya kazi katika mazingira magumu, wakidai mifugo inaingizwa msituni na baadaye wamiliki kutozwa faini.

MIKASA

“Mwaka 2018 tulikamata wafugaji wawili kutoka kijiji cha mindu wakilisha mifugo ndani ya Msitu wa Hifadhi ya Kijiji unaoitwa Liwina ‘Forest Reserve’ kinyume cha sheria,” anasema.

Macha anasimulia tukio la mfugaji wa kwanza, alikamatwa na ng’ombe 200 na alipopelekwa katika Kituo cha Polisi jirani alitakiwa kulipa faini ya Sh. milioni mbili baadaye alitoroka.

Anataja mfugaji mwingine, pia alinaswa na ng’ombe 300 katika Msitu wa Liwina na anasimulia: “Tulimkamata mfugaji huyu tukiwa kwenye doria katika msitu wetu wa hifadhi.

“Tulikuwa tunafanya doria ili kukamata wavamizi au waharifu wanaovamia msitu kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji wa ng’ombe, malisho na utengenezaji wa mbao.”

Kwa mujibu wa Macha, viongozi wa kijiji wamehangaika kufuatilia malipo katika mamlaka za kisheria, pasipo mafanikio, hali inayofanya kijiji kutofanikiwa na malipo, ambayo ni sehemu ya mapato wanayotarajia kusaidia kujenga shule ya sekondari.

“Tunataka (mfugaji) akamatwe tena, kwa sababu mwaka jana mwezi wa 12 tulikutana naye na kumuuliza faini yetu atalipa lini?

“Akasema tayari ameishalipa Sh. 500,000 kwa… Sisi kama wanakijiji hatuna uhakika na anachosema kwa sababu mpaka sasa hakuna hela yoyote iliyolipwa serikali ya kijiji,” anasema.

Rai yao wananchi hivi sasa ni kusaidiwa katika madai hayo anayodai inawafanyisha kazi ya uhifadhi na usimamizi wa misitu katika mazingira magumu.

“Kwanza hatupati posho na fedha tunayoipata kutokana na faini zinazotozwa kwa wafugaji, zinatumika katika maendeleo ya kijiji, masuala ya uhifadhi wa misitu na kufanya doria,” anasema Macha.

Hivi sasa viongozi wa kijiji wanasema wameandika barua kuhusu suala hilo na kuipeleka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru tangu Juni 15 mwaka huu, yenye nakala kwa Mkuu wa Wilaya na ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ili wawasaidie kwa hatua stahiki ichukuliwe dhidi ya suala hilo.

MTENDAJI KIJIJI

Ofisa Mtendaji wa Kijiji, Mohamed Said, anasema msitu wa Liwina unaharibiwa na wafugaji kutokana na ubishi wao katika ulipaji faini.

“Tunaomba serikali ifuatilie ambaye amesababisha kijiji kupata hasara, kwa sababu hata Ofisa Misitu, pia hakuwa na ushirikiano mzuri kwenye ufuatiliaji wa suala hili,” anasema Saidi.

Anataja manufaa waliofaidika na utawala bora kijijini hapo, mwaka 2017 kijiji kiliuza mbao zenye thamani ya Sh. milioni 5.2 na kutumia fedha hizo kujenga ghala la kuhifadhia mazao na fedha zilizobaki walitumia kuhifadhi misitu.

Anaorodesha manufaa ambayo ni kujengwa madarasa matano, ofisi moja ya walimu, matundu sita ya vyoo na hadi sasa bado wanahitaji vyumba vitatu vya madarasa na ofisi ya walimu kuwawezeshea mazingira mazuri ya kusoma, yatakayowasaidia kupata matokeo mazuri.

“Shule hii ni mpya, imeanza ujenzi mwaka 2019 na itakuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 800 hadi 1000, kuanzia ‘form one hadi four’…” anasema.

WAJUMBE MALIASILI

Mjumbe wa kamati ya Maliasili ya Kijiji cha Mindu, Edmund Komba, anasema uhifadhi wa msitu unawanufaisha na kuwepo mvua ya kila mara, inayowanufaisha katika kilimo na ustawi misitu.

“Watu wakivamia msitu na kuharibu, sisi hatunufaiki chochote. Kwa, mfano kama huyo aliyechukua hela yetu hiyo, ni rushwa, anatukatisha tamaa katika uhifadhi wa misitu. Ushauri wetu serikali itusimamie twende bega kwa bega ili tupate hela yetu ya kijiji,” anasema.

Komba hivi sasa uongozi wa kijiji unahangaika kupata Sh. milioni tatu kutoka kwa mfugaji ndiyo maana wanakijiji wanaomba serikali iingilie kati, ili wapate Sh. milioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya kata na miradi mingine ya kijiji.

Christina Zuberi, ni Mjumbe wa Kamati ya Maliasili Kijiji cha Mindu, anasema Msitu wa Liwina wameshavuna mara moja tu na kupata hela na tayari wameshanufaika.

“Kutokana na usimamizi wa msitu tulifanya doria kwa watu waliokuwa wanavuna mbao, tulishika mbao tukaziuza na kupata fedha za kujenga ghala,” anasema.

Anasema watu wanachoma moto msituni, wanalisha mifugo ndani ya msitu na ndio ya vyanzo vya maji, ombi letu tusaidiwe kusimamia msitu yetu.

Hamza Mohamed, Mjumbe wa Kamati ya Maliasili ya Kijiji Mindu, anasema huwa wanafanya doria msituni na wastani wa mara kadhaa kila mwezi.

“Mifugo ipo mingi sana inaharibu vyanzo vya maji, nyasi hakuna zinakauka, hakuna amani kwenye msitu wetu, kwa sababu wanakata miti kwa ajili ya makazi ya mifugo yao,” anasena na kuongeza:

“Hivi sasa kuna eneo kubwa la msitu ambalo limeishaharibiwa na wafugaji na hatujui wanatoka wapi.”

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Augustino Andrea, anasema wafugaji wameharibu mazingira ya msitu unaonaza kutoweka kutokana na uvamizi kilimo.

“Viongozi wetu wanakuja, kinachopatikana wanachukua wanaenda kutengeneza kwao, wanajinufaisha wenyewe,” anasema.
Klio chake ni ugumu katika ufanyaji doria, kwani hawana fedha za kuwalipa wajumbe wanaofanya doria.

OFISA TARAFA

Nipashe ilizungumza na Ofisa Misitu Tarafa, Stanley Balueshi, anayekana dai la wafugaji walikamatwa msituni kumataifa fedha akitamka ‘ni uongo.’

“Sijachukua hela yoyote kutoka kwa mfugaji, kwanza mimi ndiye niliyemkamata mfugaji akiwa anapitisha ng’ombe kutoka kijiji cha Mkowela kwenda kijiji cha Tinginya, nikiwa na watu wa Shirika la Mpingo. Tulikuwa tunatoka kijiji cha Ng’apa kwa ajili ya shughuli zetu kiofisi,” anasema.

Anasema baada ya kumkata walimpeleka Kijiji cha Mindu kumsajili na kisjha mchakato wa kisheria ulichukua mkondo wake kisheria.

Habari Kubwa