Kikombe, kifaa cha hedhi aina yake

16Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Nakuru
Nipashe
Kikombe, kifaa cha hedhi aina yake

SHIRIKA lisilo la kiserikali la mjini hapa, limezindua mpango wa kusambaza na kuhimiza matumizi ya vikombe maalum vitakavyotumika kwa kinamama wakati wa hedhi, kama njia ya kukabiliana na maradhi na kuwapunguzia gharama za kila mwezi.

Kinamama wakifunzwa kutumia kifaa hicho. PICHA: MTANDAO

Ni mradi unaoelezwa kuungwa mkono na serikali kama anavyosema mwakilishi wake Dk. Torome Kochei, kutoka Wizara ya Afya, anayeutaja kuwa mradi wa kipekee utakaowasaidia na hali zao kijinsia.

Anasema ni kifaa cha kipekee kinachozingatia usafi kwa wasiomudu mbadala, ikizingatiwa suala la hedhi kwa wenye kipato kidogo imekuwa tatizo kubwa kwa jamii nyingi nchini Kenya.

Mary Muthoni, ni miongoni mwa kinamama vijana walioshawishika kukitumia kifaa hicho, anakiri mwanzoni alikiona kifaa hicho ‘jambo geni,’ lakini sasa amebadili mtazamo wake.

Ni kifaa chenye muundo kama wa chombo cha kukinga mafuta katika chupa na kimetengenezwa kwa mpira laini, mtumiaji anahitajika kukisafisha bila kutumia dawa za kuua viini kila anapokitumia.

Mary anaeleza kuwa mwanamke anayeweza kukitumia hadi saa 12 kwa wakati mmoja, na salama kutumiwa usiku na mchana.

Shirika la Hope in Life kwa ushirikiano na wakfu wa Sulwe wameanzisha mradi wa kutoa mafunzo na kusambaza kifaa hicho cha hedhi kwa kinamama wachanga hasa wanaokabiliwa na changamoto za kifedha.

Habari Kubwa