Kikongwe aanza kulia baada ya kifo kumsahau

09Feb 2016
Nipashe
Kikongwe aanza kulia baada ya kifo kumsahau

Mwezi Mei mwaka jana, alionyesha huzuni na kulalamika tu kwamba malaika wa kifo amemsahau, watu wakaona kama utani, lakini sasa wameanza kumuelewa kwamba anatamani sana kufa. Ameanza kulia kutwa nzima, anataka afe.

Huyu ni mzee Mahashta Murasi, fundi viatu aliyestaafu kazi hiyo mwaka 1953, wakati alipokuwa na umri wa miaka 122.

Amechoka kuishi, hana dada wala kaka waliyezaliwa naye tumbo moja. Hata vitukuu vyake wanaomtunza hivi sasa, anawaona kama watu baki tu. Anataka afe akaungane na rafiki zake katika ulimwengu mwingine.

Akiwa na umri wa miaka 181 sasa, mzee huyo aliyezaliwa mwaka 1835, anatajwa na kitabu cha Guinness World Records kuwa ndiye mwanadamu pekee mwenye umri mrefu miongoni mwa wanadamu wote walio hai kwa sasa.

Alizaliwa katika mji wa Bangalore nchi India na kuishi kwenye mji huo akiwa mtoto mpaka mwaka 1903 alipohamia mji wa Varanasi, alikofanya kazi ya ufundi viatu mpaka alipostaafu mwaka 1957.

Mwaka jana, alipozungumza na waandishi wa habari, alionyesha huzuni kubwa huku akisema: "Nimeishi na kushuhudia vifo vya watoto wa vitukuu vyangu wengi. Mmoja wao alifariki miaka michache iliyopita."

"Wenzangu wengi tuliocheza nao utotoni na niliofanyakazi nao na wale tuliokuwa tukishirikiana nao kwenye umri wa uzee wamefariki na kuniacha" anasema na kuongeza kwa masikitiko: "Nahisi malaika mtoa roho amenisahau na sijui lini atanikumbuka."

Mwaka huu, 2016, mzee huyo ambaye bado anakumbukumbu nzuri, ameyarudia tena maneno yake ya kutaka kufa lakini huku akiwa anabubujikwa na machozi. Anamlilia malaika mtoa roho aje amchukue. Amechoka kabisa kuishi.

"Wenzangu wengi waliishi hadi miaka 150, hakuna aliyefikisha miaka 170, kwa nini malaika wa kifo haji kunichukua? Amenisahau, au?" Amesema mzee huyo huku akilia na kuongeza kuwa:

"Najiona kama sio tena mwanadamu, ila ni kidubwasha fulani kinachoishi."

Kwa mujibu wa mtandao wa WorldNewsDailyReport.com, umri wa mzee Murasi unathibitishwa na hati kadhaa zinazotambulika kiserikali.

Mbali ya kuwa na umri mkubwa, mzee huyo pia analalamikia hali ya kutougua maradhi yoyote kama binadamu wengine kwa sababu mara ya mwisho kabisa aliugua mafua mwaka1970, yaani miaka 45 iliyopita.

Habari Kubwa