Kili Stars kurudi ya 1994 Kombe Chalenji Kenya

04Dec 2017
Adam Fungamwango
Nipashe
Kili Stars kurudi ya 1994 Kombe Chalenji Kenya

MICHUANO ya Kombe la Chalenji kwa nchi za Ukanda wa Afrika  Mashariki na Kati, imeanza nchini Kenya.

Kikosi cha Tanzania Bara kimepangwa na timu za Zanzibar Heroes, Libya, Rwanda na wenyeji Kenya.

Pamoja na kupangwa kwenye kundi gumu, lakini matarajio ya  mashabiki wengi ni kwamba kikosi cha Tanzania Bara ambacho  kinajulikana kama Kilimanjaro Stars ni kufanya vizuri.

Na hii ni kwa sababu ya kuwa na kikosi chenye wachezaji wazuri,  wenye uwezo wa hali ya juu ambao wanatamba kwenye Ligi Kuu  Tanzania Bara.

Kwa miaka ya karibuni, Tanzania imeanza kupata wachezaji wenye uwezo na vipaji vya hali ya juu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,  kiasi kwamba wameanza kumezewa mate na kusajiliwa kwenye ligi mbalimbali Afrika na nje ya Bara hili.

Kingine ni kwamba Tanzania Bara ilishawahi kutwaa kombe hilo  mwaka 1994 michuano hiyo ikichezwa huko huko nchini Kenya na iliondoka ikiwa  haitarajiwi kufanya vema, hivyo baadhi wanaona kama historia  inaweza kujirudia.Chini ya Kocha Mkuu Ammy Ninje, kama Tanzania Bara itatwaa  kombe hilo itakuwa ni mara ya sita.

Hadi sasa imelishatwaa kombe hilo mara tano. Mara tatu wakati ikiitwa  Tanzania Bara na mara mbili kabla ya nchi kupata uhuru wakati  huo ikiitwa Tanganyika.

Timu hiyo ilianza kucheza michuano hiyo kwa mara ya kwanza mwaka  1945.

Michuano hiyo ilianzishwa mwaka 1926 ikiitwa Gossage Cup  kutokana na kudhaminiwa na kampuni ya sabuni, iliyokuwa ikimilikiwa na mzungu William Gossage.

Mwandishi wa makala haya amekusanya rekodi ya miaka ambayo Tanzania Bara ilifanikiwa kutwaa ubingwa na jinsi ilivyoutwaa kabla na baada ya uhuru.

1. Tanganyika 2-0 Kenya-1949 (Zanzibar)Mwaka 1949 ndiyo kwa mara ya kwanza Tanzania Bara wakati huo  ikiitwa Tanganyika kwa sababu ilikuwa haijapata uhuru, ilitwaa  Kombe la Chalenji wakati huo likiitwa Gossage Cup.

Michuano ilichezwa mjini Zanzibar. Tanganyika iliifunga Uganda kwa mikwaju ya penalti, huku Kenya ikiichapa Zanzibar, hivyo fainali ilikuwa ni kati ya Tanganyika na Zanzibar.

Desemba 8, 1949 fainali hiyo ilichezwa na Tanganyika kushinda  mabao 2-0 yaliyofungwa na Paulo na Juma Abdullah.

2. Tanganyika 3-2 Kenya-1951 (Tanganyika)Baada ya kuukosa kwa mwaka mmoja wa 1950, mwaka 1951 ilifanikiwa kutwaa ubingwa, ikiwa ni mara ya pili tangu ianze kushiriki michuano hiyo. 

Michuano hiyo ilichezwa jijini Dar es Salaam huku fainali kwa mara nyingine tena ilikuwa ni kati ya Tanganyika na Kenya. Tanganyika ilishinda kwa mabao 3-2, fainali ikichezwa Septemba 29, 1951 jijini Dar es Salaam.

Nasson alifunga mabao mawili, Kambi akifunga moja kwa upande wa Tanganyika, huku Elijah akiifungia Kenya na moja la kujifunga wenyewe kwa wenyeji, kupitia kwa beki wao Hamid.

3. Tanzania Bara 4-3 Uganda-1974 (Tanzania)Ilikuwa ni mwaka 1974, Tanzania Bara ilipokuja tena kuchukua Kombe la Chelenji. Tayari wakati huo nchi ilikuwa imeshapata uhuru mwaka 1961 na kuungana na Zanzibar mwaka 1964, hivyo sasa kutumia jina la Tanzania Bara.

Kulikuwa na makundi mawili, A likiwa na Tanzania Bara, Kenya na  Zambia, huku Kundi B likiwa na timu za Uganda, Zanzibar na  Somalia. Timu moja iliyoshika nafasi ya kwanza kila kundi iliingia  fainali ambazo ni Tanzania Bara Kundi A na Uganda Kundi B.

Timu hizo zilitoka sare ya mabao 1-1 kwa dakika 90, lakini  Tanzania Bara ilitwaa ubingwa kwa mikwaju ya penalti 5-3.

4. Tanzania Bara 4-3 Uganda-1994 (Kenya)

Miaka 20 baadaye, mwaka 1994, kilichokuja kutokea kilikuwa ni  kama marudio tu ya kile kilichotokea mwaka 1974 nchini Tanzania.

Tanzania Bara ilitwaa Kombe la Chalenji kwa staili ile ile dhidi ya timu ile ile ya Uganda na kwa idadi ile ile ya mabao ya penalti.

Tofauti ndogo ilikuwa ni idadi ya mabao ndani ya dakika 90 badala ya 1-1 kama ilivyokuwa mwaka 1974, ikawa 2-2, lakini pia  tofauti nyingine ilikuwa ni nchi iliyofanyikia michuano hiyo.

Mwaka 1974 ilikuwa ni Tanzania, lakini mwaka huo ilikuwa nchini  Kenya. Fainali ilichezwa jijini Nairobi Desemba 10, 1994, mabao ya  Bara yakifungwa na Juma Amir Maftah na Said Mwamba 'Kizota',  huku ya Uganda yakifungwa na Idd Batambuze na George  Semogerere. Bara ilitwaa kombe kwa mikwaju 4-3 ya penalti, huku Nteze John akiibuka kuwa mfungaji bora, akiwa ameziona nyavu mara nne.

5. Tanzania Bara 1-0 Ivory Coast-2010 (Tanzania)Tanzania Bara ilitwaa Kombe la Chalenji mara ya tano na ya mwisho  mwaka 2010, michuano iliyofanyika nchini Tanzania.

Ni miaka saba sasa imepita timu hiyo haijatwaa tena kombe hilo.

Kwenye mechi hiyo iliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es  Salaam, Tanzania Bara iliifunga timu mwalikwa ya Ivory Coast bao 1-0.

Bao hilo lilifungwa na nahodha wa Taifa Stars na timu hiyo wakati  huo, Shadrack Nsajigwa kwa mkwaju wa penalti dakika ya 41 ya  mchezo.

 

Habari Kubwa